Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Phiri namba za kibabe zinambeba Simba

Phiri Robertinho Phiri namba za kibabe zinambeba Simba

Fri, 11 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Presha inaanza kuwa kubwa kwa kocha Roberto Oliveira kabla hata ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu wa 2023/2024 na sababu kubwa ni kutopata nafasi ya kucheza kwa mshambuliaji Mzambia, Moses Phiri na mashabiki wa timu hiyo wanaamini nyota huyo hatendewi haki.

Simba wameanza kumshinikiza Robertinho kumpa nafasi Phiri na kampeni hiyo imeonekana hasa katika mitandao ya kijamii na hata katika vyombo vya habari.

Kuthibitisha hilo hadi wakati Mwanaspoti linakwenda mitamboni, jina la Phiri lilikuwa ni la nne katika orodha ya majina na maneno yaliyotumika kwenye posti za mtandao wa Twitter kwa hapa Tanzania ambapo posti zaidi ya 1,153 zilitaja jina hilo.

Lakini pia katika mtandao wa Instagram, zaidi ya posti 1,000 zimeandika na kutumia jina la Phiri ambapo nyingi zilikuwa ni zile za kushinikiza nyota huyo apewe nafasi ya kucheza.

NAMBA ZINAONGEA

Uwezo wa kufumania nyavu na kupiga pasi za mwisho ambao Phiri alionyesha katika mechi za mwanzoni mwa msimu uliopita ambazo alicheza kabla ya kuumia, ndio unaonekana kuwa chachu ya ushawishi kwa mashabiki wengi wa timu hiyo kulazimisha apewe nafasi ya kucheza.

Katika msimu wa 2022/2023, Phiri alihusika na idadi ya mabao 22 katika mechi 26 za mashindano tofauti alizochezea Simba ambazo ni za Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao hayo 22 ambayo Phiri amehusika nayo, 19 ni yale aliyofunga na matatu yametokana na asisti zake.

Phiri alipachika mabao 10 katika Ligi Kuu, akafunga mabao matano kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na manne katika ASFC.

MSIKIE ROBERTINHO

Kocha Robertinho amezungumza na Mwanaspoti juu ya ishu ya Phiri akisema hana tatizo lolote na mshambuliaji huyo na na anapocheza huwa watu hawaulizi kwanini amecheza.

Robertinho alisema baada ya kutoka kuwa majeruhi anaendelea kumuandaa Phiri taratibu ili aje kuingia katika kikosi cha sasa baada ya kukosa sehemu kubwa ya mwisho wa msimu uliopita.

“Hakuna tatizo kati yangu na Phiri, hakuna kocha ambaye atamkataa mchezaji mzuri kama Phiri, tuko katika hesabu za kutengeneza timu kwasasa, kuna wakati mtamuona huyu na wakati mwingine msimuone mwingine,” alisema Robertinho.

“Kila mchezaji kwenye kikosi chetu kwasasa ni hitaji letu kiufundi, Phiri hakucheza mechi ya Simba Day lakini tukiwa Uturuki tulimpa nafasi kwenye mechi mbili, ni alicheza na watu hawakuhoji kwanini anacheza.

“Tusisahau Phiri alikuwa nje muda mrefu tunatakiwa kuanza taratibu kumrudisha kwenye ubora wake, pia tunatakiwa kutengeneza timu yenye uwiano mzuri uwanjani hatupangi timu kwa kuangalia huyu lazima acheze.

Aidha, Robertinho aliongeza hesabu zake za msimu ujao bado ziko salama na Mzambia huyo ndiye mchezaji anayeweza kuwa mbadala wa Jean Baleke na hata mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’.

“Tumesajili timu kubwa msimu huu, ambayo tunaendelea na kazi ya kuwaunganisha wale tuliobaki nao kutoka msimu uliopita na hawa waliokuja sasa nadhani taratibu tutajenga timu imara.

“Tuna malengo makubwa na Phiri kwa ubora wake wa kufunga tunafikiria awe anashindana na Baleke lakini pia anaweza kutusaidia hata tunapotaka kupata mbadala wa Saido ana ubora wa kucheza maeneo hayo.

“Kitu muhimu tumewaambia wachezaji timu itapangwa kuanzia mazoezini napenda kuona wachezaji wote wakijituma.”

MSIMU WA TAMBWE

Suala la Phiri linaelekea kufanana na lile lililomkuta nyota wa zamani wa timu hiyo Amissi Tambwe katika msimu wa 2014/2015.

Katika msimu huo, aliyekuwa kocha mpya wa Simba, Patrick Phiri alionekana kutompa nafasi ya kutosha ya kucheza Tambwe ambaye msimu mmoja nyuma alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo na Ligi Kuu baada ya kupachika mabao 19 na badala yake akawa anampa nafasi ya mara kwa mara nyota mpya aliyesajiliwa na timu hiyo, Dan Sserunkuma kutoka Uganda.

Kitendo cha kuwekwa benchi kilimchosha Tambwe ambaye katika msimu huohuo aliamua kutimkia Yanga ambako aligeuka kuwa lulu na kutoa mchango mkubwa katika mafanikio ya timu hiyo ikiwamo kuipa ubingwa wa Ligi Kuu.

Katika msimu wa kwanza tu kuichezea Yanga, Tambwe alipachika mabao 13 na msimu uliofuata akaibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu akifumania nyavu mara 21.

WADAU

Nyota wa zamani wa Nazareth ya Njombe, Tigana Lukinja alisema Phiri alishathibitisha uwezo wake nchini na ndio maana mashabiki wamekuwa wakipigania acheze.

Phiri ni mmoja kati ya washambuliaji wazuri wenye ubora wa juu aliokwishauonyesha ndani ya kikosi cha Simba. Mabao 10 chini ya mechi 15 za nusu ya msimu ambazo alicheza kabla ya kuja kwa Robertinho. Pia, hadi mwisho wa msimu amehusika na mabao 22 katika mechi 26 katika mashindano yote, itoshe kusema ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.

“Labda kama kuna sababu nyingine za nje ya uwanja ambazo zinamuweka benchi na hasa ukichukulia ‘performance’ za baadhi ya wachezaji ambao wanaorodheshwa kwenye kikosi.

“Hofu ni kama ataanza kumtumia sasa atatafsirika ni presha ya mashabiki si mahitaji ya kiufundi lakini kwa maoni yangu Phiri ni mchezaji mzuri sana.”

Nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden alisema suala la Phiri liko chin ya Robertinho.

“Kocha ndiye mwenye uamuzi wa mwisho. Simba ina wachezaji wengi wazuri hivyo yeyote anaweza kupangwa na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri.”

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: