Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Fainali hii, Yanga washiwe wao tu

YANGA MASHABIKI ER.jpeg Mashabiki wa Yanga

Sun, 28 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kabla klabu 20 za Ligi Kuu England (EPL) hazijashuka uwanjani jioni ya leo ili kuhitimisha msimu wa ligi hiyo, jijini Dar es Salaam mashabiki wa soka watakuwa wameshajua matokeo ya pambano la kwanza la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na USM Alger ya Algeria.

Ligi ya England inahitimishwa kuanzia saa 12:30 jioni kwa timu 20 wakiwamo mabingwa Manchester City kushuka uwanjani kukamilisha ratiba na kujua timu zitakazoungana na Southampton kushuka daraja, ila wakati huo mashabiki wa soka nchini watakuwa njiani kurudi makwao wakiwa wana furaha au huzuni kutegemeana na matokeo ya pambano hilo la fainali litakalopigwa Kwa Mkapa.

Hii ni fainali ya 20 kwa michuano hiyo tangu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuamua kuliunganisha Kombe la CAF na lile la Washindi Afrika na kuwa Kombe la Shirikisho Afrika, michuano iliyoanza rasmi mwaka 2004.

Pia ni pambano la tisa linalozikutanisha timu za Afrika Kaskazini a.k.a Waarabu dhidi ya kanda nyingine, lakini ni mtego ambao Yanga inapaswa kuutegua, kwani katika mechi nane zilizopita zilizokutanisha timu za Kiarabu na kanda nyingine Wabantu halisia wameishia kunyanyaswa mara sita na mbili tu ndizo walizofanya kweli.

Stade Malien ya Mali na TP Mazembe ndizo pekee zilizojitutumua na kuwapiga Waarabu walipokutana kwenye fainali ya michuano hii tangu 2004, hivyo kama Yanga itafanya kweli kwa kupaa ushindi jioni ya leo kisha kwenda kushinda ugenini itakuwa ni ya tatu. Mtego huo!

Yanga itaikaribisha USM Alger kuanzia saa 10:00 jioni, huku zote zikiwa zinafukuzia taji la kwanza la CAF kwani licha ya Waalgeria kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2015 iliishia kunyukwa na TP Mazembe hivyo ni nafasi nyingine ya kujiuliza mbele ya Yanga inayocheza fainali ya kwanza ya CAF.

Ni pambano lisilotabirika, lakini lenye kurejea mechi mbili za makundi za michuano hiyo hiyo msimu wa 2018 zilikutana na USM kushinda nyumbani kwa mabao 4-0 kabla ya Yanga kulipa kisasi ikiwa pia nyumbani kwa kuwanyuka wapinzani wao mabao 2-1. Mwaka huo USM Alger ilitolewa robo fainali na ASl Masry ya Misri iliwafunga nje ndani kwa bao 1-0 na kung'olewa kwa jumla ya mabao 2-0.

Yanga imefika hatua hiyo kwa kuitoa Marumo Gallants ya Afrika kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye nusu fainali huku USM Alger ikiishinda ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0.

Rekodi zinaibeba Yanga nyumbani kwani katika mechi zote za CAF kwa msimu huu kuanzia zile za Ligi ya Mabingwa Afrika hadi hizi za Shirikisho haijapoteza zaidi ya kutoka sare tatu tofauti.

Katika mechi za raundi ya awali dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini Yanga ilishinda 5-0 ikiwa nyumbani kisha kutoka sare ya 1-1 na Al Hilal ya Sudan na kuangukia kwenye play-off ya Shirikisho.

Katika hatua hiyo mechi ya nyumbani ilitoka suluhu na Club Africain ya Tunisia kisha ikaenda kushinda ugenini na kutinga makundi na kwenye hatua hiyo hakuna mechi iliyopoteza au kutoka sare nyumbanji kabla ya kuingia robo fainali na kutoka suluhu na Rivers United ya Nigeria na kwenye nusu ilishinda 2-0 dhidi ya Marumo.

Pia rekodi kwa mechi za ugenini nazo sio mbaya kivile kwani imepoteza mechi mbili tu kuanzia Ligi ya Mabingwa hadi Shirikisho, ililala 1-0 raundi ya kwanza ya Mabingwa mbele ya Wasudan wa Al Hilal, lakini ikashinda dhidi ya Club Africain kwa bao 1-0 na kutinga makundi na mchezo wa kwanza wa hatua hiyo ililala 2-0 mbele ya US Monastir ya Tunisia kisha kutoka sare ya 1-1 na Real Bamako ya Mali kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya TP Mazembe, kisha kwenye robo na nusu ikashinda 2-0 dhidi ya Rivers United na Marumo.

Kwa upande wa USM Alger rekodi zinawabeba zaidi nyumbani, kwani kwenye mechi 14 za msimu huu za michuano ya CAF imeshinda saba zote nyumbani, lakini ikionekana ni dhaifu kwa michezo ya ugenini kwani katika mechi saba imeshinda mchezo mmoja tu uliokuwa wa raundi ya pili kisha kupoteza mmoja na kutoka sare mbili kwenye hatua ya makundi.

Katika robo fainali pia ilipoteza moja ugenini na kwenye nusu fainali ilitoka suluhu, kuonyesha wazi kwa rekodi hizo za USM Alger ikiwa ugeninui na ile ya Yanga ikiwa nyumbani ni wazi Vijana wa Jangwani kama watakomaa jioni ya leo wanaweza kurahisisha kazi kabla ya kwenda ugenini.

USM Alger kwa mechi saba za nyumbani imeruhusu mabao mawili tu na kufunga 16, wakati kwa ugenini imefunga sita na kufungwa saba, hivyo kuonyesha walivyo fiftefifte kwenye kujilinda na kufunga mabao, hivyo ni wajibu wa Yanga kujipanga ili kuweza kutoboa kwenye mchezo huo.

Kocha wa Yanga Nasreddine alisema kwamba anajua pambano hilo ni gumu kwa aina ya mpinzani wake alivyo, lakini alishakaa na kuzungumza na wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanafanya kila njia kupata matokeo mazuri nyumbani kisha kwenda kukomaa ugenini kama ilivyokuwa kwa mechi zilizopita.

Mashabiki wenye kiu ya kutaka kushuhudia fainali ya kwanza ya CAF jijini Dar es Salaam bila ya shaka watajitokeza kuipa nguvu Yanga kwenye pambano hilo kabla ya kuungana nao tena jijini Algers kwenye pambano la marudiano wakichagizwa na ndege iliyotolewa na Rais Samia Hassan Suluhu.

Hii ni bonge la fainali kwani inazikutanisha timu zenye rekodi zinazokaribia kufanana, lakini zikiwa zinahitaji kuweka heshima kwenye michuano hiyo ya CAF, mbali na kutaka kuonyesha ubabe mbele ya mwenzake baada ya mwaka 2018 kila mmoja kushinda nyumbani. Ngoja tuone itakuwaje!

Hapa chini ni rekodi ya fainali 19 zilizopita za michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu mwaka 2004 na matokeo yake, huku timu za Kiarabu zikitawala kwa kiasi kikubwa kubeba taji hilo, ikifanya hivyo mara 14 dhidi ya tano za timu za ukanda mwingine baranai Afrika.

2004

Hearts of Oak 2-2 Asante Kotoko (Heart of Oak inashinda kwa penalti 8-7)

2005

FAR Rabat 3-1 Dolphins FC

2006

Etoile Du Sahel 1-1 FAR Rabat (Bao la ugenini linaibeba Etoile Du Sahel)

2007

CS Sfaxien 5-2 Al Merrikh

2008

CS Sfaxien 2-2 Etoile Du Sahel (Sfaxien inashinda kwa bao la ugenini)

2009

Stade Malien 2-2 ES Setif (Stade Malien ikabeba kwa penalti 3-2)

2010

FUS Rabat 3-2 CS Sfaxien

2011

MAS Fez 1-1 Club Africain (MAS Fez inashinda kwa penalti 6-5)

2012

AC Leopards 4-3 Djoliba AC

2013

CS Sfaxien 3-2 TP Mazembe

2014

Al Ahly 2-2 Sewe Sport (Al Ahly inashinda kwa faida ya bao la ugenini)

2015

Etoile Du Sahel 2-1 Orlando Pirates

2016

TP Mazembe 5-2 MO Bejaia

2017

TP Mazembe 2-1 SuperSport United

2018

Raja Casablanca 4-3 AS Vita

2019

Zamalek 1-1 RS Berkane (Zamalek inashinda kwa penalti 5-3)

2020

RS Berkane 1-0 Pyramids

2021

Raja Casablanca 2-1 JS Kabylie

2022

RS Berkane 1-1 Orlando Pirates (RS Berkane imeshinda kwa penalti 5-4)

Mabingwa wa Jumla

3 CS Sfaxien (Tunisia)

2 Etoile Du Sahel (Tunisia)

RS Berklane (Morocco)

TP Mazembe (DR Congo)

Raja Casabalanca (Morocco)

1 FAR Rabat (Morocco)

Heart of Oak (Ghana)

Stade Malien (Mali)

FUS Rabat (Morocco)

MAS Fez (Morocco)

AC Leopard (Congo)

Al Ahly (Misri)

Zamalek (Misri)

4.7 Bilioni

Fedha inazobeba bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu huu

2.3 Bilioni

Fedha inazotwaa timu itakayopoteza kwenye fainali na kushika nafasi ya pili.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: