Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi 5 za kibabe Simba ikitinga robo fainali CAF

Simba Wapigwa 3 Rekodi 5 za kibabe Simba ikitinga robo fainali CAF

Mon, 20 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa mara ya nne, timu ya Simba imefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa kwa kipindi cha miaka mitano.

Juzi imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipoirarua bila huruma, Horoya AC ya Guinea mabao 7-0 mechi ikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tatu na mara moja Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa kipindi chote hiki, Simba ilikuwa inatinga vipi kwenye hatua hiyo? Makala haya yanakuletea hatua zote ambazo timu hiyo ilikuwa inatinga, huku baadhi ya wachezaji wakiweka rekodi mbalimbali.

Mara tatu robo Ligi ya Mabingwa

Mara ya kwanza Simba kutinga hatua hiyo ilikuwa ni Machi 16, mwaka 2019, ilipoifunga AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa yaliyofungwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Clatous Chama, huku wageni wakianza kutangulia kwa bao la Kazadi Kasengu ambaye kwa sasa yupo Singida Big Stars.

Simba ilikuwa Kundi D, ikasonga mbele kwa pointi tisa, ikifungwa mabao 5-0 mara mbili na timu za Al Ahly ya Misri na AS Vita Club ikiwa ugenini, na mabao 2-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria, lakini ikapiga hesabu zake vema kama kawaida kwenye uwanja wa nyumbani, ikaichapa JS Saoura mabao 3-0, Al Ahly ikafa bao 1-0, kabla ya kutinga hatua hiyo kwenye mechi dhidi ya AS Vita.

Msimu wa 2020/21, Simba ilirudia tena ilichokifanya 2019, ilipofanikiwa kutinga robo fainali hapo hapo kwa Mpaka, ikiifunga tena timu hiyo hiyo ya AS Vita Club, Aprili 3, 2021, lakini safari hii mabao 4-1.

Safari hii tena, Simba ilipangwa kundi moja na Al Ahly pamoja na AS Vita Club, kilichobadilika ni timu moja, badala ya JS Saoura, ikaingia Al Merrikh ya Sudan, pia idadi ya mabao, kwani Wakongo walikufa mabao 4-1 kwa Mkapa.

Yalikuwa ni mabao mawili ya Chama dakika ya 45 na 84, Luis Miquissone na Rally Bwalya dakika ya 66 yaliyoipeleka hatua hiyo.

Ikikwa kwenye Kundi A, Simba safari hii haikuwa ya pili, badala yake ililiongoza kundi ikiwa na pointi 13, Al Ahly ambayo ilikwenda kutwaa ubingwa, ilikuwa chini yake ikikusanya pointi 10.

Simba ilishinda ugenini bao 1-0 dhidi ya AS Vita Club, ikaichapa Al Ahly bao 1-0 nyumbani, suluhu ya ugenini dhidi ya Al Merrikh, ikawachapa Wasudan hao mabao 3-0 nyumbani, ikapoteza bao 1-0 nchini Misri dhidi ya Al Ahly, kabla ya kuifanya tena ngazi As Vita Club kwa mara nyingine.

Juzi ilikuwa ni mara ya tatu, ilipata ushindi mnono wa mabao 7-0, yaliyofungwa na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Mzambia Clatous Chama ndiye aliyeongoza mauaji ya jana, akifunga mabao matatu 'hat-trick', straika raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jean Balake na Saido Kanoute raia wa Mali wakifunga mabao mawili kila mmoja.

Imefikisha pointi tisa ambazo hazitofikiwa na Horoya wala Vipers, hivyo kutoka Kundi C msimu huu, imekwenda Simba na Raja Casablanca ya Morocco.

Mara moja Kombe la Shirikisho

Msimu wa 2020/21, Simba ilitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kwa namna iliyowashangaza wengi na timu dhaifu ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ikaangukia kwenye Kombe la Shirikisho ambako nako ilifanikiwa pia kufika hatua ya robo fainali.

Ikiwa Kundi D, ilifanikiwa kushika nafasi ya pili chini ya RS Berkane ambayo ilikwenda kutwaa kombe hilo, zote zikimaliza na pointi 10.

Mechi iliyoipeleka Simba hatua hiyo ilichezwa Aprili 3, 2022 Uwanja wa Benjamin Mkapa iliivurumisha US Gerndamerie ya Niger mabao 4-0, yaliyowekwa wavuni na Chris Mugalu aliyefunga mawili dakika ya 68 na 78, Sadio Kanoute dakika ya 63, na moja wakijifunga wenyewe.

Mabao mengi mechi moja

Mpaka sasa Simba imeweka rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi kwenye mechi moja, katika hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa msimu huu.

Kabla ya mechi ya juzi, ni mechi mbili ambazo zilikuwa na ushindi mkubwa kwa timu, kwenye kundi hilo hilo, Raja Casablanca ya Morocco iliifunga Vipers ya Uganda mabao 5-0 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliiadhibu Al Ahly mabao 5-2 kwenye Kundi B.

Chama mfalme wa robo fainali

Kiungo Mzambia, Clatous Chama, ameweka rekodi ya kufunga mechi zote ambazo Simba ilikuwa inahitaji ushindi kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kufanikiwa kuivusha.

Machi 16 mwaka 2019, ilipoifunga AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mabao 2-1 alifunga bao la pili dakika ya 90, 2021 ilipoifunga AS Vita Club 4-1, akifunga mabao mawili na juzi alifunga 'hat-trick', mechi ambazo zote ilifanikiwa kupita hatua za makundi.

Chama pia anafunga 'hat-trick' ya pili kwenye mechi za hatua ya makundi, nyingine ikiwekwa na Mahmoud Kahraba wa Al Ahly, Machi 17, mwaka huu akiipa ushindi wa mabao 4-0 timu yake dhidi ya Coton Sport ya Cameroon.

Kanoute naye wamo

Si mara nyingi kuona Kanoute akifunga mabao, lakini mchezaji huyo raia wa Mali ameweka rekodi ya kuwa mmoja wa wafungaji wa mabao yaliyoipeleka Simba robo fainali kwenye mechi za kimataifa mara mbili.

Wakati Chama akiweka rekodi hiyo mara tatu kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika tu, Kanoute amefanya hivyo juzi na mechi za Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu uliopita.

Aprili 3, 2022 dhidi ya US Gerndamerie ya Niger mabao 4-0, alifunga bao moja, likiwa ni moja ya mabao yaliyoiwezesha Simba kwenda robo fainali na juzi alifunga mawili.

Kwa matokeo hayo, sasa Simba inasubiri kukamilisha tu ratiba ya michuano hiyo hatua ya makundi kwa kucheza mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Raja Casablaca ya Morocco Machi 31, mwaka huu, kwani timu hizo tayari zimefuzu.

Katika Kundi C, Horoya AC na Vipers ambazo zitakutana mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi, hakuna inayoweza kufikia pointi tisa ilizonazo Simba lakini pia Wekundu wa Msimbazi hao hata kama wataifunga Raja Casablanca Machi 31, hawawezi kufikisha alama 13 walizonazo Wamorocco hao.

Kwa mantiki hiyo, Raja Casablanca inatinga robo fainali ikiwa kinara wa Kundi C, wakati Simba ikienda ikiwa nafasi ya pili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: