Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Yanga hii, haikuwa rahisi!

Yanga Tizi Geita Kikosi cha Yanga

Mon, 10 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Achana na matokeo ya kuandika historia ya kuvuka makundi ikiwa kinara na kwenda robo fainali.

Sahau pia matokeo iliyopata kwenye mchezo wa jana wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Geita Gold uliopigwa usiku.

Ukweli ni kwamba Yanga kwa sasa ipo kwenye kiwango cha juu cha mafanikio msimu huu ikiwa inajiandaa kuvaana na Rivers United ya Nigeria kwenye mechi za robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipenya makundi kutoka Kundi D.

Kama haitoshi timu hiyo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikinyemelea taji la pili mfululizo la ubingwa huo, ikiwa ndio vinara wa kubeba mataji mengi kwa sasa ikiwa na 28 na ikibeba la msimu huu litakuwa na 29. Nane zaidi na iliyonayo Simba ambao ndio wapinzani na watani wao wa jadi.

Kwenye michuano ya ASFC wao ndio watetezi wakilitwaa msimu uliopita kwa kuifunga Coastal Union kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 na hii yote haikuja kirahisi imetokana na kazi kubwa iliyofanywa na mabosi wa klabu hiyo.

Utajiuliza jeuri hii inatoka wapi? Jibu ni moja tu kwanza ni ubora wa kikosi chao ambacho baada ya usajili wa misimu mitatu wamekuwa na kikosi bora kilichorudisha heshima yao.

Kando na kikosi hicho, kuna ufadhili na jeuri kubwa ya fedha wakiishi kitajiri chini ya GSM ambao ndio wanaotoa fedha katika kumsajili kila staa wa timu hiyo lakini kuna kichwa kimoja kilichosimamia sajili zote hizo za jeuri akianza kwa kudharaulika mpaka sasa amekuwa mafia kwa kufanikisha kuunda kikosi imara ambaye ni Injinia Hersi Said.

Hapa chini ni sajili 26 zilizofanywa na mabosi wa Yanga chini ya Injinia Hersi akipigwa tafu na bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ aliyeitoka Yanga kwenye maisha ya kutembeza bakuli mara alipojiondoa klabu kwa aliyekuwa mfadhili mkuu na bilionea wa zamani, Yusuf Manji.

MAKIPA WATATU WAKALI Hersi alifanikisha usajili wa makipa watatu wa kibabe kuanzia Djigui Diarra raia wa Mali ambaye ni kipa namba moja na wasaidizi wake wa nguvu Aboutwalib Mshery ambaye kwa sasa ni majeruhi na Metacha Mnata ambao wote kwa sasa ni makipa wa timu za taifa.

Makipa hao kwa vipindi tofauti wamekuwa wakibadilishana kwenye mechi za timu hiyo na kuwasahaulisha kabisa mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa na presha enzi za makipa kama Younde Rostand, Faruk Shikhalo na Klaus Kindoki waliokuwa wakifungwa mabao ya kushangaza uwanjani.

MABEKI waNANE WA MAANA Rais huyo wa Yanga alifanikisha sajili zingine nane za mabeki tofauti kuanzia mabeki wa pembeni kulia, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, kushoto Lomalisa Mutambala, mabeki wa kati Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, nahodha Bakar Mwamnyeto, Dickson Job, ambao hawa wote wamekuwa katika kiwango bora wakipishana vizuri katika kikosi chao cha kwanza na kucheza kwa mafanikio huku wengine kama David Bryson na Mamadou Doumbia wakiwa bado wanasubiri nafasi ya kuingia kikosi cha kwanza.

Mabeki hawa wameipa mafanikio makubwa Yanga katika misimu hii miwili wakiifanya kuwa timu ambayo haifungiki kirahisi wakimaliza bila kupoteza mchezo msimu uliopita huku pia wakiwa mabingwa lakini mpaka sasa msimu huu wakipoteza mchezo mmoja huku pia wakiendelea kuwa timu iliyoruhusu mabao machache wakiruhusu mabao 11 kwenye mechi 24.

VIUNGO WANANE MATATA Katikati pia Hersi alifanikisha sajili za viungo wanane matata kuanzia Mukoko Tonombe, Carlor Carmo ‘Carlinhos’ ambao baadaye waliuzwa pia wamo Yannick Bangala ambaye alikuwa mchezaji bora wa ligi msimu uliopita ukiwa ni msimu wake wa kwanza, yumo Mganda Khalid Aucho, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya.

Wengine wamo viungo washambuliaji wa pembeni Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, Farid Mussa wakipishana katika kikosi hicho, huku wengine Bernard Morrison, Denis Nkane wakiwemo lakini wakiwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi ingawa sasa wameanza mazoezi.

MASTRAIKA WATATU Pale kwenye safu ya ushambuliaji Hersi kama kuna zawadi kubwa aliyowapa wananchi na hata nchi na haitasahau basi ni kumshusha mshambuliaji Mkongomani Fiston Mayele ambaye licha ya kuja kama mchezaji asiyekuwa na jina kubwa lakini alifanikiwa kuwa staa mkubwa wa ligi akimaliza mfungaji wa pili kwa mabao 16 msimu uliopita na msimu huu akiendelea na moto huo wa akiongoza kwa ufungaji akipachika mabao 15.

Mayele sasa ameleta pacha wake Kennedy Musonda raia wa Zambia Hersi akifanikisha usajili kutoka klabu ya Power Dynamo ya Zambia akiwazidi akili TP Mazembe waliokaribia kumchukua lakini jina lingine kubwa alilopambana kwa vita kumleta Yanga ni kiungo mshambuliaji Stephanie Aziz KI kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast. Takwimu za mabao yao na namna Yanga inavyotetemesha kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa ni uthibitisho tosha mabosi Yanga waliamua.

MAKOCHA WAZITO Hakuishia hapo, Injinia Hersi na wenzake walishusha makocha wenye viwango na wanaoibeba Yanga, akianza na kocha mkubwa aliyewarudishia heshima kubwa Mtunisia Nasreddine Nabi akisaidiwa na Mrundi Cedric Kaze, huku Milton Nienov raia wa Brazil akija kama kocha wa makipa akitua Jangwani baada ya kutemwa na Simba na kuwaboresha vizuri makipa wa timu hiyo.

WATAALAM WENGINE Kwenye benchi hilo pia wamo watalaamu tofauti watatu akiwemo kocha wa mazoezi ya viungo Helmy Gueldich maarufu kama ‘Manywele’ kutokana mtindo wa nywele zake nyingi zilizotawanyika, kazi yake ikijitambulisha kutokana na kikosi hicho kuimarika uwanjani kwa kuwa fiti na kucheza kwa ubora muda wote uwanjani tofauti na awali kikionekana kukata upepo mwishoni, yumo daktari wa Viungo Youssef Ammar na Mtaalamu wa kuchambua mikanda ya video ya wapinzani Khalil Ben Youssef.

USAJILI MZIMA Mukoko, Kisinda, Bangala, Aucho, Kibwana, Job, Diarra, Mshery, Metacha, Mayele, Musonda, Moloko, Mudathir, Djuma, Lomalisa, Bacca, Mwamnyeto, Aziz KI, Sure Boy, Metacha, Nabi, Kaze, Milton, Helmy, Khalili, Youssef.

MSIKIE HERSI Akizungumzia hatua hiyo Hersi alisema shabaha kubwa ya mafanikio hayo ya Yanga kuwa na kikosi bora ilikuwa ni kuirudisha klabu hiyo kongwe kuwa na kikosi bora kitakachoweza kushindana uwanjani.

Hersi alisema katika kufanikisha safari hiyo kila mchezaji alikuwa na mchakato mgumu wa kumpata ambao ulihitaji umakini na wepesi wa haraka katika kumalizana nao huku akiwashukuru wafadhili wao GSM kwa kujitolea nguvu yao ya fedha kufanikisha muundo wa kikosi chao.

“Malengo yalianza kwa shabaha yetu kubwa ni kuirudisha Yanga ubora wake kwa kuwa na kikosi imara kitakachoweza kushindana uwanjani na kupata matokeo bora, hili halikufanyika kwa usiku mmoja tulifanikisha hili kwa hatua mbalimbali mpaka sasa tuko hapa,” alisema Hersi ambaye tangu ameingia Yanga ameiongoza timu hiyo kuchukua mataji ya ngao za jamii mbili, ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Shirikisho na ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.

“Tulikuwa na dhamira kubwa ya kuwa na timu bora kama hii na bado tunataka kikubwa zaidi ya hiki, kwa sasa sote tunaona Yanga inajipigania yenyewe uwanjani kwa ubora lakini niseme huwezi kuwa na timu ya namna hii kisha ukakwepa kutambua nguvu ya wafadhili wetu GSM.

“Unaweza kuwa na hesabu za kumpata mchezaji lakini utahitaji nguvu ya fedha kumfikia kwa haraka, ukishampata utahitaji kumtunza kwa maisha yake ya kila siku, hii ndio hatua ngumu ambayo inatulazimu kutambua nguvu ya wenzetu hawa na faida yake sasa tunaona wadhamini mbalimbali wanakuja sasa na hata klabu inapata mafanikio.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: