Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwanini Msuva Simba?

Msuva Bn Kwanini Msuva Simba?

Fri, 23 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mshambuliaji Simon Msuva ameziingiza vitani klabu tatu kubwa Simba,Yanga, Azam kuwania saini yake baada ya kumaliza mkataba na timu ya Al Qadisiyah FC ya Saudi Arabia na sasa vigogo hao watauana.

Msuva aliyekuja nchini kujiunga kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars iliyocheza mechi ya kuwania tiketi ya fainali za Afrika (Afcon) 2023, alinukuliwa katika mahojiano juzi, akisema anaweza kucheza tena hapa, japo ana ofa nyingi nje, ila ushawishi wa fedha unaweza kumpeleka kokote kukinukisha.

Kwa hapa nchini bado Msuva ataangukia kwa vigogo hao watatu na pengine Singida Fountain Gate zilizo na msuli wa kuweza kubadili akili ya mshambuliaji huyo kwa nguvu ya fedha lakini kokote atakapotua anaweza kuwa staa mkubwa kutokana na vikosi vya timu zote.

KWA NINI SIMBA

Simba kama itaingia vitani kumshawishi Msuva inaweza ikalamba dume kutokana na ubora wa mshambuliaji huyo anayeshikilia nafasi ya tatu kwa mabao ndani ya Stars akiwa na 21, nyuma ya Mrisho Ngassa anayeongoza kwa kufunga 25 na nahodha Mbwana Samatta mwenye 22, kwani anamudu kutumika kama winga au mshambuliaji wa kati.

Msuva ambaye awali aliwika akiwa na Yanga ana kasi ambayo inahitajika kwa falsafa za kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' ambaye kwa sasa mabosi wa Wekundu hao wako sokoni kusaka mtu mwenye ubora wa kucheza winga au mshambuliaji wa kati.

Msuli pekee ambao Simba itatakiwa kujipanga nao ni kumtengea fedha za kutosha mshambuliaji huyo ambazo zitamfanya abadili mawazo ya kurudi majuu.

Kocha Robertinho, atakapopelekewa jina la Msuva mezani hataweza kutumia zaidi ya nusu saa kulipitisha katika usajili wake mpya ndani ya kikosi hicho kutokana na ubora ambao amewahi kuuonyesha huko nyuma.

Jana Robertinho aliliambia Mwanaspoti kwamba hana uhakika kama winga huyo anaweza kurejea nchini, lakini endapo atapatikana utakuwa ni usajili bora kwa timu hiyo inayosaka kurejesha heshima baada ya kushindwa kutwaa taji lolote kwa misimu miwili mfululizo mbele ya Yanga.

"Unadhani anaweza kurejea Tanzania kwa sasa? Kama amesema anaweza kurudi nchini na viongozi wakampata nadhani utakuwa ni usajili mkubwa, hakuna kocha atayekataa kufanya kazi na mshambuliaji wa aina yake," alisema Robertinho ambaye yuko kwao Brazil kwa mapumziko.

KWA YANGA NAKO

Ikiwa chini ya kocha aliyetimka Nasreddine Nabi, Yanga msimu uliopita ilipambana kuinasa saini ya Msuva ambaye alikuwa mchezaji wao wa mwisho hapa nchini kabla ya kwenda Difaa el Jadida.

Tajiri wa Yanga, Ghalib Said Mohamed 'GSM', dirisha la usajili lililopita alimwekea dau kubwa la kufuru Msuva akimtaka akubali kurejea klabuni hapo kwa kumfanya mchezaji anayelipwa vizuri kabla ya kukimbilia Ligi ya Saudia.

Msuva ambaye ameifungia Al Qadisiyah FC mabao 8 msimu uliomalizika akiibuka mfungaji bora wa timu yake, hawezi kukosa nafasi ya kuanza katika kikosi cha Yanga wakati huu pia klabu yao ikisaka mshambuliaji mwenye kasi.

Yanga wanapambana kutafuta saini ya Makabi Lilepo na kazi kubwa inaonekana kwenye mshahara wake lakini endapo mabosi wao watapiga hesabu ndefu za kumgeukia Msuva ambaye anatajwa kuwa shabiki wao kwa kumwekea dau kubwa la usajili na mshahara mzuri wanaweza kuinasa saini yake na kuachana na Lilepo.

Kama Yanga ikimpata Msuva ambaye alikuwa mfungaji bora misimu miwili tofauti ya 2014-2015 na 2016/2017 kwa kufunga mabao 17 na 14 mtawalia, itakuwa na uhakika wa kuwa na staa kwenye timu hiyo kwa kuwa hatatakiwa kupewa muda wa kuizoea Ligi Kuu kwani ni mazingira ambayo ameshayaishi.

Wakati anaondoka Msuva alikuwa akuitumika kama winga na alionekana kuziba vyema pengo la Ngassa aliyekuwa ametimkia Afrika Kusini na tangu alipoondoka kwenda Morocco kukipiga Difaa El Jadida na baadae Wydad Casablanca kabla ya kuingia nao mgogoro na kwenda Saudia hajapatikana wa kuziba mashimo yake licha ya kuletwa mastaa kadhaa kama Tuisila Kisinda na Jesus Morocco.

HATA AZAM FC WAMO

Kama hufahamu Msuva amewahi kupikwa pale Azam Complex, Chamazi na matajiri wa timu hiyo kabla ya kutimka kuichezea Moro United na baadaye kutua Yanga 2012, lakini hesabu zao pia hazitakosea kutua kwa mshambuliaji huyo.

Azam bado haina mtu wa uhakika kwenye safu yao ya ushambuliaji wakiwategemea Prince Dube na Mkongomani Idris Mbombo pekee ambao bado wamekuwa hawana uwezo wa muendelezo.

Msuva hana mtu ambaye atamnyima namba ya kuanza katika kikosi cha kwanza ndani ya Azam FC kutokana na ubora wake na kasi aliyonayo, huyu akisaidiana na Feisal Salum 'Fei Toto' wanaweza kuifikisha Azam hatua ya makundi ya Kombe la Shrikisho Afrika.

Ikumbukwe kwa sasa Azam imekuwa ikiacha wachezaji kadhaa ikiwa na mikakati ya kuijenga timu mpya, hivyo ingizo la Msuva linaweza kuibeba kwa kumtumia eneo lote la mbele, kutokana na nyota huyo anatumika kama winga wa pande zote mbili na eneo la mshambuliaji wa kati na pia wa pili.

SINGIDA FG

Singida Big Stars ambayo kwa sasa imebadili jina la kuwa Singida Fountain Gate nayo ina nafasi ya kumsajili Msuva, kutokana na uwezo wake kiuchumi, lakini mipango ya timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa, huku ikiwa na wachezaji wachache wenye uwezo kama wake.

Deus Kaseke aliyejaribu kuvaa viatu vya Msuva ndani ya Yanga, hajaonyesha makali kikosini, sawa na ilivyo kwa Francis Kazady na Bright Adjei walioongezwa dirisha dogo, hivyo ujio wa nyota huyo wa kimataifa utaisaidia timu hiyo kufanya makubwa iwapo itaamua kumvalia njuga na kumsajili.

Bahati nzuri ni kwamba kocha Hans Pluijm amewahi kumnoa Msuva na kumfanya awe mkali hadi anaondoka kwenda Morocco, hivyo kutua kwake kutamrahisishia kazi akishirikiana na wakali wengine watakaosajiliwa kikosini hapo kwa msimu ujao.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: