Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele: Tunachafua mpaka fainali CAF

Mzize MAYELE Fiston Mayele

Wed, 5 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, staa wa Yanga, Mkongomani, Fiston Mayele, ameibuka na kutamka kuwa, hakuna atakayewazuia na sasa wanaitaka fainali ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kauli hiyo imekuja mara baada ya Yanga, Jumapili iliyopita kufanikiwa kupata ushindi wa bao 0-1 ugenini dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa mwisho wa Kundi D kunako michuano hiyo.

Yanga imemaliza Kundi D wakiwa wanaoongoza baada ya kukusanya pointi 13 sawa na US Monastir, Real Bamako wana 5 na TP Mazembe 3.

Akizungumza nasi, Mayele alisema malengo ya awali yalikuwa ni kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo, lakini sasa hivi yamebadilika, hivyo wanaitaka fainali msimu huu.

Mayele alisema kikubwa kinachompa jeuri ya wao kucheza fainali ni ubora walionao huku wakiwa na wachezaji wenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano mikubwa Afrika.

Aliongeza kuwa, wapo tayari kukutana na yeyote watakayepangwa naye robo fainali.

“Sioni sababu yoyote ya kushindwa kufuzu kucheza hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani tuna kila sababu, kama wachezaji wapo bora, wenye uwezo na uzoefu mkubwa wa kucheza michuano hii.

“Malengo ya kwanza yalikuwa ni kufika hatua ya makundi ya michuano hii, lakini baada ya kufuzu Robo Fainali, sasa tumeongeza malengo, hivyo tunataka kucheza fainali.

“Tupo tayari kukutana na timu yoyote katika hatua hii ya robo fainali, kwani hakuna tunayemuogopa, hivyo tusubirie hiyo droo itakayochezeshwa kwa ajili ya kumjua mpinzani wetu,” alisema Mayele.

Kesho Jumatano, droo ya robo fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa ambapo timu zilizofuzu kwa kuongoza makundi yao ni Marumo Gallants (Afrika Kusini), ASEC Mimosas (Ivory Coast, ASFAR (Morocco) na Yanga (Tanzania).

Zilizoshika nafasi ya pili ni USM Alger (Algeria), Rivers United (Nigeria), Pyramids (Misri) na US Monastir (Tunisia). Yanga inaweza kupangwa kucheza dhidi ya USM Alger, Rivers United au Pyramids.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: