Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho: Nimepata mashine tu msimu ujao

Robertinho X Bocco Kocha wa Simba Robert Oliviera "Robertinho"

Fri, 23 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kiu ya mashabiki wa Simba kwa sasa ni kutaka kujua mastaa wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao, mbali na zile 'thank you' wanayopewa wale wanaotemwa kwenye kikosi cha sasa, lakini kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' amewaambia 'tulieni kuna vyuma vinasaini', kisha akaomba apewe wiki tano kwenye kambi ya maandalizi ya msimu (pre season) waone mambo.

Wanasimba wamekosa utulivu kwa sasa kutokana na misimu miwili kushuhudia timu yao ikishindwa kubeba taji lolote mbele ya watani wao, Yanga ambao walienda mbali kimataifa kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuwatambia huko mtaani.

Hata hivyo, Robertinho amekuwa na mipango mingi mizuri aliyoiwasilisha mezani kwa mabosi wa klabu hiyo, kuhakikisha vinaletwa vyuma vya maana ili kurejesha heshima ya timu hiyo ndani ya anga za kimataifa na baadhi yao wameshasainishwa na kumpa faraja kubwa kocha huyo.

Akiwa kwao Brazili, Kocha Robertinho amechekelea ripoti ya mabosi wake ya kuwasainisha mastaa wapya akisema hadi sasa mwendo ni mzuri katika kumletea watu ambao watairudisha heshima ya wekundu hao kuwania mataji akitamba tayari wameshamnasa winga mmoja wa kazi anayejua kufunga.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia simu kutoka Brazili, Robertinho alisema hadi mabosi wake watakapomaliza usajili alioupendekeza basi Wanasimba watakuwa na kila sababu ya kutembea kifua mbele kwani sasa atakuwa anahitaji wiki tano pekee za kuingia kambini Ulaya kukipika kikosi hicho.

Alisema anaamini muda huo utakaokwenda sambamba na kuwalisha mbinu na mazoezi ya maana itasaidia kurudi kwenye mashindani ikiwa na operesheni kabambe ya kurejesha mataji Msimbazi kwa msimu ujao baada ya msimu huu kubugi kidogo katika Ligi Kuu, ASFC na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imepanga kwenda kuweka kambi katika nchi ya Uturuki kujiandaa na msimu mpya wakiachana na kambi za Afrika kwa muda baada ya kuweka kambi Misri msimu uliopita.

"Kawaida tunahitaji wiki nane kujiandaa na msimu mpya, lakini kutokana na ishu ya muda, mimi hata nikipata wiki tano tu zinatosha kabisa kumaliza kazi ya kutengeneza timu," alisema Robertinho ambaye hajapoteza mechi yoyote ya ligi msimu uliopita na kuongeza;

"Nafurahia kazi ya viongozi wangu huko Tanzania, ripoti wanayonipa inanipa raha mpaka sasa tuko salama kuwapata mastaa wote ambao tumewataka kwa ajili ya kuijenga timu mpya. Tumeshampata mshambuliaji ambaye pia anaweza kucheza kama winga niliyekuwa namhitaji nadhani kwa rekodi zake zinazozijua sasa ni wakati wake kuja kuyaleta makali hayo hapa Simba."

Japo Robertinho hakuanika jina la nyota huyo aliyefurahishwa kusajiliwa kwake, lakini Mwanaspoti linafahamu Simba imemsainisha miaka miwili nyota Mcameroon, Leandre Onana aliyefunga mabao 16 katika Ligi Kuu ya Rwanda akiwa na Rayon Sports akimudu kucheza winga na straika.

Kwa ratiba ya kambi ya Simba ya maandalizi ya msimu, Robertinho alisema Simba itahitaji mechi zisizopungua nne za kirafiki zitakazokuja kupima kwa nyakati tofauti ubora wao kabla ya kurudi nchini.

"Tutaanza na mechi nyepesi zaidi na baadaye tunaweza kucheza na timu za daraja la katikati na ile wiki ya mwisho tunaweza kuanza kucheza na timu ngumu, nitafurahi kama tutakapokwenda litakuwa eneo la kutupa mechi za namna hiyo."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: