Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee Manara afunguka ya moyoni Yanga

Mzee Manara Mayele .jpeg Mzee Manara afunguka ya moyoni Yanga

Sat, 1 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sunday Manara anasema amecheza Yanga kwa kipindi kirefu, hivyo analo jambo la kuwafundisha watu kuhusu uongozi, anaamini akipewa uongozi anaweza kufanya mambo mazuri zaidi kutokana na uzoefu wake wa soka, lakini wengi wanahisi anaweza kuwanyima ugali.

Kiungo huyo wa ushambuliaji anasema zamani wachezaji walikuwa bora kwasababu walikuwa karibu na mashabiki na viongozi, hivyo iliwarahisishia kushauriwa na kuwa bora na uongozi kufanya kazi yao kwa uweledi.

“Uongozi ndio msingi wa maendeleo na soka letu kukua kwani nina imani wachezaji wa zamani wana mchango kwa vijana kwani wameona mengi.

“Iwekwe mijadala ya wazi ili kuwapa fursa watu wotoe maoni na kukosoa mahali wanapoona hapako sawa,hapo viongozi watajua wafanye nini kwani Kidole kimoja hakiwezi kuvunja chawa.”

SHIDA YA WAZAWA

Sunday anasema wachezaji wa zamani walikuwa bora kwa sababu walikuwa na mapenzi ya dhati na walichokuwa wanakifanya na waliangalia walipotoka na kuwapa mwanga sehemu za kurekebisha.

Anaongeza faida za kuangalia wapi umekosea ni kubwa kwani itakufanya kutokurudia makosa, mchezaji au uongozi anapojua makosa yao inakuwa rahisi kuwa na maendeleo.

“Simba kwa kipindi cha miaka miwili au mitatu nyuma ilikuwa na timu yenye kikosi bora Afrika lakini kwa kutokuangalia wapi wamekosea wamejikuta na timu ambayo kila mtu anainyooshea kidole.

“Rekodi zitakufanya kujua wapi umekosea, kumuuza wachezaji kama Luis Miquissone na Clatous Chama kwenda Morocco na Misri sio maendeleo ila unapowatoa viungo unaiathiri timu kwa sababu kikosi bora kinaweza kuleta pesa chenyewe.”

NAFASI YA WACHEZAJI WAZAWA

Sunday anasema suala la wageni kupewa kipaumbele kuliko wazawa halikubali, kwasababu wageni wengi walioletwa nchini ni wachache tu ndio wazuri wengi wao ni wabovu.

Anasema kuwaheshimu sana wageni kunawafanya wazawa kujihisi hawana thamani na kwa kutokupewa nafasi kunawafanya kupoteza ubora wao.

“Bado sijauona ubora wa wageni, kwani bado tunao wazawa wengi ambao wako bora ila tunakosea tunapowapa wageni nafasi kubwa hata kama hawana uwezo.”

UKUBWA DAWA

Wachezaji wa zamani hawapewi nafasi katika soka kwa sababu walioshikilia nafasi hizo wanajua kuwa hawastahili na wanahisi udhaifu wao utajulikana kama watawaruhusu wazee kutoa ushauri.

“Nchi za wenzetu zinathamini mchango wa wachezaji wa zamani na unapokuwa na mtu mwenye jicho la kuona mbali anaweza kuwapa tahadhari mapema kutokana na maamuzi yanayofanywa.

“Mazingira yanaonyesha bado wakongwe tunahitajika sana katika soka letu, kwasababu sisi tuilicheza kikosi kizima tukiwa wazawa na tulikuwa bora kuliko sasa ijapokuwa mazingira hayakuwa rafiki na tulifika mbali tofauti na sasa hawafiki popote wakiwa hawana ubora kama wetu.”

JICHO LAKE

Sunday anasema analiona soka likiendelea kupanda na kushuka kwani linaongozwa na wafanyabiashara na sio wapenzi wa mpira, hivyo hawana uchungu na hata timu zikiporomoka.

Anasema kama makosa ya nyuma hayatasahihishwa basi Tanzania haitafika mbali na mipango ya miaka mitano au kumi inaweza kuwekwa lakini isiweze kutimia kwa nchi kushindwa kufika inapotaka.

“Tunahitaji kubadilisha namna tunavyoongoza mpira, tuache kuhisi kama ni biashara kwani hatukuzi vya kwetu ila tunanunua wachezaji wa nje ili tupate magoli na sio ubora.

“Tunaweza kuuza wachezaji wetu wenyewe kama watakuwa bora na ili kufikia huko kunahitajika muda na maboresho makubwa ambayo yatatupa pesa.”

MCHEZAJI WAKE BORA

Sunday anasema Clement (sasa Walid) Mzize, ni wachezaji bora kwake japokuwa nafasi yake inachukuliwa na wageni ila ana ubora kila anapopata fursa.

Pia, anamtaja Mohammed Hussein Tshabalala kuwa ni bora sana kati ya wachezaji wa Tanzania.

Anasema kuna wachezaji wengi bora ila kama hawapewi nafasi ya kucheza mara kwa mara hawawezi kuonekana kwani uwanjani ndipo kunakompa sifa mchezaji sio benchi.

“Mchezaji bora ni yule anayecheza mechi 30-40 kwa msimu, hicho ndicho kipimo kwani atakutana na misukosuko mingi ambayo itamfanya kuwa imara na kujiamini.

“Kujiamini ndio kunakomfanya mchezaji kuwa bora kwani anapocheza mara kwa mara lazima atakua kiakili na kimbinu.”

WOSIA

Sunday anasema wachezaji wapende kukosolewa na watafute fursa za kurekebishwa ili wasirudie makosa lakini wawe na mapenzi ya dhati na mchezo wanaoucheza na kuachana na tamaa ya pesa.

Anasisitiza mchezaji anatakiwa awe na ratiba yake na kuwa na chati ya uwezo inayopanda na sio inayoshuka.

Mchezaji hawezi kuwa bora kama hatakubali kujiangalia wapi anakosea na afanye nini ili kujirekebisha.

“Lawama zinaumiza ila ukijishusha na kuzifanyia kazi, basi lazima utakuwa bora pia kutokata tamaa kunamfanya na kuwa na wivu wa kufanya vizuri, ogopa sifa za kila mara hazitakufikisha mbali.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: