Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka 88 ya kibabe Yanga

Mashabiki Yanga Kwa Mkapa Mashabiki wa Yanga SC

Sat, 22 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Waliosema siku haigandi hawajakosea. Leo Jumamosi, wababe hao wa soka nchini na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Yanga inahitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Kilele hicho kinafanyika leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, kikipambwa na burudani mbalimbali ikiwamo ya muziki kisha saa 1:00 usiku kikosi kipya cha Yanga cha msimu ujao kitashuka uwanjani hapo kuvaana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Tamasha hilo la tano kwa Yanga tangu lilipoasisiwa mwaka 2019, limekuja wakati klabu hiyo ikitimiza Miaka 88 tangu ilipoanzishwa Februari 11, 1935, japo historia inaonyesha chimbuko iliasisiwa kati ya 1926-29 kwa lengo la kuwaunganisha Waafrika kudai uhuru wa Tanganyika.

Inaelezwa Yanga iliundwa na wananchi wanyonge, wengi wakiwa manamba wa mashambani, wachuuzi na waafrika ambao walikuwa wakitengwa mbele ya watu weupe na hii imechangia mabosi wa klabu hiyo kuasisi tamasha hilo kufahamika Wiki ya Mwananchi.

Wanaoifahamu zaidi Yanga wanasema ilianza kwa jina la Jangwani Boys kisha kuja kuitwa Navigation kabla ya kubadili jina miaka ya 1930 na kujiita Taliana FC.

Hata hivyo mwanzoni mwa 1930, Yanga ilibadilishwa jina na kuwa, New Young na kisha kuasisiwa rasmi mwaka 1935 na miezi michache baadaye timu iligawanyika kwa baadhi ya wachezaji kujiengua na kwenda kuasisi klabu ya Sundeland (Simba) iliyozaliwa Agosti 1936.

Upo mkanganyiko juu ya tarehe rasmi ya kuasisiwa kwake, baadhi wakisema ni Juni na wengine wakidai ni Februari 11, hata hivyo ni kwamba Yanga ni moja ya klabu kongwe nchini na barani Afrika, kwani leo klabu hiyo inaadhimisha pia miaka 88 tangu ilipoasisiwa. Umri huu si mdogo!

REKODI ZA KIBABE

Pamoja na kuwa moja ya klabu kongwe nchini, Yanga ambayo ilianza kulitumia jina hilo mwanzoni mwa miaka ya 1970 baada ya agizo la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume aliyezitaka timu zote kuwa na majina ya kiafrika, pia Yanga ina rekodi tamu na za kibabe.

Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na kuandika historia ya kufika robo fainali ikifanya hivyo mara mbili mfululizo, yaani 1969 na 1970.

Kitu cha ajabu ni kwamba Yanga ilifika hatua hiyo na kucheza na Asante Kotoko ya Ghana na moja ya mechi yao iliamuliwa kwa kurushwa kwa sarafu baada ya kushindwa kupata mbabe katika mechi zote mbili za awali.

Achana na rekodi hiyo, Yanga pia ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifanya hivyo mwaka 1998, msimu mmoja tu tangu Klabu Bingwa Afrika ibadilishwe mfumo wake mwaka 1997.

Pia Yanga inashikilia rekodi ya kuwa klabu pekee mpaka sasa ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikifanya hivyo misimu miwili tofauti.

Yanga ilicheza hatua hiyo mwaka 2016 na kurudia tena 2018, ingawa mara zote imeshindwa kuvuka hatua hiyo kwenda robo fainali.

Kubwa zaidi ni kwamba msimu uliopita Yanga iliweka historia ya kusisimua baada ya kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa nchi ya kidole baada ya matokeo ya mwisho kuwa sare ya 2-2, lakini USM Alger ya Algeria ilitwaa kwa faida ya bao la ugenini. Yanga ilipoteza nyumbani mabao 2-1 na kwenda kushinda ugenini 1-0.

Mbali na rekodi hiyo, Yanga pia ilikuwa klabu ya kwanza Tanzania Bara kucheza robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1995, mwaka mmoja tu baada ya Malindi kufika hatua 1994.

YAPIGA BAO

Ni kweli Simba ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ikitwaa taji mara sita, lakini Wekundu hao kwa Yanga wamekaa.

Ndio, licha ya Simba kushikilia rekodi ya kubeba taji hilo mara nyingi, lakini hawajawahi kutwaa nje ya Tanzania, tofauti na Yanga ambao inashikilia rekodi mpaka sasa kwa kufanya hivyo.

Vijana wa Jangwani waliandikia historia kwa kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 1993 nchini Uganda, tena ikienda Kampala kinyonge kulinganisha na watani wao walioenda kwa ndege wakiwa ndio watetezi na kurudi mikono mitupu.

Kama kuna watu waliodhani Yanga ilibahatisha mwaka huo, basi walikosea kwani ilirejea tena rekodi hiyo mwaka 1999 walipoenda kutwaa ubingwa nchi Uganda kwa mara nyingine.

Rekodi zinaonyesha hadi sasa Yanga imetwaa taji hilo mara tano ikiwa nyuma ya taji moja dhidi ya watani wao, huku Azam FC ikifuatia kwa kulibeba mara mbili, 2015 na 2018.

HUKO BARA SASA

Licha ya kubeba mataji matano ya Afrika Mashariki na Kati, lakini Yanga bado ni Baba Lao katika Ligi Kuu ya Bara kwani tangu ilipoasisiwa mwaka 1965 imetwaa ubingwa mara 29.

Wao ndio vinara wakifuatiwa na watani wao waliobeba mara 22 hadi sasa, pia ndio wababe wa kwanza katika mechi ya watani walipofumua Simba bao 1-0 Juni 7, 1965.

Katika mchezo huo bao pekee la Yanga liliwekwa kimiani na Mawazo Shomvi kabla ya pambano kuvunjika dakika ya 80 na kugoma kurudiana na watani wao waliokuja kupewa ubingwa mwaka huo wa kwanza kwa kuasisiwa kwa Ligi ya Bara.

Pia kama hujui ni Yanga haohao iliyokuwa ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani kwa kuifunga Simba mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa Juni 1, 1968.

Mabao ya Yanga yaliwekwa kimiani na Maulid Dilunga na Saleh Zimbwe waliyefunga mawili kila mmoja na Kitwana Manara 'Popat'.

Hata hivyo ni Yanga hao hao waliokuja kuandikia historia ya aibu kwa kufumuliwa mabao 6-0 na watani wao Julai 19, 1977 ikiwa sasa imetimia miaka 46 inaahaha kufuta aibu hiyo bila mafanikio.

Aidha Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kunyakua ubingwa wa nchi mara tano mfululizo ikifanya hivyo miaka ya 1968-72, japo Simba nayo ilikuja kufanya hivyo baadaye kati ya 1976-80 na misimu minne iliyopita ilibeba mara mfululizo.

Lakini ni Yanga tena waliandika rekodi ambayo mpaka leo haijawahi kufikiwa na timu yoyote katika Ligi Kuu ikiwamo Simba kwa kutwaa mataji mara tatu tatu mfululizo katika vipindi vitatu.

Ilitwaa mara tatu mfululizo kwa mara ya kwanza mwaka 1991-93 kisha ikarudia tena 1996-98 na 2007-2010, ingawa Simba ilijibu misimu minne mfululizo kulitwa taji hilo kabla ya msimu uliomalizika Juni 29, Yanga kuwazidi akili. Hata hivyo Simba misimu nne mfululizo iliyopita iluitwaa taji hilo kabla ya Yanga kuwanyang'anya kwa misimu miwili ikibeba pia ASFC na Ngao ya Jamii.

KAUNDA ILIFUNIKA

Kwa sasa Simba inatambia uwanja wake wa mazoezi uliopo, MO Simba Arena Bunju, huku Azam wakitangulia mapema kuwa na uwanja wa kisasa, lakini unaambiwa Yanga ndio baba lao toka zamani.

Yanga ndio iliyokuwa klabu ya kwanza kumiliki uwanja wake mwenyewe, walipoujenga Uwanja wa Kaunda, uliokuwa mitaa ya Jangwani na Twiga yalipo makao yao makuu.

Uwanja huo uliifanya Yanga kufunika kwa klabu za Tanzania kwani walikuwa wakitambulisha vikosi vyao kuanzia za watoto, vijana mpaka timu yao kubwa kwenye uwanjani huo.

Pia waliutumia kwa mechi zao mbalimbali za kirafiki kabla ya mafuriko ya mara kwa mara kuwatibulia na kuufanya uwanja huo ufe, japo hivi karibuni walitaka kuufufua upya na kushindikana.

Lakini kama hujui, mbali na uwanja,Yanga pia ndio klabu iliyokuwa na jengo linaloweza kuwahifadhi wachezaji na viongozi wake kwenye makao yao makuu, mbali na kuwa klabu ya kwanza nchini kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wachezaji fedha zao benki.

MATAJI KIBAO

Mbali na kubeba mataji mengi ya Ligi Kuu, Yanga pia inashikilia rekodi kadhaa za kubeba mataji mengine mbalimbali ikiwamo ya michuano ya Ligi Kuu ya Muungano (sasa haipo, iliyoshirikisha timu za Bara na Zanzibar).

Imetwaa michuano ya Kombe la FA/ASFC mara saba ikiwa ni rekodi ikifanya hivyo 1967, 1974, 1999, 2001, 2015-16, 2021-22 na 2022-23), Kombe la Nyerere, Kombe la Tusker, Kombe la CCM, Kombe la Hedex mbali na kubeba pia Ngao ya Jamii mara saba ikiwa nyuma ya Simba iliyotwaa mara tisa.

NYOTA NJE YA NCHI

Simba kwa sasa inajimwambafai kwa Mbwana Samatta, kucheza Ligi Kuu ya England, huku ikitamba kuwa ni klabu inayoachia nyota wake wengi kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Hata hivyo ukweli usiopingika, Yanga ndio klabu ya kwanza kuachia nyota wake kucheza soka nje ya nchi na kutoa mchezaji wa kwanza kucheza soka barani Ulaya.

Kama unabisha, pole yako kwani mwaka 1977 nyota wake, Sunday Manara 'Computer', alitimka Uholanzi kukupiga soka la kulipwa katika klabu ya Heracles na kumkutanisha na wakali waliotamba enzi hizo duniani kama Ruud Krol, Jaan Rep, Joan Neeskens, Van Hangem na gwiji lao, Johan Cruyff Mbali na mchezaji huyo, lakini Yanga pia iliwahi kuchezwa na Shaaban Nonda 'Papii' ambaye amewahi kuwika klabu mbalimbali barani Ulaya, kitu kinachoifanya isiwe klabu ya kuichukulia poa.

Aidha, Yanga imefundishwa na makocha mbalimbali waliowahi kutamba Ulaya na duniani kwa ujumla ambao waliitengenezea mfumo bomba ulioifanya hadi leo kuwa moja ya klabu tishio nchini, licha ya kwamba yenyewe imejifedlisha kwenye anga za kimataifa.

MIGOGORO KIBAO

Licha ya mafanikio makubwa kisoka nchini, lakini Yanga inaweza kuwa klabu iliyowahi kukumbwa na migogoro iliyoacha historia nchini, mbali na ule mgawanyiko uliokuja kuizaa Simba 1936.

Yanga ilikaribia kufutika kama sio hekima zilizotumika kutuliza mambo wakati wa mgogoro wa kihistoria ulitokea mwaka 1975 na kusababisha kuzaliwa kwa Pan Africans na kuibuka kwa utani wa Kandambili na Raizon.

Aidha Yanga miaka ya katikati ya 1990 ilikumbana na kisanga kingine kilicholazimisha hadi serikali kuingilia kati ya Yanga Asili na Yanga Kampuni iliyosababisha kutimuliwa kwa timu nzima.

Mzozo huo uliibuka kutokana na pande mbili za Wafadhili waliokongozwa na kina Abbas Gulamali, Mohammed Viran na wenzake dhidi ya uongozi wa George Mpondela 'Fidel Castro' na wenzake kiasi Waziri wa Mambo ya Ndani enzi hizol, Augustine Mrema kuingilia kati.

Kifupi ni kwamba katika miaka 88 ya uhai wa Yanga klabu hiyo imepita kwenye vipindi tofauti vyenye ladha ya utamu wa asali na uchungu wa shubiri.

Hata hivyo mwisho wa yote ni kwamba Yanga bado inaendelea kupambana ikibaki kuwa klabu ya kipekee na ya kihistoria nchini ikiendeleza falsafa yao ya Daima Mbele Nyuma Mwiko. Happy Birthday Dar Young Africans a.k.a Yanga Chama la Mwananchi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: