Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Onana wa Simba aibuka Dar

Onana Dar Onana wa Simba aibuka Dar

Wed, 5 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mashabiki wa Simba wakisubiri kwa hamu fujo za kutambulishwa kwa mastaa wao wapya Mwanaspoti limemnasa Leandre Willy Onana (23), ambaye amefanya vipimo tayari kwa ajili ya msimu mpya akiwa na timu hiyo.

Onana ambaye anacheza winga wa kulia, kushoto na kiungo mshambuliaji imethibitishwa kuwa amemalizana na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akiwa anatokea Rayon Sports ya Rwanda, amefanya vipimo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili sambamba na mastaa wengine wazawa.

Zoezi la upimaji wa Afya limefanyika juzi huku mastaa wengine waliofanyiwa vipimo ukiachana na Mcameroon huyo ni Shomari Kapombe, Ali Salim, Habibu Kyombo, Ahmed Teru, Mohammed Mussa, Israel Mwenda, Mzamiru Yassin na Nasoro Kapama.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa la kwanza kueleza kuhusu usajili huu jana, liliweka kambi kwenye Hospitali hiyo na kumuona Onana akiwa mmoja kati ya wachezaji waliofanya vipimo hivyo pamoja na kwamba hakuwa kwenye listi iliyokuwa imesambaa mtandaoni na bado hajatambulishwa rasmi. Kwanini vipimo vya afya:

Huu ni utaratibu ambao unafanyika dunia nzima kwa wanasoka kupimwa mwanzoni mwa msimu wa ligi, ambapo kwa wachezaji wapya hutakiwa kufuzu kwanza hapa kabla ya kupewa mkataba rasmi.

Kwa mujibu wa utaratibu wa upimaji afya ambao hapa kwetu umekuja hivi karibuni, kila mchezaji hutakiwa kufanyiwa vipimo kwenye vituo ambavyo vina vifaa vya kisasa na unaweza kuchukua saa 12-24, iwapo taratibu zote zitafuatwa.

Uchunguzi huu wa afya hutakiwa kuangalia hutegemeana na umri, afya kwa jumla, historia ya familia na mienendo na mitindo ya kimaisha ikiwamo kama mwanamichezo anatumia tumbaku au kilevi chochote.

Lakini pia hujikita kwenye matatizo ya mfumo wa moyo na mzunguko wa damu, mfumo wa upumuaji, mfumo wa fahamu, mfumo wa mifupa na misuli na mengineyo.

Vilevile uchunguzi wa kimwili ikiwamo upimaji wa shinikizo la damu, kasi ya upumuaji, joto la mwili, mdundisho wa damu katika mshipa. Vipimo vya uzito, urefu, na upimaji wa ukubwa wa misuli na mwili pia hufanywa kubaini uzito mkubwa au mdogo.

Vipimo vya kisasa huweza kutumika kuweza kubaini matatizo ya kiafya yaliyojikita kwa ndani zaidi ikiwamo vipimo vya picha za CT na MRI. Kwa upande wa uchunguzi wa mwili unaweza ukahusisha maabara na vipimo vya picha.

Vipimo kama vya wingi wa damu na kundi lake, kipimo cha picha nzima ya damu, kiwango cha sukari ya mwili, vipimo vya maambukizi ya magonjwa ya kujamiana na VVU.

Fifa iliweka mwongozo wa uchunguzi wa kiafya wa kina wa moyo hasa baada ya matukio ya wanasoka kufariki viwanjani.

Uchunguzi wa moyo ni muhimu sana, kwani inahofiwa endapo mchezaji atakuwa anashiriki michezo matatizo katika mfumo wa damu na moyo unaweza kumsababishia moyo kusimama na kupata kifo cha ghafla.

Wakati zoezi la vipimo likifanyika kwa mastaa hao mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake litajwe kwenye gazeti alisema wachezaji wa Simba wanatakiwa kwenda Mlonganzila kukamilisha vipimo vyao vya moyo kwa kuwa pale jana kulikuwa na foleni ndefu.

Waliobaki:

Wakati kundi la kwanza wakikamilisha kwa upande wa wazawa ambao hawakupima juzi ni Aishi Manula, Mohammed Hussein 'Tshabalala', John Bocco, Kibu Denis na Jimmyson Mwanuke.

Wakati mastaa wakigeni ambao watapimwa leo ni Clatous Chama, Jean Baleke, Sadio Kanoute, Peter Banda, Saido Ntibazonkiza, Joash Onyango, Moses Phiri, Pape Sakho na Henock Inonga na wachezaji wenguine waliosajiliwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: