Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna jambo Yanga inapaswa kulifikiria

Gsm 0 Kuna jambo Yanga inapaswa kulifikiria

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika, Rais wa Yanga, Hersi Said aliposti picha akiwa ndani ya Uwanja wa TP Mazembe kisha akaandika "ALHAMDULILLAH! Leo ilikuwa KINZUMBI na JOSH….. Sorry……… KIVUMBI NA JASHO

Ni kama alikuwa akidokeza kwamba kuna jambo kubwa la usajili liko njiani linalomhusu nyota wa TP Mzembe, Phillippe Beni KINZUMBI, winga anayevaa jezi namba saba ya TP Mazembe. Kwenye mechi zote mbili dhidi ya Yanga, japo TP Mazembe ilipoteza, lakini Kinzumbi aling'ara sana na kuwavutia watu wengi.

Ilianza kwenye mchezo wa Dar es Salaam ambapo baada ya filimbi ya mwisho, Hersi alimfuata Kinzumbi na kuongea naye kwa takriban dakika tano na kisha kuongozana naye kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo. Kwa hiyo ujumbe ule wa kwenye mechi ya pili ukaleta hisia kwa mashabiki wa Yanga kwamba tayari winga huyo ameshamalizana na klabu yao.

Haikujulikana moja kwa moja kwamba JOSH aliyetajwa pale alikuwa yupi na ilikuwaje hadi akatajwa. Lakini kwenye uwanja wa maoni, wengi wakaitafsiri kama vita ya msimu ujao kati ya winga huyo na Joash Onyango wa Simba kwenye mechi za watani. Onyango ameshatimka zake Siomba na sasa yupo Singida Fountain Gate.

Hata hivyo, winga huwa hana vita kubwa na beki wa kati, zaidi ya beki wa pembeni. Hutokea mara chache wakakutana, lakini huwezi kuitabiri vita vya wachezaji wa nafasi hizo. Hiyo ikapita na kusahaulika. Msimu ukaisha na Joash Onyango hayupo tena Simba.

Pia stori za Kinzumbi hazipo tena. Hata hivyo, kuna stori za Yanga kumalizana Mkongomani kutoka AS Maniema ya huko huko DR Congo, Maxi Mpia Ngenzeli ambaye ni mchezaji bora wa ligi ya nchi hiyo msimu wa 2020/21. Hapo ndipo kwenye hofu ya Pumzi ya Moto kwamba Yanga inataka kuongeza mpasuko ndani ya klabu yao? Kivipi? Yanga tayari ina mpasuko kati ya wachezaji wa kikongo na viongozi. Djuma Shaaban, Yannick Bangala na Joyce Lomalisa wamepeleka barua kutaka kuvunja mikataba yao. Wachezaji hao wameuambia uongozi kwamba wanataka kwenda Azam FC.

Hili liliwarusha roho na kuona Azam FC inawahujumu, lakini nadhani wamegundua siyo kweli. Huku hilo likiendelea, Yanga wameshakata tamaa ya kumbakisha Fiston Mayele ambaye anatajwa kutaka kutimkia Uarabuni. Taarifa za ndani zinadai wachezaji wa Kikongomani kwa msimu mzima wamekuwa na malalamiko kwamba hawana furaha ndani ya Yanga, wakidaiwa kulalamika.

Wachezaji wa Kikongo wanasema hawapati heshima wanayostahili licha ya kuisaidia Yanga kupata mafanikio makubwa msimu uliopita hasa baada ya kuikuta ikiwa na hali mbaya. Kinachodaiwa malalamiko yamekuwa yakifukuta kwa ndani na yalianza kujidhihirisha baada ya mchezo wa kwanza wa

Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan. Kuelekea mchezo wa marudiano kule Sudan, wachezaji wengi raia wa DR Congo walidaiwa kusema wanaumwa. Ukatumika ushawishi mkubwa ili wacheze. Hata hivyo Yanga ikatolewa. Kwenye mchezo wa Lubumbashi dhidi ya TP Mazembe pia ilidaiwa kulikuwa na sintofahamu kwao lakini ilimalizwa kishujaa na viongozi.

Malalamiko yao mengine yalikuwa kwamba haiwezekani Clement Mzinze akacheza halafu Tuisila Kisinda akaanza nje. Walihisi mwezao hatendewi haki. Sasa kwenye kundi lenye shida hivi kuongeza Mkongomani mwingine ni kuongeza shida. Hapo ndipo kwenye hofu ya Pumzi ya Moto.

YANGA NA WAKONGOMANI

Baada ya mchezo ule wa Lubumbashi ukurasa huu uliandika historia ya Yanga na Wakongomani tangu zama za Mayaula Mayoni, lakini kuna upande wa pili ambao sio mzuri kwa Yanga.

Rejea mipasuko miwili mikubwa na ya kihistoria ya klabu hiyo - ule wa 1976 uliojificha kwenye Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliozaa Pan African na ule wa 1995 uliojificha kwenye Yanga Kampuni na Yanga Asili.

Mipasuko yote hii ilisababisha kundi kubwa la wachezaji nyota wa Yanga kufukuzwa na ilikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na raia wa DR Congo aliyeitwa Tambwe Leya.

Tambwe alikuwa kocha wa Yanga kuanzia 1974 akichukua nafasi ya Dk Victor Stanculescu wa Romania. Alikuja Tanzania kama kocha mwenye mafanikio makubwa kutokana na kuiongoza TP Mazembe kutwaa mara mbili mfululizo ubingwa wa Afrika 1967 na 1968.

MGOGORO WA 1975 Chini ya Tambwe, Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu), tena kwa kuivua Simba kwa kuifunga mabao 2-1 kwenye fainali iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana - Mwanza inayobaki kuwa mechi bora zaidi katika historia ya watani, kiasi cha kubatizwa jina la Nyamagana Thriller.

Lakini 1975 akaingia mgogoro na nyota mkubwa zaidi wa Yanga wakati huo, Sunday Manara na wachezaji wengine waandamizi kwenye timu waliokuwa upande wa Sunday.

Baada ya ubingwa wa 1974, Yanga ilitakiwa kushiriki Klabu Bingwa Afrika 1975 na ilipangwa kucheza na Enugu Rangers ya Nigeria iliyokuwa na kipa bora Afrika wakati huo, Patrick Okala. Katika kujiandaa Yanga ikaenda kuweka kambi nchini Kenya kwa mwaliko wa chama cha soka cha nchi hiyo.

Lakini Tambwe hakumuorodhesha Sunday kama sehemu ya kikosi kitakachokwenda Kenya. Tambwe alifanya hivyo kama adhabu kwa Sunday ambaye hakuhudhuria mazoezi kwa wiki moja bila ruhusa.

Awali Sunday aliomba ruhusa lakini akakataliwa, lakini akajipa mwenyewe na kukaa nyumbani wiki nzima. Aliporudi akashushwa chini kufanya mazoezi na timu ya vijana, na akakatwa kwenye safari. Mgogoro ndipo ulipoanzia. Presha ikaja kutoka kwa mashabiki na viongozi wa Yanga wakaingilia kati.

Meneja wa Yanga wakati huo, Shiraz Shariff akajitokeza na kusema Sunday atakwenda Kenya kwa amri ya viongozi. Na kweli akaenda. Kuingiliwa huko na viongozi kukazidi kuchochea utambi na mgogoro ukakua na kuleta makundi ndani ya timu yaliyogawa viongozi na hatimaye 1976 wachezaji na viongozi waliokuwa upande wa Sunday wakafukuzwa akiwemo Sunday mwenyewe.

MGOGORO WA 1995

Mgogoro wa Yanga wa 1975-76 uliitikisa nchi kiasi cha serikali kumfukuza Tambwe kwa kigezo cha kiusalama kwa sababu ya ugeni wake. Lakini mgeni hakuwa yeye tu, hata kocha wa Simba, Nabby Camara alikuwa mgeni aliyekuwa raia wa Guinea.

Ili kuweka sawa mizania na yeye akafukuzwa nchini kwa kigezo kilekile. Sababu za kiusalama. Mwaka 1994 Yanga wakamrudisha Tambwe wakati wakiwa na kocha mkuu kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany. Tambwe akashindwa kufanya kazi na Tauzany hivyo akashuka chini kuwa kocha wa timu ya vijana.

Ndipo alipotengeneza kikosi kilichoitwa Black Stars cha kina Silvanus Ibraham, Anwar Awadh na Maalumu Saleh 'Romario'. Kikosi hiki baadaye kikapandishwa na kuitwa Yanga Yossoa 1995. Lakini katika kipindi hicho ndipo ulipoibuka mgogoro mkubwa wa Yanga Kampuni na Yanga Asili.

Tambwe alikuwa upande wa Yanga Asili yaani wahafidhina wasiotaka mageuzi ndani ya klabu. Mgogoro huu ulisababisha mpasuko Yanga ulioendelea hadi miaka ya 2000 ulipomalizwa na Yusuf Manji. Tambwe alijihusisha na mgogoro wa 1975 ulioipasua Yanga katikati. Akajihusisha na mgogoro wa 1995 ulioipoteza Yanga kwa muongo mzima. Yanga iwaze kupunguza Wakongomani siyo kuongeza. Itanishukuru baadaye.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: