Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwanini Bangala aondoke Yanga

Bangala 58309 Yannick Bangala

Fri, 23 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nyota wa Yanga Yannick Bangala amezua taharuki baada ya kuhojiwa na chombo kimoja cha habari na kusema ana asilimia 80 za kuondoka Yanga na 20 za kubaki.

Kuna sababu nyingi nyuma ya kauli hiyo, lakini moja ya maswali makubwa ambayo wadau wanajiuliza, anasemaje hivyo ilihali bado ana mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo?

Gazeti hili kupitia vyanzo mbalimbali ndani ya Yanga na kwa upande wa Bangala limeelezwa ni kweli beki huyo aliomba kuondoka, sambamba na Djuma Shabani na Joyce Lomalisa, lakini hadi sasa maombi hayo hayajawasaidia kwani wote wamebakiza mwaka mmoja.

Jibu ambalo uongozi wa Yanga uliwapa wachezaji hao ni kuwataka wapeleke ofa mezani za timu zinazohitaji kununua mikataba yao ili ziwasajili kisha watazipitia na baadaye kutoa jibu la mwisho.

Moja ya chanzo chetu ndani ya Yanga kilieleza kuwa Bangala na Djuma wanaidai Yanga fedha za usajili za mwaka mmoja (msimu ujao), kwani waliposaini mkataba mpya wa miaka miwili, walipewa fedha ya mwaka mmoja, huku wa pili wakikubaliana kulipwa baada ya mwaka mmoja kumalizika (sasa).

Sababu nyingine zilizopo nyuma ya Bangala na Lomalisa inaelezwa nyota hao wanahitajika na Azam FC, hivyo wanasukuma kuondoka Yanga ili kwenda kula maisha Chamazi, jambo ambalo halijawa rasmi na huenda lisitokee kwani Azam FC haijatuma ofa kwa Yanga.

Bangala pia alikuwa kwenye rada za Simba, lakini ni kama dili hilo limekufa kutokana na Wekundu wa Msimbazi kuchungulia mkataba wa Bangala na Yanga ikiwemo vipengele vya kumnunua na kuona watahitajika kutoa fedha nyingi kumpata.

Sababu nyingine iliyoelezwa kwa Bangala, Djuma na Lomalisa kuomba kuondoka Yanga ni baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Nasreddine Nabi anayetajwa kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afika Kusini.

Inaaminika kuwa baada ya kuondoka kwa Nabi huenda wakakosa utawala kama waliokuwa nao kipindi chake na kocha mpya anaweza kuja na mapendekezo, mbinu na mifumo yake, ambayo huenda wakakosa nafasi ya kung'ara.

Lakini chanzo kingine kilieleza kuwa uhusiano wa wachezaji hao na Rais wa Yanga, Hersi Saidi, hauko sawa na hilo ndilo limesukuma nyota hao wa zamani wa AS Vita ya DR Congo kuomba kuondoka.

Pamoja na yote hayo, juzi, raia hao wa DR Congo waliondoka nchini kwenda kwao kukiwa hakuna mwafaka kati yao na Yanga na huenda kila kitu kikamalizwa na wawakilishi wao ambao baadhi wapo Tanzania. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hery Morris alisema siku zote mchezaji huwa anaangalia maisha yake kuliko timu, hivyo inawezekana kuna ofa zimeenda kwao.

"Kwa klabu ya Yanga ni changamoto kama ikitokea wataondoka kwa sababu wengi wao walikuwa wanaanza kwenye kikosi cha kwanza hivyo kunaweza kukatokea pengo," alisema Morris.

Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Bakari Kigodeko alisema hadi wachezaji hao wanazungumza maana yake kuna jambo lipo ndani ya Yanga ndiyo maana wanataka kuondoka.

"Nadhani viongozi wa Yanga inabidi wakae chini na kuangalia mikataba ya wachezaji hao, sio rahisi wachezaji wanaotoka nchi moja watake kuondoka kwa pamoja lazima kutakuwa na kitu cha tofauti.

"Wote hao ni muhimu na walikuwa kwenye kikosi cha kwanza sasa wanapotaka kuondoka kuna shida, wachezaji wa kigeni huwa wapo makini kwenye maisha kuliko kama timu na wanatusaidia kuonyesha umuhimu wa kusoma mikataba," alisema Kigodeko.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: