Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ntibazonkiza kuanzia benchi msmu ujao

SAIDOOO Kiungo wa Simba SC, Saido Ntibazonkiza

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kushinda tuzo nne za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) msimu uliopita, bila shaka yoyote Mshambuliaji Saido Ntibazonkiza ndiye mchezaji Bora wa Simba kwa 2022/2023. Ntibazonkiza ndiye mchezaji mwenye wasifu wa juu zaidi kwenye ligi yetu.

Tumempata nchini ni kwa sababu tu umri unamtupa mkono. Ni kwa sababu tu anamalizia soka lake, akiwa wa moto, hakuna timu Tanzania ingeweza kumsajili. Hakuna hata moja. Kila nikitazama aina ya wachezaji wanaotangazwa kusajiliwa na Simba kuelekea msimu ujao, napata maswali mengi sana.

Nimeona Simba wamemtambulisha Aubin Kramo. Fundi kweli kweli kutoka Asec Memosas, ni mtu na nusu kwenye kushambulia. Kwa ubora wake na namba ambazo amekuja nazo kikosini, namuona moja kwa moja akiingia kwenye kikosi cha kwanza.

Nimeona pia jina la Essambo Onana, fundi mwingine kutoka Cameroon alikuwa na msimu bora sana pale kwenye ligi ya Rwanda. Hakuwa mfungaji Bora kwa bahati mbaya. Hakuwa mchezaji bora wa ligi ya Rwanda kwa bahati mbaya. Ni mtu na nusu mwingine ambaye amejiunga na wababe hao wa Msimbazi.

Hawa wachezaji wote wawili, ni wazi kuwa wanaingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.

Idara ya Ushambuliaji ya Simba inakwenda kuwa na ushindani mkubwa sana. Unaiona nafasi ya Ntibazonkiza? Naomba maoni yako kwa njia ya Ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Ntibazonkiza bado ni mchezaji mzuri sana. Tuzo nne alizoshinda msimu uliopita, hazikuja kwa bahati mbaya. Simba haikuwa na shida kwenye eneo la ushambuliaji, ndiyo maana wao ndiyo timu iliyofunga mabao mengi sana msimu uliopita kwenye ligi kuliko timu nyingine yoyote Tanzania (75).

Kumleta Kramo na Onana ni kuongeza wanaume wa shoka kundini. Simuoni Clatous Chota Chama akienda Benchi. Simuoni Jean Baleke akianzia benchi. Kocha Robertinho atakuwa na kazi kubwa sana. Robertinho atakuwa na presha kubwa sana. Kila sare kwake, zitakuja habari za kutaka atimuliwe. Kila kichapo kwake, kitamnyima usingizi.

Namuangalia Kibu Dennis na ubora wake, nawaangalia Onana na Kramo, kisha pasi namuachia Robertinho. Hii ya Msimu ujao itakuwa na presha kubwa sana kwa Kocha. Ukiiangalia kwenye makaratasi, unaona kama Simba wamekamilika. Lakini unajua kitakachotoa Uwanjani? Wote hatuna uhakika.

Nadhani hata Robertinho naye hana uhakika, uzuri ligi muda mchache ujao itakuwa inaanza, tutajua tu mbivu na mbichi. Namtazama Onana. Namtazama Kramo. Ntibazonkiza kuanzia benchi? Bado majibu.

Moja kati ya jambo ambalo Simba walizidiwa sana na Yanga msimu uliopita, ni upana wa kikosi. Yanga walikuwa na wachezaji wengi wazuri kwenye benchi lao. Simba walikuwa na wachezaji wazuri sana 11 wa kikosi cha kwanza tu. Benchi la Simba lilikuwa limekondeana. Halikuwa na watu wengi wa kazi.

Plani A ikishindikana, Simba walikuwa wanapata shida. Kwa usajili wa msimu huu, naona Simba wakiwa na Benchi lililojaa wanaume wa kweli. Kama kuna mahali ambapo bado Simba hawajakaa sawa, ni eneo alilokuwa anacheza Jonas Mkude.

Wamekuja wachezaji wengi pale lakini tangu Mkude aanze kwenda benchi, Simba haijawahi kuwa sawa. Ni muhimu sana kumleta Mkata Umeme. Mimi sio shabiki wa Sadio Kanoute hata kidogo. Rafu nyingi, maarifa kidogo. Simba wanahitaji kuleta kiungo wa kucheza na Mzamiru Yassini.

Naona wamejaza wachezaji wengi kwenye idara ya ushambuliaji lakini huku nyuma, bado hawako sawa. Ni muda sasa wa kupata pia mabeki wa kulia na kushoto wenye uwezo mkubwa. Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ni binadamu. Kuna muda na wao watachoka. Unahitaji kuanza kuandaa mbadala kwenye eneo hilo pia.

Kusajili wachezaji wazuri ni jambo moja, kupata timu ye ushindani ni jambo lingine. Hili la pili ndiyo gumu zaidi. Kuna kelele nyingi sana kwenye usajili kuliko uwezo wa wachezaji uwanjani. Sehemu kubwa ya wachezaji wa kigeni waliondoka msimu huu, walisajiliwa pia msimu uliopita.

Sitarajii kuona hilo likitokea msimu huu, kocha ana kazi kubwa sana kuliko viongozi. Uongozi kazi yao kubwa ni kutoa pesa za kusajili wachezaji. Hakuna kingine. Kocha ana kazi ya kutengeneza timu. Kocha ana kazi ya kuwapa raha wana Simba. Misimu miwili wakitoka patupu, wana Simba hawana raha.

Robertinho ndiyo amebeba furaha ya wana Simba. Nikitazama kelele za ujio Onana na Kramo, najiuliza Mchezaji Bora wa Simba msimu ujao ataanza kweli kwenye kikosi cha kwanza? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: