Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Macho kwa Maxi, Musonda

Maxi Avic Town Macho kwa Maxi, Musonda

Sun, 20 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga leo kitashuka uwanjani Azam Complex kwa ajili ya mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asas ya Djibouti huku macho na masikio ya mashabiki wa klabu hiyo wakielekeza kwa Maxi Nzengeli na Kennedy Musonda watakaokuwa na jukumu la kutupia mabao.

Yanga itakuwa mgeni wa Asas iliyoamua kutumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi za nyumbani za kimataifa. Yanga imetoka kupoteza Ngao ya Jamii mbele ya watani wao, Simba na mchezo wa leo utapigwa kuanzia saa 11:00 jioni.

Msimu uliopita Yanga ilianzia hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini na kushinda kwa mabao 9-0, huku aliyekuwa straika wa timu hiyo, Fiston Mayele akipiga hat- trick mbili zilizomfanya amalize mechi za awali akiwa na mabao saba.

Yanga ilipopenya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuing’oa Club Africain ya Tunisia, Mayele aling’ara kwa kufunga mabao saba na kumaliza kinara wa michuano hiyo msimu huo, na timu hiyo kufika fainali na kulikosa taji kwa faida ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria waliotoka nao sare ya 2-2.

Kutokana na matokeo ya msimu uliopita ni wazi Musonda, Maxi na wachezaji wengine wa eneo la ushambuliaji watakuwa na kazi ya kufukia mashimo yaliyoachwa na Mayele kuhakikisha kesho wanatoka na ushindi mnono.

Matumaini makubwa kwa Yanga yapo kwa nyota hao ambao ndio wamekuwa wakizungumzwa kwa namna tofauti tofauti.

Maxi amekuwa kipenzi cha wana Yanga kwa sasa kutokana na aina ya uchezaji huku Musonda akionekana kushindwa kuonyesha makeke kama mashabiki wa timu hiyo walivyotarajia baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kinara wa upachikaji wa mabao, Mayele.

Msimu uliopita kimataifa, Musonda alihusika kwenye mabao sita akifunga matatu na kuasisti matatu, hivyo kesho nyota hao na wengine wanatakiwa kufanya mambo mbele ya Asas inayotumikiwa na beki wa zamani wa Vital’O ya Burundi na Simba, Gilbert Kazze.

Asas ndio timu iliyofunga mabao mengi kwenye ligi ya Djibouti msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya pili ikizidiwa pointi mbili na bingwa, Garde Republic kwani ilitupia kambani mabao 40 na yenyewe kufungwa mabao 13.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: