Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu ndo Aziz Ki mwamba wa Ouagadougou

Aziz Ki Yanga Hat Aziz Ki

Wed, 12 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara timu ya Yanga jana imeendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Kagera Sugar, mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Mabao ya Yanga yamefungwa na nyota wake, Stephane Aziz KI aliyefunga hat-trick dakika ya 43, 45 na 90, huku Fiston Mayele pia akifunga dakika ya 49.

Bao la nne limefungwa na Bernard Morrison dakika ya 84 likiwa ni la tatu kwake akiwa na kikosi hicho msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho alipoifunga Geita Gold Oktoba 29, mwaka jana.

ZIFUATAZO NI DONDOO MUHIMU ZA MCHEZO HUU

Mabao matatu ya Aziz KI aliyoyafunga nyota huyo yanamfanya kufikisha manane ya Ligi Kuu Bara hadi sasa huku mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni dhidi ya Namungo Februari 4, mwaka huu.

Hat-Trick ya Aziz KI ni ya saba msimu huu katika Ligi Kuu Bara huku akiwa ni mchezaji wa pili kwa Yanga kufunga baada ya Fiston Mayele dhidi ya Singida Big Stars Novemba 17, mwaka jana.

Fiston Mayele amefikisha mabao 16 ya Ligi Kuu Bara akiwa ameifikia rekodi aliyoiweka msimu uliopita nyuma ya aliyekuwa kinara na mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole anayekipiga FC Lupopo ya DR Congo aliyefunga 17.

Tangu mara ya mwisho Yanga ifungwe mabao 2-1 na Ihefu katika Ligi Kuu Bara Novemba 29, mwaka jana, huu ni ushindi wa 12, mfululizo na kati ya mechi hizo imefunga mabao 26 na kuruhusu matatu tu.

Mara ya mwisho kwa Kagera Sugar kuifunga Yanga ilikuwa ni ushindi wa 3-0, Januari 15 mwaka 2020, kwa mabao ya Yusuf Mhilu, Ally Ramadhan na Peter Mwalyanzi katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ndio ulikuwa ni wa kwanza kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Mbelgiji, Luc Eymael ambaye hata hivyo alidumu kwa miezi sita tu na kutimuliwa Julai 27, 2020 kwa kile kilichoelezwa kutoa matamshi ya kibaguzi.

Eymael aliyechukua nafasi ya Mwinyi Zahera alitoa kauli hizo ikiwa ni muda mchache tu tangu timu hiyo ikumbane na kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizi uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Novemba 13, mwaka jana Yanga ilishinda pia bao 1-0, lililofungwa na Clement Mzize.

Mchezo wa mwisho uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baina ya timu hizi, Februari 27, mwaka jana Yanga ilishinda mabao 3-0 yaliyofungwa na nyota wake, Fiston Mayele aliyefunga mawili na Saidi Ntibazonkiza 'Saido' ambaye anaichezea Klabu ya Simba kwa sasa.

Mchezo uliozalisha mabao mengi baina ya timu hizi pindi zilipokutana ni ule wa 6-2 uliopigwa Oktoba 22, mwaka 2016 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Donald Ngoma na Obrey Chirwa ambao kila mmoja wao alifunga mawili huku mengine yakifungwa na Simon Msuva na Deus Kaseke.

Kwa upande wa mabao yote ya Kagera Sugar yalifungwa na nyota wake, Mbaraka Yusuph na baada tu ya kipigo hicho uongozi wa Klabu hiyo uliwasimamisha, Hussein Shariff na Erick Kyaruzi kwa tuhuma za kuihujumu timu yao.

Huu ni mchezo wa 17 kwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime tangu achukue timu hiyo Oktoba 30, mwaka jana kutoka kwa Mkenya, Francis Baraza aliyetimuliwa Oktoba 28, mwaka jana kutokana na matokeo mabovu.

Katika michezo hiyo ameshinda sita, sare sita na kupoteza mitano tu ingawa kiujumla katika michezo 26 iliyocheza timu hiyo msimu huu imeshinda minane, sare minane na kupoteza 10 ikisalia nafasi ya nane na pointi zake 32.

Kwa upande wa Yanga huu ni mchezo wa 25 ambapo kati ya hiyo imeshinda 22, sare miwili na kupoteza mmoja tu ikiendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 68 nyuma ya Simba iliyoko ya pili na 60.

Baada ya mchezo huu Yanga itashuka tena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili hii ya Aprili 16 kucheza na watani zao wa jadi Simba huku mechi ya mwisho baina ya timu hizo ikiisha kwa sare ya bao 1-1, Oktoba 23, mwaka jana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: