Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Na Msuva? Hii imeenda Yanga

Msuva Ml.jpeg Simon Msuva

Sat, 22 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hisia za wengi leo zinaelekezwa kwa nyota saba waliosajiliwa na Yanga katika dirisha kubwa la usajili linaloendelea wakati itakapokabiliana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Mkapa, saa 1 usiku.

Wachezaji hao ni Gift Fred, Maxi Nzengeli, Mahlatse 'Skudu' Makudubela, Nickson Kibabage, Jonas Mkude, Yao Attohoula na Pacome Zouzoua.

Hamu kubwa ni kuona ni kwa namna gani nyota hao wanaweza kuingia katika kikosi cha kwanza cha Yanga, ambacho hakijaondokewa na kundi kubwa la wachezaji katika dirisha hili la usajili linaloendelea huku wakionekana kuongeza ushindani wa nafasi katika kikosi hicho.

Lakini haitoishia kwa nyota hao tu, bali pia kutakuwa na sura mpya kadhaa zitakazokuwepo kwenye benchi la ufundi zikiongozwa na kocha mkuu, Miguel Gamondi na msaidizi wake, Moussa Ndaw, ambao wamechukua nafasi za Nasreddine Nabi na Kaze Cedrick walioondoka.

Metacha kuandika historia

Kwa kuwemo kwenye kikosi cha Yanga leo, kipa Metacha Mnata ataweka historia ya kuwa mchezaji pekee aliyemo kikosini, ambaye alikuwa kwenye kikosi cha Yanga kilichoshiriki tamasha la kwanza la Wiki ya Mwananchi.

Wakati Metacha akiweka rekodi hiyo, Bakari Mwamnyeto atashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza idadi kubwa ya mechi za kilele cha Wiki ya Mwananchi, huu utakuwa mchezo wake wa nne akiwa ameshacheza mitatu iliyopita hadi sasa dhidi ya timu za Aigle Noir, Zanaco na Vipers.

Yanga bila Mayele

Baada ya kuwapa raha kwa misimu miwili tofauti, mshambuliaji Fiston Mayele hatokuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kitakachotambulishwa leo kwa vile ameachana na timu hiyo na kujiunga na Pyramids ya Misri.

Mbali na Mayele, wachezaji wengine ambao hawatokuwa sehemu ya kikosi cha Yanga leo ni Yannick Bangala, Bernard Morrison, Tuisila Kisinda na Djuma Shaban.

Uteja kufutwa

Ushindi dhidi ya Kaizer Chiefs leo bila shaka utamaliza nuksi, ambayo Yanga wamekuwa nayo katika mechi za kilele cha Wiki ya Mwananchi na katika awamu nne zilizopita imepata ushindi mara moja tu ilipoichapa Aigle Noir ya Burundi kwa mabao 2-0, 2020.

Kabla ya kuichapa Aigle Noir, 2019, mwaka mmoja nyuma ililazimishwa sare ya 1-1 na Kariobang Sharks ya Kenya, 2021 ikapoteza dhidi ya Zanaco FC ya Zambia kwa mabao 2-1 na 2022 ikachapwa 2-0 na Vipers ya Uganda.

Mashabiki waahidiwa raha

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi leo ili kuisapoti timu.

"Kesho ni siku kubwa kwa mashabiki wa Yanga pamoja na sisi wote tunakwenda kupata nafasi ya kusherekea kufunguliwa kwa msimu huu mpya tukiwa na matarajio ya kuendelea kuipambania Klabu hii kubwa yenye historia kubwa.

"Kwenye upande wa timu bado tuko kwenye maandalizi, na mchezo wa kesho dhidi ya Kaizer Chiefs. Tutautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi yetu kwa msimu ujao," alisema Gamondi.

Nyota mpya wa Yanga, Makubela alisema wamejiandaa kuwapa mashabiki thamani inayostahili.

"Tupo kwenye maandalizi ya awali kujiandaa na msimu mpya. Kwa niaba ya wachezaji wenzangu ujumbe wetu kwenu tunaomba kesho mje kwa wingi tumewaandalia burudani nzuri," alisema Makubela.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: