Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota hawa watainogesha Simba Day 2023

Jose Luis Miquissone Noma.jpeg Luis Miquissone

Sun, 6 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ile siku ambayo mashabiki wa Simba walikuwa wakiisubiri kwa hamu hatimaye imekaribia kushuhudia nyota wao na benchi la ufundi wakitambulishwa kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano 2023/24 huku wakitesti mitambo kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya mabingwa wa Zambia, Power Dynamos.

Kuonyesha kuwa wenye nchi wameitikia jambo lao, siku tatu kabla ya tukio wekundu hao wa Msimbazi waliweka rekodi ya kuuza tiketi zote za tamasha hivyo, yaani wameujaza Uwanja wa Benjamini Mkapa mapema tu. Hapo kabla haijawahi kutokea.

Tiketi za Platnum ziliisha siku moja baada ya kutangazwa kuuzwa zikifuatiwa na VIP A siku mbili baadaye.

Katika kilele hiki cha Simba Day wapo wachezaji ambao wanatazamiwa kunogesha tamasha hili kutokana na usajili wao kugonga vichwa vya habari na hakika wanasimba wanataka kuwaona wajue yaliyomo yamo kama ambavyo wamekuwa wakipambwa? 

CHE MALONE

Julai 9, uongozi wa Simba ulimtangaza beki wa kati, Che Fondoh Malone (24) raia wa Cameroon kutoka Cotton Sports FC  aliyesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili ili kuziba nafasi ya Mkenya, Joash Onyango aliyetimkia Singida FG.

Che Malone amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Cotton Sports kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Cameroon msimu uliopita akiwa nahodha huku akicheza karibu mechi zote, Wanasimba wana shauku ya kuona ubora wake akiwa na jezi ya chama lao.

Che Malone ambaye anajulikana kwa jina la utani ‘Ukuta wa Yericko’ ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu Cameroon (MVP) msimu wa 2022/23.

Kitasa huyo ni mchezaji mwenye uzoefu wa kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Shirikisho, alikuwa mchezaji wa tatu kutambulishwa wakati wa dirisha hili kubwa la usajili baada ya Willy Essomba Onana na Aubin Kramo Kouame.

LUIS MIQUISSONE

Tangu kuondoka kwake Msimbazi katika awamu yake ya kwanza hakupatikana winga wa aina yake ambaye alikuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango ndio maana mabosi wa timu hiyo wamefanya uamuzi ya kumrejesha nyumbani, Luis Miquissone akitokea Misri ambako alikuwa akiichezea Al Ahly.

Shauku ya mashabiki wa Simba ni kutaka kuona je, huyu ni yule yule ambaye alikuwa akiwafanya mabeki wa timu pinzani kulala na viatu kwa kasi na usumbufu wake akishambulia kutokea pembeni kulia au kushoto?

Simba imepata huduma ya Miquissone baada ya nyota huyo kuvunja mkataba na Al Ahly. Kurejea kwa Miquissone kunatazamwa kama faida kutokana uzoefu mkubwa na soka la Afrika lakini kubwa zaidi analijua vema soka la Tanzania.

FABRICE NGOMA

Huu ni miongoni mwa sajili ambazo zilizungumzwa sana kutokana na nyota huyo wa Kimataifa wa DR Congo kuhusishwa na Yanga, hivyo macho ya mashabiki wa Simba yatakuwa kwake kuona yale ambayo alikuwa akiyafanya na Al Hilal ya Sudan.

Ngoma ni mchezaji mzoefu ambaye anaweza kucheza kama kiungo mkabaji huku akiwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi kwa usahihi kutoka nyuma hadi mbele kwa washambuliaji.

Ngoma ni mchezaji mwenye wasifu mkubwa katika soka la Afrika hivyo anaweza kukonga mioyo ya mashabiki wa Simba msimu ujao wa 2023/24.

Ngoma anakumbukwa kwa kiwango bora alichoonyesha mwaka 2018 akiwa katika kikosi bora cha AS Vita kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Raja Casablanca huku akifunga bao la tatu.

Mbali na Al Hilal na AS Vita, Ngoma ambaye ana urefu wa futi sita pia amewahi kuzitumikia klabu za Raja Casablanca (Morocco), Al Fahaheel FC (Kuwait) na Ifeanyi Ubah FC (Nigeria).

WILLY ONANA

Hiki ni chuma kingine ambacho kinaweza kunogesha Simba Day, kwanza ni chaguo la kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Essomba Onana (23) raia wa Cameroon alitua Simba kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

Onana amesajiliwa kutoka Rayon Sports ya Rwanda ambapo msimu uliopita ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini humo (MVP).

Onana ni mchezaji mwenye kipaji na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi za mbalimbali uwanjani wingi zote mbili pia anaweza kumudu nyuma ya mshambuliaji (namba 10) pia mshambuliaji kivuli (false number nine).

Msimu uliopita Onana aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu nchini Rwanda baada ya kufunga mabao 16 na kusaidia kupatikana kwa mengine matano (asisti).

AUBIN KRAMO 

Kramo mwenye umri wa miaka 27 ametua Simba baada ya Kusaini mkataba wa miaka miwili. Mwamba huyo wa zamani wa miamba ya Ivory Coast, ASEC Mimosas anaweza kunogesha Simba Day kutokana na uzoefu wake.

Kutua kwa Aubin Kramo Kouame kunaifanya Simba kwenye eneo la ushambuliaji kuwe na Wachezaji wengine hatari ambao ni Onana, Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama, Jean Baleke, Moses Phiri na yeye mwenyewe Aubin.

Aubin alikuwa mchezaji wa pili mpya wa Simba baada ya mshambuliaji Onana kutambulishwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: