Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Simba, Yanga na Singida tu sasa

Simba Players Chama Ni Simba, Yanga na Singida tu sasa

Thu, 31 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sasa ni rasmi timu tatu tu za Tanzania ndizo zilizosalia kwenye michuano ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya Azam, JKU na KMKM kuchemsha kwenye hatua ya awali.

Vigogo vya soka Yanga na Simba vimebeba dhamana ya kupeperusha bendera ya taifa katika Ligi ya Mabingwa, wakati Singida Fountain Gate ikikomaa michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya Azam na JKU kuchemsha kama ilivyo kwa KMKM iliyokuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa.

Simba ilipata ofa ya kuanzia raundi ya kwanza baada ya msimu uliopita kuishia hatua ya robo fainali na mechi zao za raundi hiyo sasa itacheza na Power Dynamos ya Zambia iliyoitoa African Stars ya Namibia, huku Yanga ikikutana na El Merrikh ya Sudan iliyotoa Otoho d’Oyo ya Jamhuri ya Congo. Kwa upande wa Singida inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza iliyoitoa JKU ya Zanzibar itakutana na Future ya Misri ambayo inaanzia raundi ya kwanza kama ilivyo kwa Simba.

Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa kina juu ya timu hizo pindi zitakapokutana kuanzia Septemba, mwaka huu.

EL MERRIKH v YANGA

Yanga itakutana na El Merreikh ya Sudan katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa jumla wa mabao 7-1 dhidi ya Asas FC ya Djibouti - michezo yote ikipigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Miguel Gamondi kilikata tiketi hiyo baada ya mchezo wa kwanza kushinda mabao 2-0 huku marudiano kikishinda 5-1, michezo yote ikichezwa Azam Complex.

El Merrikh inakutana na Yanga baada ya kuitoa AS Otoho d’oyo ya Congo Brazzaville kwa faida ya bao la ugenini baada ya kufungana 1-1 katika mchezo wa kwanza kisha marudiano kutoka suluhu.

Yanga itaanzia ugenini Morocco badala ya Rwanda baada ya El Merrikh kuachana na Uwanja wa Huye na kuamuamechi za nyumbani dhidi ya vijana wa Miguel Gamondi ipigwe Morocco kwa vile nchi ya Sudan inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mechi ya mkondo wa kwanza itachezwa kati ya Septemba 15-17, huku ile ya marudiano ikichezwa kati ya Septemba 29 hadi Oktoba Mosi na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi itakayoanza kati ya Novemba 24-26.

Yanga imekuwa tishio kwenye eneo la ushambuliaji na uzuiaji kwa sababu katika michezo mitatu iliyopita ya mashindano yote imefunga jumla ya mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa moja.

Kwa upande wa El Merrikh sio timu ya kutisha sana kutokana na kiwango chake cha hivi karibuni, kwani katika michezo mitatu ya mashindano yote imefunga bao moja na kuruhusu mabao mawili.

El Merrikh imetwaa mataji 19 ya Ligi Kuu Sudan kuanzia mwaka 1970, 1972, 1974, 1978, 1982, 1985, 1990, 1993, 1997, 2000, 2001, 2002, 2008, 2011, 2013, 2015, 2018, 2018–2019 na 2019–2020.

El Merrikh ina rekodi ya kipekee kwani imewahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Washindi mwaka Afrika 1989 baada ya kunyakua taji hilo kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 dhidi ya Bendel United ya Nigeria.

Mwaka 2017 El Merrikh ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ingawa haikuweza kufua dafu mbele ya CS Sfaxien ya Tunisia iliyotwaa ubingwa huo kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2.

Licha ya rekodi hizo ila Yanga inapaswa kuongeza umakini zaidi ili kutimiza ndoto ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani imetimia miaka 25 tangu ilipofanya hivyo - mwaka 1998.

POWER DYNAMOS v SIMBA

Kikosi cha Simba chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kitakutana na Power Dynamos ya Zambia katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupigania nafasi ya kutinga makundi.

Simba ambayo imeanzia hatua ya pili inakutana na Dynamos iliyoitoa African Stars ya Namibia kwa ushindi wa bao 1-0, ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndoladhidi, Zambia. Dynamos imebebwa na faida ya bao la ugenini ililolipata Namibia katika mchezo wa kwanza ilipochapwa 2-1 hivyo kuifanya Simba kuanzia mechi ya mkondo wa kwanza Zambia kati ya Septemba 15-17.

Simba inafukuzia kuendeleza rekodi yake nzuri ya kutinga kwa mara nyingine hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyofanya kuanzia mwaka 2003, 2018/2019, 2020/2021 na 2022/2023.

Ikumbukwe Simba iliifunga mabingwa hao wa Zambia kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki wiki chache zilizopita kwa mabao 2-0, katika Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Mkapa. Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Willy Onana na Fabrice Ngoma na kufuta uteja kwao wa kushindwa kushinda wakati kikosi hicho kikicheza na kuhudhuriwa na marais wa nchi uwanjani.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Dynamos imeshiriki mara tatu tu mwaka 1998 na 2012 ilipoishia hatua ya pili huku 2001 ikishindwa kufanya vizuri zaidi baada ya kutolewa hatua ya kwanza. Kombe la Washindi Afrika kabla ya kuunganishwa na kuitwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004, iliishia hatua ya pili mwaka 1985 na iliposhiriki tena mwaka 1995 ilitolewa raundi ya kwanza.

Rekodi zinawabeba zaidi katika michuano ya Kombe la Washindi kwani ilifika robo fainali mara nne kuanzia mwaka 1981, 1986, 1999 na 2003 huku ikitolewa hatua ya pili mara tatu ikianza 1988, 1989 na 1992.

Mwaka 1991 ilitwaa taji la michuano hiyo kwa kuifunga BCC Lions ya Nigeria kwa jumla ya mabao 5-4.

SINGIDA v FUTURE FC

Singida itakutana na Future ya Misri katika hatua inayofuata baada ya kuwaondosha wawakilishi wenzake wa Tanzania, JKU ya visiwani Zanzibar kwa jumla ya mabao 4-3, hivyo kubakia wenyewe kwenye Kombe la Shirikisho.

Hii ni mara ya kwanza kwa Singida kushiriki michuano mikubwa Afrika ingawa licha ya ugeni na ukosefu wa uzoefu kwao ila ina kikosi kizuri kinachoweza kushindana na timu yoyote.

Wapinzania hao wa Singida walianzishwa mwaka 2011 wakifahamika kama Coca Cola ingawa Septemba 2, 2021 walibadilishwa na kuitwa Future huku ikitumia Uwanja wa Al Salam wenye kubeba mashabiki 30, 000.

Msimu uliopita Future ilishinda Kombe la Ligi baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Ghazl El Mahalla kwenye fainali na kumaliza nafasi ya nne na kufuzu Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili mfululizo.

MSIKIE PAWASA

Nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema katika hatua inayofuata jambo kubwa kwa timu za Tanzania ni kucheza kwa malengo zaidi kwani kadri zinavyosogea mbele ndipo ugumu huongezeka.

“Unaweza ukajisifu kwa rekodi nzuri, lakini ukashangaa hatua ya mapema tu unatolewa, timu zetu zimeonyesha zina wachezaji wanaoweza kutupigania na binafsi naziona zikifika mbali,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: