Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi na Yanga, ndoa iliyoisha kwa amani na miguno

Nabi Na Rais Hersi Said Nabi na Yanga, ndoa iliyoisha kwa amani na miguno

Tue, 20 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Itachekesha kusema kwamba mmoja kati ya makocha waliodumu sana katika timu kubwa katika miaka ya karibuni hapa nchini hatimaye ameng’oka. Nassiredine Nabi. Anaweza kuwa amekaa misimu mitatu tu Yanga lakini kwa mpira wetu amekaa muda mrefu. Katika kipindi chake unadhani Simba na Azam wamepita makocha wangapi?

Hii ndio hali halisi ya mpira wetu. Tumeiga kutoka kwa wenzetu wa sehemu nyingine za Afrika. Huku kwetu Afrika kocha huwa anadumu kwa msimu mmoja tu. Akidumu sana basi ni misimu miwili. Kocha anaweza kuwa bingwa msimu huu halafu akashika nafasi ya pili msimu unaofuata akakutana na barua ya kuachishwa kazi.

Nabi ameachana na Yanga katika taarifa iliyotufikia usiku wa manane. Sijui kwanini Yanga wanapenda kutoa taarifa zao usiku wa manane. Hata hivyo nilitabiri kwamba huenda Yanga wangempoteza Nabi kabla ya mshambuliaji wao, Fiston Mayele.

Juzi Nabi amenukuliwa katika mtandao wake wa kijamii kwamba hakukuwa na mazungumzo yoyote ya mkataba ambao yalikuwa yameendelea kati yake na Yanga. Ni tarifa iliyoshtua kidogo hasa kwa kuzingatia kwamba Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alituambia kwamba walikuwa na mpango Nabi.

Vyovyote ilivyo ukweli ni kwamba Nabi ana ofa mkononi. Nadhani ana majivuno na ofa ambazo zipo mikononi mwake. Ilikuwa lazima apate ofa baada ya kuifikisha Yanga katika fainali za kombe la shirikisho. Ambacho niliamini awali ni kwamba Yanga wangepambana kumbakiza Nabi.

Hata hivyo naanza kupata wasiwasi baada ya kauli ya Nabi kwamba huenda Yanga tayari walishakuwa na mipango yao mingine kabla hata ya pambano lao la fainali la Shirikisho. Nabi ametuambia kwamba mara ya mwisho kuzungumza na Yanga ilikuwa ni katika pambano lao la makundi dhidi ya TP Mazembe.

Vyovyote ilivyo umekuwa mwisho mwema. Haukuwa mwisho wa kufukuzana. Nabi ameondoka kwa heshima Yanga. Sasa hivi najaribu kujikumbusha kwamba hata machozi yake aliyotoa katika pambano la fainali la mwisho kule Algeria dhidi ya USM Alger alikuwa anamaanisha kwamba hilo lilikuwa pambano lake la mwisho Yanga.

Yanga imetwaa mataji 29 ya Ligi kuu ya Tanzania. Nabi hatakumbukwa sana kwa mataji yake mawili ya Ligi Kuu kwa sababu kuna makocha wengi wametwaa mataji haya. Nabi atakumbukwa zaidi kwa kuipeleka Yanga katika fainali za kombe la Shirikisho. Hakuna kocha aliyewahi kuipeleka Yanga katika hatua za juu zaidi za michuano ya CAF zaidi yake yeye.

Yanga itatimiza miaka 89, Februari mwakani na katika idadi ya makocha wake wanaozidi zaidi ya 200 hakuna kocha ambaye amewahi kufanya kitu ambacho Nabi amefanya. Na kwa namna ambavyo ameondoka nadhani atakumbukwa daima. Labda siku moja akirudi kufundisha Simba anaweza kuvunja daraja lake la heshima na Yanga lakini vinginevyo atakumbukwa daima.

Kwa upande wa Yanga wenyewe wana jambo la kujisifu kwa Nabi. Sawa, alikuwa kocha mzuri lakini wao wenyewe waliweza kumkusanyia wachezaji walio bora. Kama Nabi angekutakana na wachezaji waliokuwa chini ya Mwinyi Zahera sidhani kama Yanga ingeweza kufanya ilichofanya katika msimu ulioisha.

Hii ni kesi ambayo inamkabili Pep Guardiola. kuna watu wanabishana kuhusu ubora wake au ubora wa wachezaji wake. ukweli ni kwamba hapo vimekutana vitu viwili vilivyo bora. Guardiola ni kocha aliye bora, lakini ambaye pia ana wachezaji bora.

Inawezekana kiburi cha Yanga kwa upande mwingine wa kumuachia Nabi kiurahisi kinatokana na kikosi walichonacho kwa sasa na pia pesa walinazo nazo kwa sasa. Labda wanaamini kwamba wanaweza kumpata kocha bora pengine zaidi ya Nabi ambaye atakiunganisha kikosi chao bora.

Inawezekana pia kwamba Yanga wameona wana nafasi ya kumpa kocha aliye bora zaidi kuweza kuwafikisha mbali zaidi ya Nabi. Kumbuka kwamba Yanga wamefanikiwa katika michuano ya Shirikisho tu lakini wana deni kubwa la kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya mabingwa.

Mara ya mwisho kwao kugusa robo fainali ilikuwa mwaka 1998 na wakati huo ilikuwa katika mfumo tofauti kiasi kwamba timu ambayo ingegusa hatua ya makundi ilikuwa tayari imefika katika hatua ya robo fainali. Watani wao wamekwenda hatua hii mara kadhaa wakiwa katika mfumo mpya ambao ni mgumu zaidi.

Yanga hii mpya iliyo chini ya GSM walipoijenga timu yao walitaka kwanza kurudisha ubingwa wa Ligi ambao ulikuwa katika mikono ya Simba kwa miaka minne mfululizo. Lakini pia wakakata kufanya vizuri katika michuano ya Afrika.

Katika michuano ya Afrika iliyo mikubwa ya Ligi ya mabingwa Yanga haikufanya vizuri chini ya Nabi. Wamefanya vizuri katika michuano ya Shirikisho. Labda wanaona wanahitaji kocha ambaye atawapeleka mbali zaidi katika michuano mikubwa zaidi barani Afrika.

Baina yao naona wote wawili wameongezeana wasifu. Yanga imemkuza Nabi na Nabi ameikuza Yanga. Wote wawili wanaweza kupata wateja wengine kwa urahisi tu baada ya kufikia mafanikio ambayo wameifikia kwa pamoja.

Nabi anaweza kupata timu kubwa kwa urahisi tu baada ya kile alichoifanyia Yanga, lakini Yanga pia inaweza kumpata kocha mzuri au wachezaji wazuri kwa urahisi tu baada ya kuchomoza kuwa miongoni mwa timu nzuri Afrika msimu ulioisha.

Kila la kheri kwa Nabi. Binafsi nitamkumbuka kwa baadhi ya mambo ya msingi. Haya ni mambo ya uwanjani zaidi. Nabi alikuwa na uwezo mkubwa wa kuisoma mechi na kufanya mabadiliko kadri mechi inavyoendelea hasa katika kipindi cha pili.

Mara kadhaa katika mwanzo wa kipindi cha pili angeweza kufanya mabadiliko ya wachezaji au mbinu ambayo yangebadili mchezo mzima. Kipindi cha pili Yanga wangeingia tofauti na walivyocheza katika kipindi cha kwanza.

Lakini pia Nabi alikuwa na uwezo mkubwa wa kuibadilisha mechi iliyofuata. Tazama jinsi ambavyo Yanga walicheza na Club Africain hapa Dar es Salaam, halafu tazama namna walivyocheza tofauti kule Tunis. Zilikuwa mechi mbili tofauti.

Tazama Yanga walivyocheza na USM Alger hapa Dar es Salaam, halafu tazama namna walivyocheza vizuri kule Algeria. Zilikuwa mechi mbili tofuti. Huu ulikuwa ubora mkubwa wa Nabi ambao makocha wengi huwa hawana.

Lakini zaidi nitamkumbuka Nabi kwa kuwa kocha mwenye uwezo mkubwa wa kuchukua maamuzi magumu uwanjani. Kuna wakati alikuwa anaweza kumuweka benchi mchezaji kama Aziz Ki kwa urahisi tu licha ya kuja nchini kwa mbwembwe.

Ni wachezaji wachache ambao hawakukumbana na makali yake pindi walipopoteza ubora uwanjani. Ukiachana na Mayele pamoja na kipa, Djigui Diarra, wachezaji wengi wa Yanga walikumbana na makali ya Nabi pale walipopoteza fomu au kutokuwa katika wakati mzuri uwanjani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: