Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nani kurithi Ufalme wa Mayele Yanga?

MAYELE TRE.jpeg Fiston Mayele

Thu, 20 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ufalme wa straika Fiston Mayele ndani ya kikosi cha Yanga ulitokana na kucheza kwa kiwango cha juu katika misimu miwili akifunga mabao 33 kwenye Ligi Kuu, nje na michuano mingine kama ile ya CAF na aliibuka mfungaji bora akiwa na mabao saba.

Ubora aliouonyesha Mayele Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), ulizivuta timu nyingi kutamani huduma yake na msimu ujao hatakuwa sehemu ya wana Jangwani akitajwa atajiunga na Pyramids ya Misri.

Ndani ya msimu mmoja uliopita Mayele amebeba tuzo tano - nne kwenye Ligi Kuu ambazo ni Mfungaji Bora (17), Bao Bora la msimu, Mchezaji Bora wa msimu na akiwa kwenye kikosi bora cha msimu na Mfungaji Bora wa CAF katika michuano ya Kombe la Shirikisho (saba).

Swali ni je kijiti chake cha ufalme kitamwangukia staa gani ndani ya kikosi hicho, kama ilivyokuwa kwa Mkongomani huyo (Mayele), ambaye licha ya uwezo wake uwanjani, staili yake ya ushangiliaji ya kutetema ilitikisa ndani na nje hadi kugonga hodi kanisani.

Mwanaspoti linakuletea mastaa watano Yanga kulingana na wasifu wao ambao huenda nyota zao zikang'ara baada ya kuondoka kwa Mayele na kikubwa kikiwa ni aina ya ubora wa kazi watakazoanya chini ya kocha mpya, Miguel Gamondi.

Kennedy Musonda

Wakati Yanga inamsajili dirisha dogo straika Kennedy Musonda kutoka Power Dynamos ya Zambia alikuwa kinara wa mabao 11 katika Ligi Kuu ya nchi hiyo, hivyo CV yake hiyo ilitarajiwa kumwongezea nguvu Mayele ambaye alikuwa kwenye kiwango kikubwa.

Ubora wa Mayele ulimpa kibarua kigumu sana Musonda kupata ufalme Yanga na msimu ulioisha kwenye Ligi Kuu alimaliza na mabao mawili aliyofunga dhidi Geita Gold na Dodoma Jiji.

Itategemea na jinsi atakavyomshawishi kocha Gamondi kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza na kiwango kikiwa bora cha kuibeba Yanga kwenye mazingira magumu na mepesi anaweza akawa mbadala wa ufalme wa Mayele.

Aziz Ki

Alipokewa kwa shangwe na Wanajangwani. Winga Stephane Aziz Ki ametokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast na kutokana na uwezo aliouonyesha kwenye Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) ni wazi ni mmoja wa watakaokuwa na ufalme Yanga.

Utambulisho wake uliwalaza macho mashabiki wa soka nchini, uongozi wa Yanga ulianza kuweka kufuli na kwa kuwa Simba ilihitaji huduma yake ikamkosa, basi wengi walisubiri hadi usiku wa manane walipoliachia jina lake.

Msimu ulioisha Ki kuna muda kiwango chake kilikuwa juu, wakati mwingine kushuka alimaliza na mabao tisa, akiifunga Mtibwa nyumbani na ugenini, hat trick dhidi ya Kagera Sugar, Simba, Azam FC, Namungo na Singida Big Stars (Singida Fountain Gate).

Kitakachomfanya aweze kuchukua mikoba ya ufalme wa Mayele ni kiwango atakachokionyesha kuendana na ukubwa wa jina lake lilivyokuwa kabla ya kazi.

Jonas Mkude

Yanga imemsajili Jonas Mkude baada ya kuachwa Simba aliyoitumikia miaka 13, tangu alipokuwa akikichezea kikosi 'B' mwaka 2010, siyo mchezaji mbaya ilikuwa inatajwa nidhamu ni kati ya vitu vilivyofanya wasiendelee naye, lakini mchezaji huyo akiamua kutulia na akajituma kwa bidii anaweza akawa miongoni mwa wanaoweza wakapokea kijiti cha ufalme.

Yannick Bangala

Yanick Bangala raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni kiungo fundi na msimu wa 2021/22 ndiye alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ingawa uliopita hakuambulia tuzo yoyote, akijituma na akacheza kwa kiwango kikubwa anaweza akawa miongoni mwa wanaoweza wakabadili baada ya ufalme wa Mayele licha ya kuibuka taarifa huenda akaachana na kikosi hicho.

Khalid Aucho

Akiwa chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi alitumika kucheza nafasi nyingi hadi walimpa jina la 'Dokta Aucho' kwa maana ya kuleta majibu sehemu ngumu, msimu ujao akicheza kwa kiwango ana nafasi ya kuchukua kijiti cha ufalme.

Iliwahi kutokea Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda ndiye alikuwa nyota aliyependwa kwa muda mrefu ndani ya kikosi hicho, licha ya kutoka na kurejea tena, ujio wa Meddie Kagere 2018-2022 ulifuta ufalme wake.

Simba ilimsajili Kagere kutoka Gor Mahia ya Kenya na ndani ya misimu miwili mfululizo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kuanzia (2018/19 mabao 23) na (2019/20, mabao 22) uliofuatia akawa na mabao 14 na wakati anaondoka msimu wa mwisho alikuwa na mabao saba.

Ukiachana na hilo kwa Yanga, Mayele alifuta ufalme wa Heritier Makambo aliyefunga mabao 17 msimu wa 2018/19 wakati anaondoka Jangwani na kwenda kujiunga na Horoya ya Guinea ambako alishindwa kuonyesha kiwango kikubwa, pamoja na hilo wakati anarejea mashabiki walitarajia kuona kiwango chake kikubwa, lakini haikuwa hivyo hadi akaondoka tena.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: