Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa staili hii bado tano zipo Yanga

YANGA NZENGELI.jpeg Kwa staili hii bado tano zipo Yanga

Fri, 1 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Siku zote mchezo wa mpira wa miguu huamuliwa na walimu wa timu zinazocheza siku husika na hili ndilo lililoonekana juzi Jumanne, ambapo Yanga ikiwa mwenyeji iliwachapa JKT Tanzania mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Chamazi. Kwa staili ile Yanga waliyocheza wakiendelea nayo bado tano zipo.

JKT : 4 : 5 : 1

JKT iliingia kwa tahadhari kubwa ikijua kama ingeifunguka kungeigharimu kwa sehemu kubwa, hivyo Kocha Malale Hamsini aliamua kucheza kwa kutumia mfumo ambao uliwasaidia kuzuia zaidi.

Hapa Kocha Malale aliwatumia wachezaji watano Hassan Maulid, Sixtus Sabilo, Maka Edward, Hassan Dilunga na Najimu Magulu ili kuhakikisha Yanga haitengenezi nafasi nyingi kupitia katikati ya uwanja na katika kufanya hivyo kulikuwa na aina mbili za uzuiaji.

KUKABIA JUU: Ndani ya dakika 20 za mwanzo JKT ilihakikisha Yanga inapoanza mchezo kutoka kwa Djigui Diarra mpira hauwafikii wachezaji wengine, hivyo kazi ilikuwa kwa Sabilo, Edward Songo na Dilunga kuanza kukaba mapema.

KUKABIA CHINI: Baada ya mpango kazi uliposhindwa kufanya kazi wachezaji wa JKT walirudi chini na kumuacha Songo peke yakejuu huku wengine wote wakirudi hadi eneo la mita kama 25 kutoka golini ili kuziba kabisa mianya kwa wachezaji wa Yanga kufunga kirahisi.

Ndio sababu iliyozifanya timu zote mbili kutokupata mabao mapema hadi dakika za mwishoni kabisa za kipindi cha kwanza ambapo pigo la faulo la Stephan Aziz KI lilianza kutofautisha matokeo ya mchezo huo.

YANGA INABADILIKA VIPI

Pamoja na mchezo huo kuwa bora, mgumu na kutotabiriki hasa kutokana na kila nafasi iliyokuwa zikipatikana kuzibwa na timu zote mbili hasa JKT lakini bado wachezaji wa Yanga walikuwa wanabadilika kila muda ulivyokuwa ukisogea.

KIMFUMO: Ukianza kuangalia jinsi mpangilio wa wachezaji ndani ya uwanja pale mpira ulipoanza Yanga iliingia na mfumo wa 4 : 2 : 3 : 1 lakini kadiri muda ulivyokwenda na jinsi wapinzani JKT walivyoamua kurudi nyuma wengi Yanga ilibadilika na kutumia 4 : 1 : 4 : 1

Hapo unaweza kumuona Khalid Aucho akiwa mbele ya wachezaji wa idara ya ulinzi wakati Mudathir Yahya ambaye alikuwa chini alisogea juu kwenye mstari mmoja na kina Aziz KI , Keneth Musonda na Max Nzengeli huku kule mbele akibaki Hafiz Konkoni.

KUBADILISHANA NAFASI

Inakuwa kazi sana kujua kati ya Aziz KI na Max nani aliyecheza nafasi ya mshambuliaji wa pili nyuma ya Konkoni. Hawa ni wachezaji wanaocheza kwa nguvu kubwa wakishuka chini kuchukua mipira kwa viungo na kupanda na mipira mbele kushambulia, hii ndiyo silaha iliyowachanganya wachezaji wa JKT na kushindwa kukaa kwenye mkakati na mbinu walioanza nazo.

YANGA WALIFANIKIWA WAPI

Ukiangalia ni kwa nini Yanga ilipata mabao manne kipindi cha pili tofauti na moja kipindi cha kwanza.

UHURU: Kuna uhuru wanakuwa nao wachezaji muhimu wawili kama nilivyowataja hapo juu Aziz KI na Max ambao umekuwa chachu ya ushindi mkubwa kwenye mchezo huo na hata ile iliyopita.

KUTEMBEA NA MIPIRA-Wachezaji hao waliongoza kutembea na mipira Max mara 18 na Aziz KI mara 23.

KUTOKUWA NA WINGA

Uliiona Yanga ikicheza bila winga hasilia kitu ambacho kiliufanya upande wa kulia na kushoto kuwa wazi au kuwa na matobo na kuacha mianya kwa mabeki wa pembeni Nickson Kibabage na Yao Attohoula kupanda kila mara kusaidia mashambulizi na kufunga ndio maana Kibabage alitoa usaidizi wa bao la pili la Kennedy Musonda na Yao akifunga na kutoa usaidizi bao la tano.

JKT ILIKOSEA WAPI

Unaona wazi jinsi wachezaji wa JKT walivyoanza kwa kukaba katika eneo la juu kisha kushuka chini kukabia kwenye eneo lao, hivyo mategemeo makubwa ya Kocha Malale Hamsini kutowatumia wachezaji wenye kasi mbele kama Aziz Kada na Dany Lyanga ambao wangetumika kwenye mashambulizi ya kushtukiza, lakini kuendelea kumtumia Songo muda wote ilikuwa makosa.

Pia, JKT ilikuwa na utulivu ilipokuwa inaanzisha mpira kisha ilisogea taratibu kwenda mbele lakini ilishindwa kupenya hadi eneo la mwisho.

WALIOFANYA MAKUBWA

Edson Katanga: alikuwa muhimili mkubwa sana kwa JKT huku akipiga pasi ndefu na fupi mara 125.

Hassan Nassoro Machezo: Alihangaika sana mwanzoni kuwakaba wachezaji wengi wa kati ambao walikuwa wanamzunguka na kumsumbua kitu kilichomfanya kutumia viatu kutuliza vurugu za katikati.

Yao Attohoula: Kasi, usahihi, mikimbio mingi kusaidia kufunga na kufunga bao jana huku akipoteza pasi moja tu kati ya pasi 72 alizopiga.

Max: Pumzi aliyonayo si mchezo, yupo kila eneo la uwanja na uthibitisho ni bao lake la 5 aliloanzisha pasi ndefu kwa Yao kisha kufika kwa wakati kufunga.

Khalid Aucho: Mmoja kati ya viungo waliokuwa wakikimbia na kupiga pasi nyingi sana uwanjani, 171 huku akihusika kutengeneza faulo aliyofanyiwa Aziz KI na kufunga bao.

Mudathir Yahya: Pumzi aliyonayo, utulivu mkubwa na kufika kwenye maeneo mengi kwa wakati na kufanya maamuzi sahihi.

IPI SIRI YA GAMONDI

Kuna kitu anakifanya Kocha Miguel Gamondi ndani ya uwanja wa mazoezi mimi kwa jicho la ufundi nakiona lakini tumsubiri atengeze timu kama anavyosema.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: