Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaizer Chiefs mtauweza mziki huu?

Yanga Mziki Wachezaji wa Yanga wakiwasili kwa Mkapa leo

Sat, 22 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa tano wa Kilele cha Wiki ya Mwananchi kwa klabu ya Yanga unafikia tamati leo wakati wanachama na mashabiki wa klabu hiyo watajumuika pamoja kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kupata burudani mbalimbali ya kuhitimishwa na pambano la kukata na shoka.

Tamasha hilo ambalo huchagizwa na wasanii mbalimbali ambao hujitokeza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki, pia hutumika kucheza mchezo wa kirafiki ambapo safari hii itacheza na timu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Yanga ilianzisha tamasha hilo ikifuata nyayo za watani wao, Simba waliokuwa wa kwanza kuanzisha Simba Day mwaka 2009, ikiwa ni miaka 10 kabla ya Wanajangwani nao kuzinduka na kuja na Wiki ya Mwananchi ambayo imekuwa ikitumika kutambulisha jezi na kikosi kipya.

Mwanaspoti linakuletea orodha na matokeo ya mechi zote nne za nyuma ambazo Yanga ilicheza tangu tamasha hilo kubwa na la kuvutia nchini lilipoasisiwa rasmi mwaka 2019 chini ya uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla kabla ya kumpisha Injinia Hersi Said.

YANGA 1-1 KARIOBANG SHARKS (2019)

Hili ndilo lilikuwa ni pambano la kwanza la 'Wiki ya Mwananchi' kwa Yanga ambapo ilicheza mchezo wa kirafiki na Kariobang Sharks ya Kenya.

Katika mchezo huu uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku wageni Kariobang ilipata bao la utangulizi dakika ya 49 kupitia kwa Patrick Otieno kisha dakika sita baadaye Patrick Sibomana aliyekuwa mpya kklabu hapo aliisawazishia Yanga kwa penalti.

Licha ya timu zote kuchakarika kusaka mabao mengine, lakini dakika 90 zilipolia kuashiria mchezo umemalizika Wananchi walitoka uwanjani kinyonge kwa sare hiyo.

YANGA 2-0 AIGLE NOIR (2020)

Yanga ikionekana ya moto sana ilicheza mechi yake ya pili kwenye kilele hicho dhidi ya klabu ya Aigle Noir kutoka nchini Burundi.

Mabao kwenye mchezo huo yalifungwa na Mghana, Michael Sarpong aliyeifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 59 kwa kichwa kikali kutokana na krosi iliyopigwa na Ditram Nchimbi huku lile la pili likifungwa na winga Tuisila Kisinda 'TK Master'.

Ushindi huu uliamsha shangwe kwa mashabiki wa Yanga waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja huo chini ya kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic.

Hili ndilo pambano pekee ambalo Yanga ilipata ushindi kwenye Wiki ya Mwananchi, kwani mechi zilizofuata baadae ziliisha kwa aibu kwa kutibuliwa sherehe na wageni waliowaalika wenyewe.

YANGA 1-2 ZANACO (2021)

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir msimu wa 2019, msimu uliofuata Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Zanaco ya Zambia.

Mshambuliaji kutoka DR Congo, Heritier Makambo alianza kuifungia Yanga bao la utangulizi dakika ya 30 tu ya mchezo baada ya kuwapiga chenga za fedheha mabeki wa Zanaco kufuatia kupokea pasi safi ya aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' (sasa yupo Azam FC).

Kufuatia bao hilo, Zanaco ilijibu mapigo ambapo winga wa kulia, Ackim Mumba alisawazisha dakika ya 60, kabla ya kiungo Kelvin Kapumbu kufunga la ushindi dakika ya 76 na kuzima kabisa shangwe za maelfu ya mashabiki wa Yanga waliofurika kwa Mkapa.

YANGA 0-2 VIPERS (2022)

Mchezo huu uliofanyika Agosti 6, mwaka jana Yanga ilifanya vibaya tena kwenye tamasha hili baada ya kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Vipers ya Uganda.

Katika mchezo huo ulioanza kwa kasi kwa timu zote, mabao ya Vipers yalifungwa na kiungo Milton Karisa dakika ya kwanza tu, huku lile la pili likifungwa na Anukani Bright dakika ya 64 mbele ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Vipers iliyokuwa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Uganda iliingia katika mchezo huo ikiwa na Kocha Mkuu Mbrazili, Roberto Oliveira 'Robertinho' ambaye baada ya kuipa mafanikio hayo aliondoka na kujiunga na Simba Januari 3, mwaka huu hadi sasa anaendelea kukinoa kikosi hicho.

SAFARI HII KAIZER CHIEFS

Kilele cha Wiki ya Mwananchi leo itahitimishwa na pambano la kukata na shoka kati ya wenyeji Yanga ambayo safari hii imeialika Kaizer Chiefs kutoka Afrika Kusini katika mchezo huu wa tano kwenye tamasha hili huku ikiwa na rekodi ya kushinda mechi moja tu kati ya hizo.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha mpya Muagentina, Miguel Gamondi aliyechukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyetua FAR Rabat ya Morocco ataiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu alipotambulishwa Juni 24 mwaka huu kwenye mkutano wa klabu hiyo.

Mashabiki wa Yanga wana kiu ya kuona wachezaji wao wapya waliosajiliwa kile watakachokifanya japo hofu imekuwa kubwa kutokana na baadhi ya mastaa walioipa mafanikio makubwa timu hiyo kuondoka kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.

Miongoni mwa mastaa hao ni mfungaji wao bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele aliyefunga mabao 17, huku akiibuka pia kidedea katika Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia kufunga mabao saba na kuchukua kiatu cha dhahabu.

Mastaa wapya waliosajiliwa msimu huu ambao mashabiki wana kiu kubwa ya kuwaona uwanjani kama kweli watawafikisha nchi ya ahadi ni Nickson Kibabage, Gift Fred, Maxi Mpia Nzegeli, Mahlatsi Makudubela 'Skudu' na Jonas Mkude aliyeichezea Simba miaka 13 na Kouassi Yao.

Je, sherehe zitaitashaje safari hii? Ni suala la kusubiri kuona mziki mpya wa Yanga utakavyowasha moto mbele ya AmaKhosi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: