Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jeshi la Simba litakavyokuwa

Crescentius Magori Crescentius Magori

Thu, 27 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba ipo kazini. Inataka kuhakikisha inamaliza usajili kabla ya Julai Mosi mwaka huu ili ipae kwendi nchini Misri kuweka kambi maalumu ya msimu mpya 'Pre Season' ikiwa na jeshi lake kamili kuanzia benchi la ufundi na mastaa wake wote.

Hadi sasa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara 22, wamekamilisha usajili wa wachezaji wasiopungua watatu, lakini pia imeendelea kuwapa 'Thank You' baadhi ya nyota waliokuwepo kikosini hapo kwa msimu uliopita sambamba na kuwaongezea mikataba mastaa wengine.

Unavyosoma hapa, vigogo wa Simba wanaohusika na usajili tayari wamepishana angani kupata saini za mastaa tofauti kwa ajili ya msimu ujao. Siku chache zilizopita Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori alikuwa Zambia kwenda kumalizana na winga, Joshua Mutale kutoka Power Dynamos ambaye nyota huyo tayari yupo Dar es Salaam kukamilisha mipango ya usajili ikiwemo kutambulishwa.

Pia kiungo Debora Fernandes Mavumbo kutoka Mutondo Stars naye dili lake na Simba lipo hatua za mwisho akiwa tayari amefika hapa nchini akifungiwa kwenye moja ya hoteli ya kifahari.

Lakini pia Simba ilimtambulisha beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union licha ya kwamba usajili wake huo unapigiwa kelele na klabu yake wakidai kulikuwa na ukiukwaji wa malipo ya fedha za uhamisho. Pia ipo mbioni kumtambulisha kiungo Omary Abdallah Omary kutoka Mashujaa ya mkoani Kigoma na Yusuf Kagoma kutokea Singida Fountain Gate.

Hapo wanafika wachezaji watano wapya ambao mambo yasipobadilika msimu ujao watakipiga Msimbazi. Mwingine ni mshambuliaji Steven Mukwala kutoka Uganda ambaye msimu uliopita alikuwa akikipiga Asante Kotoko na muda wowote kuanzia sasa atatua nchini kusaini mkataba kwani makubaliano ya kila kitu yamefikiwa kwa njia ya simu.

Wakati hayo yakiendelea, inafahamika kwamba Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah Muhene 'Try Again', yuko nchini DR Congo na inaelezwa ameenda kukamilisha dili za wachezaji wawili.

Kuna beki wa kati, Nathan Idumba Fasika aliyekiwasha kwenye klabu za Valerenga ya Norway, Cape Town City (Afrika Kusini) na FC Saint Eloi (DR Congo). Mwingine ni winga Elie Mpanzu kutoka AS Vita na kama atafanikiwa basi atarudi nao nchini kwa maandalizi ya mwisho kwenda Misri kuweka kambi.

Haijaishia hapo, Simba pia ipo kwenye mazungumzo mazuri na kiungo mkabaji Agustine Okejepha kutoka Rivers United ya Nigeria na huenda wakafikia muafaka wa kusaini mkataba.

Okejepha raia wa Nigeria, anatajwa kama mrithi sahihi wa Sadio Kanoute aliyemaliza mkataba Msimbazi huku ikielezwa hana mpango wa kusalia kikosini hapo sambamba na Babacar Sarr anayetajwa kuwepo kwenye mikakati ya kuvunjiwa mkataba ingawa bado pande zote mbili hazijafika muafaka.

Tayari Simba imeachana na Shaban Chilunda, John Bocco, Saidi Ntibazonkiza, Henock Inonga, Luis Miquissone na Kennedy Juma, huku wengine wengi wakitarajiwa kuagwa muda wowote.

WANNE UHAKIKA

Nyota wanne ambao mikataba yao ilikuwa ukingoni kumalizika ndani ya kikosi hicho, tayari wameongezewa hivyo wana uhakika wa kuendelea kuitumikia Simba kwa msimu ujao. Watatu kati ya hao wameshatambulishwa rasmi ambao ni Kibu Denis, Israel Mwenda na Mzamiru Yassin, huku Shomari Kapombe ambaye inaelezwa amepewa mwaka mmoja naye atatangazwa muda wowote.

BENCHI LA UFUNDI

Msimu uliopita Simba ilimaliza na Juma Mgunda ambaye alikuwa Kaimu Kocha Mkuu akichukua mikoba ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka mwezi Aprili siku chache baada ya kuchapwa 2-1 na Yanga. Mgunda alikuwa akisaidiana na Seleman Matola ambapo walipambana na timu hiyo ikashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Taarifa zilizopo hivi sasa ni kwamba, Mgunda mkataba wake na Simba umemalizika, lakini hata hivyo mipango iliyopo muda mrefu ni kusaka kocha mwingine ambaye ataiongoza timu hiyo msimu ujao watakapoenda kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na ile ya ndani ikiwemo Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na Ngao ya Jamii.

Kutokana na hilo, Simba wamepanga kabla ya kufika Ijumaa, wawe wamemtambulisha kocha wao mpya ambaye atakuja kuungana na jeshi lake hilo jijini Dar es Salaam kwani mikakati iliyopo ni kwamba kuanzia leo Alhamisi mastaa wataanza kuwasili kambini ili kesho Ijumaa wakutane na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Rais wa Heshima wa Klabu hiyo, Mohamed Dewji 'Mo' kwa ajili ya kuweka mikakati sawa kabla ya kwenda kuanza pre season.

Kocha anayepewa nafasi zaidi ni Msauzi, Steve Kompela ambaye taarifa zilizopo zinabainisha kuwa walifanya naye mawasiliano hapo awali. Wengine watakaoongezeka katika benchi la ufundi ni kocha wa viungo, kocha wa makipa na meneja wa timu ambaye anatajwa kurudishwa kundini Patrick Rweyemamu.

KIKOSI KITAKAVYOKUWA

Kama mambo hayatabadilika, basi Simba katika kikosi chao cha msimu ujao kitakuwa na maingizo mapya si chini ya nane ikiwa ni mchanganyiko wa wazawa na kimataifa ambao ni Nathan Fasika Idumba, Debora Fernandes Mavumbo, Agustine Okejepha, Joshua Mutale, Steven Mukwala, Elie Mpanzu, Lameck Lawi, Omary Abdallah Omary na Yusuf Kagoma.

Mziki wao utasomeka hivi; 1.Ayoub Lakred, 2.Israel Mwenda, 3.Mohamed Hussein 'Tshabalala', 4.Che Malone Fondoh, 5.Fasika Idumba, 6.Agustine Okejepha, 7.Joshua Mutale, 8.Debora Mavumbo, 9.Steven Mukwala, 10.Kibu Denis na 11.Eli Mpanzu. Watakaoingia ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Omary Abdallah Omary, Aubin Kramo, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma na Yusuf Kagoma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: