Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matano ya kuitengeneza Yanga ya Gamondi

Yanga Gamondi As Mambo matano ya kuitengeneza Yanga ya Gamondi

Thu, 31 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kouassi Yao (26) ni jina linalotajwa na kuzungumzwa sana kwa sasa. Ni beki wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga aliyesajiliwa kutoka ASEC Mimosas kwenye dirisha hili la usajili linalotarajiwa kufungwa Agosti 31.

Yao ametua Yanga kuziba pengo la Djuma Shaban aliyeachwa baada ya kuomba kuondoka kwenda kujaribu changamoto sehemu nyingine.

Kwa Yao, Yanga imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, pia kuna maingizo mapya kama Nickson Kibabage (Singida Fountain Gate), Jonas Mkude (huru), Maxi Nzengeli (AS Maniema Union), Gift Fred (SC Villa), Mahlatsi Makudubela (Marumo Gallants), Pacome Zouzoua (ASEC) na Hafiz Konkoni. Yao anatajwa sana kutokana na ubora wake aliouonyesha kwenye mechi za timu hiyo alizocheza.

Hata hivyo, Kocha wa kikosi hicho kinachopambana kufika kufanya makubwa zaidi msimu huu, Miguel Gamondi, ana kazi ya kufanya hasa kwenye kutengeneza safu bora ya ushambuliaji kama ilivyokuwa msimu uliopita iliyoongozwa na Fiston Mayele.

Misimu miwili ya mafanikio Yanga, haikuwa kazi ndogo chini ya Kocha Nasreddine Nabi na Wanayanga wote wanatembea vifua mbele wakitamba ubora wa kikosi chao na mataji huku ikifanikiwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ili kubaki kwenye ubora ule wa misimu miwili iliyopita na zaidi, kuna mambo matano Kocha Gamondi anapaswa kutembea nayo na kuifanya Yanga izidi kutamba.

SAFU YA USHAMBULIAJI

Msimu uliopita safu ya ushambuliaji ilikuwa hatari na bora zaidi chini ya Mayele aliyeimbwa sana na aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa mabao 17 sambamba na Saido Ntibazonkiza wa Simba.

Msimu huu hayupo na amewaacha Kennedy Musonda na Clement Mzize na ameongezwa Hafiz Kankoni kwenye eneo hilo ambaye amefunga mabao mawili hadi sasa dhidi ya KMC kwenye Ligi Kuu Bara na moja dhidi ya Asas FC ya Djibout kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, mashabiki bado hawajaielewa safu yao ya ushambuliaji licha ya nyota hao kuwa na mchango kwenye mechi walizocheza hadi sasa na kocha Gamondi amesisitiza ni mapema sana kuzungumzia safu ya ushambuliaji kwa sababu anaamini wachezaji hao wana uwezo na watafanya mambo makubwa hivyo kazi imebaki kwake. Hapo akazie tu kuifanya iwe bora.

UBORA WA AZIZI KI

Chini ya Kocha Nabi, Yanga ilikuwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Stephan Aziz Ki waliocheza namba 10 na wote walipata nafasi ya kucheza.

Msimu huu Feitoto hayupo na Kocha Gamondi anamtumia zaidi Aziz Ki na Zouzoua Pacome na wakati mwingine Maxi Nzengeli kwenye kupandisha mashambulizi.

Vyovyote atakavyomtumia Aziz Ki, amekuwa na mchango mkubwa msimu huu na amefunga na kuchangia mabao msimu huu katika mechi sita za timu hiyo hadi sasa kabla ya mchezo wa jana dhidi ya JKT Tanzania.

Ubora wa Ki unamsumbua kichwa Gamondi wa nani aanze kati yake Maxi na Pacome ingawa amekuwa akiwatumia wote kwani na amekuwa akifanya mzunguko kwenye kuchagua wachezaji na wote kufanya vyema. Ni namna tu atakavyowatumia.

KUTETEA TAJI

Huu ni mtihani mkubwa kwake kwa sasa. Baada ya kutema taji moja la Ngao ya Jamii, Yanga sasa imebakisha mataji mawili makubwa nchini, Ligi Kuu Bara na Azam Sports Federation Cup (ASFC) na Gamondi anatakiwa kuhakikisha makombe hayo mawili yanasalia Jangwani.

Nabi alishinda makombe yote matatu kwenye misimu miwili mfululizo akiiongoza Yanga na sasa chini ya Gamondi kikosi kilichotwaa mataji kina mabadiliko machache hivyo wakishirikiana na wale waliopo, ni kazi kwa Gamondi kutengeneza muunganiko wa kuhakikisha wanatetea mataji hayo mawili na hilo limeanza kuonekana baada ya michezo yote sita aliyoisimamia Yanga hadi sasa kuruhusu bao moja tu kwenye ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Asas ya Djiout.

Wachezaji waliosepa na walikuwa kikosi cha kwanza ni Mayele, Yanick Bangala, Fei Toto, Shaban Djuma, Tuisila Kisinda, Bernard Morrison.

MFUMO

Nabi alishawahi kulithibitishia gazeti hili mfumo wa 4-3-3 ndio besti kwake na ulimpa matokeo mazuri hasa kwenye mashindano ya kimataifa alikoweka rekodi kwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia alikuwa muumini wa mfumo wa 4-2-31 na 3-5-2 mifumo ambayo imempa nafasi ya kufanya vizuri ndani ya misimu miwili aliyokuwa na Yanga kabla ya kutimkia AS FAR Rabat.

Hivyo Kocha Gamondi anayeiongoza Yanga msimu huu, ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wachezaji wake wanatambua mfumo anaoutumia na ili kumpa matokeo, ingawa kikosi chake kimekuwa kikishambulia kwa kasi na kupata idadi kubwa ya mabao.

KUONDOA UFALME

Msimu uliopita chini ya Nabi, Mayele alijitengenezea ufalme ndani ya kikosi hicho kutokana na uwezo wake wa kutupia mabao na asipoonekana timu ilikuwa ikipambana kupata matokeo.

Pamoja na yeye muda mwingine kukosa mabao akiwa ndani ya timu lakini uwepo wake ulikuwa unatoa nafasi ya mchezaji mwingine kufunga na yeye akihusika kutoa pasi au kufunga au kuchangia bao kwa namna yoyote.

Chini ya Gamondi ameonekana kuwa na utaratibu wa tofauti akitaka kila mchezaji kuwa na nafasi ya kutoa mchango kwenye timu na amebadilisha aina ya uchezaji timu inakaba pamoja na kushambulia pamoja.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: