Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtihani wa Gamondi kwa makocha

Yanga Gamondi As Miguel Gamondi.

Fri, 1 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna utata kwamba Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kwa sasa amekuwa habari nyingine baada ya kuifanya timu hiyo kuwa kuanza vizuri kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu yoyote kwa sasa kwenye Ligi Kuu ikijua inakwenda kukutana na Yanga huwa inajipanga zaidi, kwani wanajua mchezo huo hauwezi kwenda kuwa mwepesi hata kidogo.

Kwa muda mchache, Gamondi ameifanya timu hiyo kutokuwa na nyota wa kumtegemea katika kikosi chake, hali ambayo inawafanya wachezaji wake kupambane.

Hali hiyo inawapa mtihani makocha wa timu pinzani kukabiliana naye, kwani mbinu za Gamondi zimekuwa zikiwazidi kete pindi inapokutana na kikosi chake.

Yanga ya sasa imeonekana kuwa na spidi ya kutosha ndani ya uwanja ikiwa na mpira kwenda kwa mpinzani kuanzia kwa mabeki wake wakishika mpira, na kasi huongezeka inapofika katikati ya uwanja.

Timu pinzani inalazimika kubadili mbinu inapokutana na Yanga, jambo ambalo lilianza kwa KMC, ambayo kupitia kwa kocha wake, Abduhimid Moallin alikiri kubadili mbinu kuendana na kasi ya Yanga.

Si kazi pekee ya beki kukaba kwa sasa ndani ya Yanga, bali ni kila mchezaji jambo ambalo linawasaidia pia kuupokonya mpira kwa wapinzani na kurejea miguuni mwao.

Gamondi amezidi kuwachanganya wapinzani wake, kwani ni ngumu kumtabiria kikosi chake ataanza na yupi kwa sababu ni kawaida kubadili wachezaji watano wa kikosi cha kwanza kwenye kila mechi.

Kocha huyo raia wa Argentina, Gamondi amekuwa akibadili wachezaji mara kwa mara, japokuwa eneo la kiungo ameendelea kuwaamini zaidi Khaldi Aucho na Mudathir Yahya.

Mbinu nyingine ambayo kocha huyo anaitumia kwa sasa ni kuyagawa mabao yake tofauti na msimu uliopita ilivyokuwa alikuwa anaangaliwa zaidi Fiston Mayele aliyetimkia Pyramid inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Katika mechi nne za kimashindano zilizopita, Yanga imefunga mabao 17, ikiruhusu bao moja la penalti dhidi ya ASAS Djibouti kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mabao hayo, mawili yamefungwa na mabeki (Dicksom Job na Yao Attohoula), matano yamefungwa na washambuliaji wa kati (Kennedy Musonda, Hafiz Konkoni na Clement Mzize), huku 10 yakifungwa na viungo, Stephen Aziz, Max Nzengeli, Mudathir, Pacome Zouzoua na Aziz Ki Ki.

Makocha wa soka wanaitaja Yanga kama timu yenye mbinu sahihi katika michezo sahihi, huku Gamondi akifanikiwa kuitoa timu hiyo katika muundo wa msimu uliopita na kuitengeneza atakavyo.

Kocha wa Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship, Aman Josiah alisema Gamondi amepata bahati ya kukuta timu ipo kwenye misingi imara na kuendeleza zaidi.

"Timu ipo kwenye hali ya ushindi kwahiyo yeye ameendelea kutengeneza mbinu na saikolojia zaidi kwa wachezaji wake na ndiyo maana wameendelea kufanya vizuri.

"Yanga ni timu mojawapo ambayo ilikuwa na maandalizi mazuri ya msimu mpya, usajili mzuri wamefanya, kwahiyo hata wale ambao wamesajili wanatakiwa kupongezwa," alisema Josiah.

Kocha wa zamani wa Yanga na Ruvu Shooting, Charles Mkwasa alisema usajili wa wachezaji wa kikosi chake hicho ndiyo chachu kubwa ambayo inafanya timu hiyo ifanye vizuri.

Mkwasa alisema wachezaji wote wameingia katika mfumo wa kutafuta bao kwa ajili ya timu kuhakikisha kikosi chao kinapata ushindi katika kila mechi.

"Kazi ya ukocha inataka matokeo mazuri, leo anazungumziwa kwa sababu matokeo ni mazuri, lakini Yanga ya sasa ina wachezaji wazuri ambao wanaweza kucheza ligi yoyote hata Ulaya," alisema Mkwasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: