Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Noma sana! Wana fedha halafu wanachizika na soka

GSM X MO Wawekezaji katika vilabu vya Simba na Yanga, Mo Dewji na GSM

Wed, 2 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uhondo unaerudi upya, wakati msimu wa mashindano ukitarajiwa kuanza tena mwezi ujao. Tutaanza na mechi za Ngao ya Jamii kwa kuzikutanisha timu nne zitakazoiwakilisha nchi kimataifa.

Ndio, Simba, Yanga, Azam Fc na Singida Fountain Gate zitakuwa jijini Tanga kuanzia Agosti 9 hadi 13 kwa ajili ya mechi za michuano hiyo inayozindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara itakayoanza siku mbili baadae mara itakapopigwa fainali ya Ngao kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Hiyo ni kwa upande wa soka la ndani, lakini kwenye anga la kimataifa nako kuna uhondo wake, wakati Ligi Kuu ya England itaanza rasmi Agosti 11, kisha kipute cha Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, itaanza kwa mechi za raundi ya awali zitakazopigwa kuanzia Agosti 18-20.

Lakini kama kawaida kwenye soka, mashabiki walio wengi sio watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na badala yake wanaburudika kupitia wenye fedha zao walioamua kuwekeza kwenye mchezo huo.

Utabisha nini? Hakuna ubishi kwamba mashabiki wengi wa soka nchini hawana uwezo mkubwa kifedha, lakini wale wenye fedha zao huwa sio wanazi wakubwa wa timu za Ligi Kuu Bara ama zile za visiwani Zanzibar. Wengi wanapenda michezo mingine kama tenisi, gofu ama kikapu.

Hiyo inatajwa kuwa ni michezo ya kishefa, hata hivyo bado kuna matajiri ambao huwezi kuwaambia kitu kuhusu soka.

Kuna baadhi ya matajiri wakiamka tu, asubuhi wao ni soka, lakini kuna wengine hawafahamu soka vizuri lakini wanazipenda timu za soka na kumwaga fedha zao kishefa zaidi.

Sio ajabu kumkuta tajiri amekosa furaha kutokana tu na timu anayoizimia na anayoimwagia fedha za kumwaga ikishindwa kufanya vizuri.

Ebu fikiria tu, tajiri ana fedha, magari na majumba ya kutosha lakini anahuzunika na kukosa amani pale timu anayoipenda inapofungwa.

Hapo chini ni baadhi ya matajiri wenye fedha zao ambao wamekuwa wapo mstari wa mbele katika soka kwa Bara na Visiwani Zanzibar kwa kuweka fedha zao kuonyesha mapenzi makubwa kwa mchezo huo na kuchangia kwa kiasi kikubwa cha furaha ya mashabiki wa nawadu wa klabu hizo.

GHALIB SAID MOHAMED (GSM)

Huyu ndiye bilionea anayewapa raha mashabiki wa Yanga. Miaka michache iliyopita, Yanga ilikuwa hoi kiuchumi na hata uwanjani, kiasi iligeuzwa wanyonge na watani wao, Simba iliyobeba mataji karibu yote kwa misimu minne mfululizo.

Simba ilikuwa ikifanya inavyotaka kwenye soka la Tanzania na anga la kimataifa. Ilibeba mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii na bado ikatetemesha hadi michuano ya CAF, wakati Yanga ikijitafuta kinyonge ikitegemea bakuli lililopewa jina la Kubwa Kuliko.

Bakuli lilikuja baada ya Yusuf Manji kujiengua wakati Yanga ikiwa kwenye kilele cha neema na mafanikio makubwa kwa misimu mitatu mfululizo, hata hivyo ujio wa GSM ukamaliza utata.

Bilionea huyo ameifanya Yanga iwe moja ya klabu inayokimbiliwa na mastaa mbalimbali kutoka nje ya nchi kutokana na namna inavyokimbiza na kuwa na uhakika wa kulipwa kiwango chochote cha fedha na matokeo uwanjani yanayonekana kwa Yanga kuandika rekodi ya kufika fainali ya CAF.

Yanga iliyoonekana ombaomba leo imekuwa timu ya kitajiri kutokana na fedha za GSM, aliyediriki kuiweka timu hiyo kambi ya 'milele' katika Kijiji cha Avic, Kigamboni na kufanya mastaa kutojisikia vibaya timu kutokwenda nje ya nchi kama ilivyozoeleka kwa namna kambi ilivyo ya kishua.

Na kama unataka kuwakera wanayanga, jaribu kumsema vibaya bilionea huyo aliyewapa faraja kwa kuwa na timu yenye uwezo wa kuwapiga nje ndani timu za Kiarabu ambazo kwa miaka mingi zilikuwa zikiwageuza vibonde wao na kama sio sheria ya bao la ugenini, huenda Yanga leo ingekuwa inatambia taji la kwanza la Afrika la Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kulikosa kiduchu mbele ya USM Alger ya Algeria, na jeuri yote ikiwa ni fedha za GSM akishirikiana na wadhamini wa klabu.

SAID SALIM BAKHRESA

Huyu ndiye tajiri mwenye mapenzi makubwa zaidi na soka nchini. Bakhresa anapenda soka usiambiwe na mtu, kwani tangu alipoanza kuchipukia kwenye utajiri soka imekuwa kama chakula chake.

Alianza kuibeba Simba, klabu anayoipenda moyoni mwake akiwa kama kiongozi na baadae mfadhili wa kimyakimya ndipo akaamua kuanzisha klabu yake binafsi ya Azam FC.

Bakhresa ni miongoni mwa matajiri wakubwa nchini akimiliki viwanda vya Unga, Juisi, Lambalamba na Maziwa. Anamiliki magari ya kutosha, boti zinazosafirisha abiria kutoka Bara kwenda Zanzibar na makorokoro mengine kibao. ikiwamo kumiliki Azam TV iliyoleta mabadiliko makubwa kwenye soka la Tanzania kutokana na udhamini aliouweka.Kwa kifupi ni kamba Bakhresa ni tajiri mkubwa.

Hata hivyo pamoja na yote huwezi kumwambia kitu kuhusu soka. Bakhresa amekuwa si mtu wa kuhudhuria sana viwanjani, lakini amekuwa hakosi kutazama mechi za Azam kupitia runinga yake ya Azam TV. Watoto wake pia wamerithi mapenzi yake ya soka na wamekuwa wakisafiri hadi nje ya nchi kwenda kutazama mechi kubwa za soka, huku wakisajili wachezaji wenye majina na ubora wa kiwango cha pro max kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wa kandanda nchini.

MOHAMMED 'MO' DEWJI

Ukisikia mtu na pesa zake, basi huwezi kumuacha Mohammed 'MO' Dewji. Ukimkuta kwenye soka ni kama vile sio yeye. MO ni mwanachama kindakindaki wa Simba akiwa kwa sasa ana cheo cha Rais wa Heshima. Amekuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za timu hiyo. Kwa sasa anataka kuinunua kabisa timu hiyo ili aiwezeshe kufanya vizuri zaidi.

Kama ulikuwa hufahamu ni kwamba MO ni tajiri, tena si Tanzania tu, Afrika kwa jumla. Familia ya MO inamiliki viwanda zaidi ya 40 Afrika na wamekuwa wakijihusisha na biashara nyingi ikiwemo za vyakula kama tambi na biskuti. Amekuwa akitengeneza Juisi, Soda na Sabuni mbalimbali. Kwa kifupi ni kwamba MO ni mfanyabiashara mkubwa.

Hata hivyo katika soka MO amekuwa chizi. Anaweza kutokea uwanjani akiwa amevalia pensi na jezi yake ya Simba na wala hajali. Mapenzi yake na soka yalimwezesha kununua Mto Singida, kishaa African Lyon lakini kwa bahati mbaya mipango yake ilivurugika na kuamua kuachana nayo.

Amekuwa akimwaga fedha hata kabla ya mchakato wa klabu kuendeshwa kwa hisa haujakamilika akifadhili kwa kila kitu usajili na gharama za timu na amekuwa akionyesha hisia za uchungu pale, Simba inapopata matokeo mabaya kiasi cha kutishia mara kadhaa kujitoa.

Hata hivyo mapenzi yake kwa Simba, yamemfanya iwe ngumu kwake kwa vile soka lipo kwenye damu yake hata kama anacheza pia mchezo wa Gofu, kiasi amekuwa akiwekeza fedha nyingi kuifanya Simba iwe ilipo.

FAHAD PIRMOHAMMED

Huyu ndiye mmiliki wa Ihefu FC, timu iliyoweka rekodi msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara kwa kuitibulia Yanga kucheza mfululizo wa mechi nyingi za Ligi Kuu bila kupoteza.

Yanga ikiwa imecheza mechi 49 bila kufungwa na kwenda kukutana na Ihefu ikiburuza mkia kwenye Uwanja wa Highland Estate unaomiliki klabu hiyo na kufumuliwa mabao 2-1 na rekodi kuishia hapo.

Bilionea huyu hana makeke na wala hajitokezi sana kama ilivyo kwa Mo Dewji na Simba yake au GSM na Yanga yake, lakini jamaa anatajwa kuwa kichaa wa soka na ndio maana amwekeza fedha nyingine kwa ajili ya timu hiyo inayomiliki uwanjani wake mwenyewe kule Mbarali.

Ihefu inatajwa moja ya klabu zilizo na uwezekaji mkubwa na inayowapa maisha wachezaji kiasi cha kuona fahari kuitumikia, licha ya kwamba haiimbwi sana kama klabu nyingine na kazi yote hiyo inatokana na fedha zinazomwaga na Fahad kuhakikisha wanawapa raha mashabiki wa soka wa Mbarali ilipo maskani ya timu hiyo iliyoapnda Ligi Kuu msimu wa kwanza wa 2020-2021 kabla ya kurejea tena msimu uliopita na kufanya kweli kwa kumaliza nafasi ya sita.

WENGINE

Sio mabilionea hao tu, lakini kuna watu wenye fedha na nafasi zao wanaojitoa kwenye soka hata kama hawatajwi moja kwa moja.

Utasema nini juu ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kocha wa zamani wa soka ambaye ameirudisha Lindi kwenye soka baada ya Kariakoo Lindi kushuka daraja kwa kuiibua Namungo iliyoweka rekodi ya kupanda Ligi Kuu na kukata tiketi ya kimataifa na kufika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2021 hata kama ilishindwa kupata ushindi au kufunga bao kwenye mechi ya kundi ililokuwepo.

Majaliwa, ni Simba lialia, lakini humwambii kitu kwa Namungo inayomiliki uwanja wa kisasa wa Kassim Majaliwa, uliopo Ruangwa mjini Lindi.

Pia kuna Mwigulu Nchemba, Yanga lialia, ambaye amekuwa wakijitolea na kuchangia mno fedha kwenye soka kuanzia klabu anayoipenda moyoni ya Yanga, hadi zile ambazo amekuwa akihusishwa nazo kama Singida United iliyotamba Ligi Kuu na kushuka daraja, DTB iliyopanda daraja na kuitwa Singida Big Stars kabla ya sasa kufahamika Singida Fountain Gate.

Idd Azan, naye ni mmoja ya watu wenye fedha zao, lakini anachizika sana na soka kiasi cha kufikia kuanzisha klabu iliyowahi kutamba kwenye Ligi Kuu, Twiga Sports kabla ya kuiuza kwa klabu ya Pan Africans kisha kupotea jumla.

Kuna mwanasiasa, Alexander Mnyeti aliyeimiliki Gwambina FC iliyowahi kutamba Ligi Kuu Bara kabla ya kushuka na kisha kuchukizwa na figisufigisu za soka la Bongo na kuifutilia mbali, ikiwa Championship.

Mnyeti ni mtu mwenye fedha zake na alidiriki kuweka hadi uwanja wa kisasa uliofahamika kama Gwambina Complex, kabla ya kuzinguliwa na wenye mamlaka ya soka la kuingiwa ubaridi.

Orodha ni ndefu, lakini ukweli ni kwamba wadau hao na wengine wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwapa raha mashabiki na wapenzi wa soka kwa kuwekeza na kutoa fedha zao, bila kujali kama wakati mwingine zinawapa karaha kwa matokeo mabaya uwanjani au figisufigisu zinazowapa stresi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: