Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Yanga: Tulistahili Ubingwa

Mastaa Yanga Ubingwa Mastaa Yanga: Tulistahili Ubingwa

Tue, 16 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mastaa wa Yanga tayari wapo Afrika Kusini walipoenda kwa ajili ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants, ikiwa ni muda mfupi tu tangu walipoiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kutamba walistahili kutetea taji hilo.

Yanga ilibeba taji hilo linalokuwa la 29 katika ligi hiyo tangu ilipoasisiwa mwaka 1965 kwa kuifunga Dodoma Jiji kwa mabao 4-2 kwenye mechi kali iliyopigwa juzi Uwanja wa Azam Complex yakifungwa na Kennedy Musonda, Farid Mussa na Mudathir Yahya aliyefunga mabao mawili, huku Collins Opare na Seif Karihe waliifungia Dodoma.

Timu hiyo imebeba taji ikiwa na michezo miwili mkononi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons na kuwafanya mastaa wa timu hiyo kutamba kwamba walistahili kwa namna walivyojitoa tangu mwanzoni mwa msimu huo.

Wakizungumza wachezaji hao akiwamo beki Dickson Job alisema msimu huu ulikuwa mgumu lakini kama wachezaji walijipanga vizuri kuhakikisha wanatimiza malengo ya kutwaa ubingwa na hatimaye yametimia.

"Tulikuwa bora sana na tumestahili kupata hiki tulichopata.

"Changamoto kubwa kwangu msimu huu ilikuwa kwenye ushindani wa namba uliopo ndani ya timu yetu, lakini kikubwa ni mimi kama mchezaji kuelewa nahitaji nini na kuweza kufanya vizuri na kupata nafasi kila wakati.

"Ushindani wa namba unadhihirisha jinsi tulivyokuwa bora msimu huu na umesaidia kuifanya timu yetu kuwa imara na kutwaa ubingwa msimu wa pili mfululizo, " alisema Job.

Naye straika, Fiston Mayele alisema msimu huu ulikuwa mgumu na ndio maana wamechelewa kuchukua ubingwa.

"Msimu uliopita tulichukua ubingwa mapema zaidi tofauti na msimu huu ambao tumetwaa ubingwa tukiwa bado na mechi mbili tu, hii inaonyesha msimu huu ligi ilikuwa ngumu.

"Ubora wa timu yetu unasababisha timu nyingi zikiwa zinakuja kutukabili zinajitahidi na kupinguza makosa hivyo kufanya mechi zetu kuwa ngumu sana, " alisema Mayele.

Beki wa pembeni Kibwana Shomari alisema wamefanya kazi kubwa msimu huu hadi kuchukua ubingwa kwani kazi haikuwa rahisi huku akimwagia sifa kocha wao Nasridinne Nabi kuwa ni bonge la kocha mwenye mbinu kali zinazoleta matokeo mazuri.

"Ligi ilikuwa ngumu kwani kila timu ilijiandaa na ilitamani kuwa mabingwa kama sisi lakini ndio hivyo sisi ndio tumeibuka mabingwa kwa sababu tulikuwa bora sana msimu huu na yote ni kutokana na kufuata maelekezo ya benchi letu la ufundi chini ya kocha mkuu Nabi ambaye ni bonge la kocha mwenye mbinu nzuri zinazotupa matokeo, " alisema Kibwana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: