Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Profesa na tahadhari kubwa Sauzi

YANGA NABI Vg Profesa na tahadhari kubwa Sauzi

Tue, 16 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi, amesema anatarajia upinzani mkali kutoka kwa Marumo Gallants katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans itakuwa mgeni katika mchezo huo utakaopigwa kesho Jumatano (Mei 17) katika Uwanja wa Royal Bafokeng uliopo Rustenburg, Afrika Kusini, huku ikihitaji sare yoyote ama kutokubali kufungwa zaidi ya bao moja ili kutinga fainali ya michuano hiyo na kuandika rekodi ya klabu, tangu kuanzishwa kwake miaka 88 iliyopita.

Hiyo ni kutokana na kushinda mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali Jumatano iliyopita kwa mabao 2-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Nabi amesema kwa sasa anaendelea kuwaongezea wachezaji wake umakini na kutumia vema nafasi wanazotengeneza ili kutafuta bao la mapema katika ardhi ya Afrika Kusini jambo litakalowachanganya Marumo Gallants.

Amesema anajua ubora wa wapinzani wao wanapokuwa nyumbani na wanahitaji kutumia madhaifu yao hasa katika safu yao ya ushambuliaji kutafuta bao la mapema katika kipindi cha kwanza.

Amesema ameona madhaifu ya mpinzani wao huyo hasa katika safu ya ulinzi, lakini akiwataka mabeki wake kuwa makini kutokana na uwezo wa safu ya ushambuliaji ya Marumo katika kutengeneza nafasi.

“Marumo Gallants si timu mbaya kwa sababu washambuliaji wake ni wazuri, mechi ya kwanza waliweza kutusumbua, lakini safu yao ya ulinzi inashida, tukiweza kutumia madhaifu yao tutarejea nyumbani tukiwa tunacheza fainali, lakini tusipokuwa makini tutaweza kupoteza hii mechi,” amesema Nabi.

Aidha, kocha huyo amesema kukosekana kwa nyota wake, Bernard Morrison, kwenye mchezo huo hakutaathiri kitu chochote kwa sababu ya kuwa na kikosi kipana hususan mbadala.

Naye Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe, amesema wamefika salama na wachezaji wote wapo salama na tayari kwa mchezo huo. “Tumefika salama, timu imefanya mazoezi katika uwanja uliopo katika hoteli tuliyofika, kazi iliyopo sasa ni wachezaji kufuata yale wanayoelekezwa na kocha ili kuhakikisha tunafanikiwa kucheza fainali ya Afrika,” amesema Kamwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: