Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngoma, Fadlu kumekucha

Fabrice Ngoma Mapinduzi.jpeg Ngoma, Fadlu kumekucha

Wed, 11 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maisha ndani ya Simba yanakwenda kasi na siku zinasonga, kwani misimu minne iliyopita walikuwa wakitamba nchini wakiwa ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (FA) na pia Ngao ya Jamii, na mambo Msimbazi yalikuwa byee!

Lakini, baada ya watani zao, Yanga kujipanga na kuja na mziki mpya mambo yalianza kubadilika Msimbazi, ambapo kwa misimu mitatu sasa timu hiyo inakimbizwa na watani zao ambao wamebeba makombe hayo yote.

Katika kujitafuta timu Simba ilianza kusuka upya kikosi na kwa msimu uliopita ukiona Simba inacheza, basi kikosini ni nadra sana kulikosa jina la kiungo mkabaji, Fabrice Ngoma.

Msimu huu chini ya kocha Davids Fadlu mambo yamegeuka kwa haraka kwa kiungo huyo Mkongomani na ameanza kuhesabiwa siku ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Ngoma ambaye alijiunga na Simba Julai 2023 akitokea Al Hilal ya Sudan, alikuwa tegemeo katika eneo la kiungo mkabaji kikosini hapo akicheza sambamba na Sadio Kanoute wakati mwingine Mzamiru Yassin au Babakar Saar aliyeingia dirisha dogo na kutoka mwisho wa msimu uliopita.

FALSAFA ZA FADLU

Mchawi wa kwanza kwa Ngoma ndani ya Simba ni ujio wa Fadlu ambaye alishuka na falsafa zake mpya akitaka kiungo mkabaji anayeweza kusogeza mashambulizi na kukaba kwa nguvu, Mkongomani huyu anakosa mambo haya makubwa mawili kwa eneo ana-locheza.

Ngoma yuko taratibu akiwa na mpira kama hatotoa pasi basi ni rahisi kumkuta hatua ambayo imekuwa ikienda kinyume na falsafa za Fadlu ambaye anataka kiungo anayesogea juu kwa haraka kupandisha mashambulizi lakini pia awe na nguvu ya kukaba wakati timu hiyo inautafuta mpira.

USAJILI MPYA

Unamuona Debora Fernandes Mavambo? Yule ndio mchawi wa pili wa Ngoma, jamaa anajua kukaba na kushambulia na utamu zaidi anapiga mashuti ya maana kama hujajipanga sawasawa utadhalilika.

Mavambo ameifanya nafasi ya Ngoma kuwa ngumu, anachofanya Fadlu sasa ni kuiunda Simba au safu ya kiungo kumzunguka Muangola huyo mwenye asili ya Kikongomani.

Fadlu kazi yake ni moja tu sasa kutafuta ni kiungo gani atacheza sambamba na Mavambo ili kukifanya kiungo cha Simba pale chini kuwa imara, hapa ndio kunamfanya Ngoma sasa kujikuta anakuwa chaguo la tatu ndani ya timu hiyo.

HAJAANZA MSIMU HUU

Tangu Fadlu arudi na Simba yake hapa nchini Ngoma hata mechi ya kirafiki hajafanikiwa kuanza, amekuwa anatokea sana benchi akipewa muda mfupi wa kucheza akishuhudia maingizo mapya yakichukua nafasi.

HATAKI KUTOKEA BENCHI

Hatua ya Ngoma kuanzia benchi inaelezwa kwamba haifurahii akitaka kuwa mchezaji anayeanza muda wote lakini tayari makocha wake wana akili tofauti ya nani na nani waaanze kwenye kikosi hicho.

Mchezo dhidi ya Coastal Union katika kusaka nafasi ya tatu kwenye Ngao ya Jamii, Ngoma alijikuta anaingia uwanjani kwa hasira kisha kwenda kupewa kadi mbili za njano ambazo baadaye zikazaa nyekundu akionekana kuwa ni kama mtu aliyekumbana na msongo wa mawazo.

HAYUPO KWENYE HESABU ZA FADLU Hesabu za maboresho ya kikosi chochote yanaanzia pale timu inapomaliza usajili na kuingia kwenye mashindano, Simba imeanzia sasa inataka kuingiza watu wapya lakini ndani ya hesabu za Fadlu, Ngoma hayuko salama.

Ikitokea Simba inataka kuingiza mtu mpya kisha kutakiwa kuamua itamuacha nani, Ngoma huenda akawa ndani ya majina mawili ya haraka katika wale watakaoachwa ndani ya wekundu hao.

SAFARI YA LIBYA Leo alfajiri kikosi cha Simba kimeelekea Libya na katika nyota 22 waliojumuishwa katika safari hiyo jina la Ngoma lipo.

Licha ya kwamba naye yupo katika msafara huo, lakini taarifa zinabainisha kwamba hayupo kwenye mipango ya kocha kuelekea mchezo huo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Hilal Tripol utakaochezwa Septemba 15 nchini humo.

Simba inajiandaa na maisha bila kiungo huyo wa zamani wa Raja Athletic ya Morocco ambapo anaweza kuachwa dirisha dogo la usajili msimu huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: