Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi aandaa sapraizi nyingine

KOCHA NABI TUNISIA Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi

Sun, 28 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wananchi wana jambo lao pale Kwa Mkapa. Mabingwa hao wa Tanzania jioni ya leo inatarajiwa kushuka uwanjani kupepetana na USM Alger ya Algeria katika pambano la mkondo wa kwanza la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku Kocha Nasreddine Nabi akiandaa sapraizi ya aina yake.

Kocha huyo aliyeweka rekodi ya kuwa wa kwanza kuifikisha Yanga hatua hiyo katika michuano ya CAF, anatarajiwa kuwasapraizi Waarabu ambao huenda walijifungia vyumbani kabla ya kuja nchini ili kukisoma kikosi hicho cha wawakilishi hao wa nchini.

Inawezekana kabisa benchi la ufundi la USMA limekomaa kumsoma zaidi Fiston Mayele na pengine Kennedy Musonda kisha kujiandaa kuwakaba wasilete madhara kwenye mchezo wa leo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni na kuchezeshwa na mwambuzi Jean-Jacques Ndala Ngambo kutoka DR Congo atakayesaidiwa na Zakhele Siwela wa Afrika Kusini na Olivier Kabene (DR Congo) huku mwamuzi wa akiba mezani Ahmad Heeralall kutoka Mauritius.

Hata hivyo, wasilojua USM Alger ni kwamba nafasi ya winga na ile ya kiungo mshambuliaji zinaonekana zinaweza kuwa silaha muhimu kwa Nabi katika mechi hiyo ya fainali, kwani kocha huyoamekuwa akifanya mabadiliko ya wachezaji mara kwa mara kwa nafasi hizo.

Kocha Nabi amekuwa akiwabadili achezaji wa nafasi hizo, mabadiliko yanaonekana kuwa mpango mkakati wa benchi la ufundi la timu hiyo katika kuvuruga mipango na mbinu za wapinzani katika mechi mbalimbali za michuano hiyo kwa msimu huu.

Tofauti na wachezaji wa nafasi nyingine, katika mechi 12 zilizopita za Shirikisho Afrika, mabadiliko ya wachezaji ya Yanga yamekuwa yakiwagusa zaidi mawinga na wachezaji wanaopangwa kucheza nyuma ya mshambuliaji wa kati.

Katika mechi ya nyumbani dhidi ya Club Africain, Yanga ilimuanzisha Tuisila Kisinda na Bernard Morrison ambao baadaye walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Farid Musa na Jesus Moloko huku nafasi ya nyuma ya mshambuliaji wa kati akipangwa Stephane Aziz Ki.

Lakini, Nabi alibadilisha ramani ya vita katika mchezo uliofuata ugenini dhidi ya Club Africain ambao walishinda bao 1-0, kwa kuwapanga Moloko na Morrison katika winga na nafasi ya zao zikichukuliwa na Farid na Bakari Mwamnyeto huku katika nafasi ya kiungo mshambuliaji nyuma ya straika wa kati akipangwa Salum Abubakar 'Sure Boy' aliyetoa pasi ya bao lililofungwa na Aziz KI.

Licha ya Sure Boy kuendelea kupewa nafasi katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Monastir ugenini, Nabi alifanya badiliko katika nafasi moja ya winga kwa kumuanzisha Kisinda katika upande mmoja na mwingine kumpa Moloko na wawili hao wakafanyiwa mabadiliko katika mechi hiyo kuwapisha Musonda na Farid.

Tofauti na mechi ya Monastir, iliyofuata dhidi ya TP Mazembe, katika winga walipangwa Moloko na Musonda huku nafasi ya kiungo nyuma ya mshambuliaji akipangwa Mudathir Yahya waliotolewa baadaye kuwapisha Moloko, Kisinda na Clement Mzize na mchezo uliofuata ugenini dhidi ya Real Bamako, katika winga walianzishwa Moloko na Musonda waliokuja kuwapisha Kisinda na Zawadi Mauya huku Mudathir akifanyiwa mabadiliko kumpa nafasi Farid.

Mabadiliko ya wachezaji wa nafasi hizo yaliendelea katika michezo yote iliyofuata kuanzia ule wa nyumbani dhidi ya Real Bamako hadi wa mwisho wa nusu fainali ugenini waliocheza na Marumo Gallants.

Na kuthibitisha hilo, wachezaji wa nafasi hizo wameonekana kugawana na kutopishana sana kwa dakika za kucheza kulinganisha na wale wa nafasi nyingine.

Ukiondoa Moloko ambaye ndio anaonekana kutumika sana kutokana na kucheza kwa dakika 733, wengine wameonekana kukaribiana kwa dakika ambazo Nabi amewatumia katika mashindano hayo.

Katika nafasi ya kiungo mshambuliaji, anayeongoza ni Aziz Ki aliyecheza kwa dakika 604 huku Mudathir akitumika kwa dakika 593 na Sure Boy akipata nafasi kwa dakika 447.

Kwa upande wa nafasi ya winga, ukiondoa Moloko, wengine na dakika zao kwenye mabano ni Musonda (434), Kisinda (427), Morrison (187) na Farid (157).

Hata kwenye mchezo wa leo kama USM Alger watakuwa wamekisoma kikosi kilichoing'oa Marumo na kudhani ndicho kinachoweza kuwaanzishwa, basi wajiandae na sapraizi, kwani kocha Nabi amepangga kuja kivingine akiwa na lengo la kupata ushindi mzuri nyumbani kabla ya kwenda ugenini.

Kocha Nabi alisema mabadiliko ambayo amekuwa akiyafanya kwa wachezaji wa nafasi hizo ni ya kawaida na yanachagizwa na ubora wa kila mmojawapo.

"Kila mechi inakuwa na mpango wake na kila mchezaji anapaswa kuwa tayari kucheza na kuisaidia timu kulingana na mahitaji ya wakati huo. Najivunia wachezaji wangu wamekuwa wakitimiza vyema majukumu yao jambo linalonipa wigo mpana wa kumtumia yeyote," alisema Nabi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: