Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Heshima imerejea Msimbazi

Simbasctanzania 36 Heshima imerejea Msimbazi

Mon, 14 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ngao imeenda bwana. Bado nini huko? Ndivyo mashabiki wa Simba walivyokuwa wakitamba kwa furaha baada ya kipa Ally Salim kugeuka shujaa akidaka penalti tatu na kuipa timu hiyo taji la kwanza msimu huu katika mechi ya Fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Simba ambayo kwa misimu miwili iliyopita ilikuwa haijapata taji lolote, jana iliiduwaza Yanga kwa kuifunga kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu, likiwa ni taji la 10 tangu mwaka 2001 michuano hiyo ilipoasisiwa.

Kipa Ally Salim ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kudaka penalti tatu za Yanga zilizopigwa na Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Kouassi Yao, ambao penalti zao zote walizipiga upande mmoja.

Hata penalti moja pekee ambayo Stephane Aziz KI alifunga pia aliipiga upande huo huo wa kulia kwa kipa Salim ambaye pia aliifuata lakini shuti lilikuwa kali mpira ukaingia wavuni.

Jean Baleke ndiye aliyemaliza mzizi wa lawama kwa kufunga mkwaju ulioirejeshea Simba heshima mbele ya mashabiki wa soka.

Mzamiru Yassin, Willy Onana pia walifunga penalti zao, huku Saido Ntibazonkiza mkwaju wake ulidakwa na Diarra Djigui na ile ya Moses Phiri ilipaa juu ya lango.

Tofauti na ilivyokuwa kabla ya pambano hilo kuanza kwa mashabiki wa Simba kuwa na presha kutojana na Ally Salim kusimama langoni, lakini baada ya penalti hizo mashabiki wao waliliimba jina la kipa huyo chipukizi.

Huo ulikuwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ dhidi ya Yanga tangu ajiunge na Simba akitokea Vipers ya Uganda.

Kocha huyo Mbrazili aliitungua Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita kwa mabao 2-0, na pia aliifunga kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi msimu uliopita wakati akiwa na Vipers.

Matokeo hayo yameifanya Simba kubebea taji la 10 la Ngao ya Jamii, tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2001 na kuiacha Yanga ikiwa na Ngao saba.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni, aliwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kwa kupoteza mchezo huo licha ya kuutawala kwa sehemu kubwa.

Gamondi alikiri pambano lilikuwa kali kwani wamecheza na timu ngumu, huku Robertinho aliwapogeza wachezaji, viongozi na kila Mwanasimba kwa kupata ushindi huo.

Robertinho alisema pambano lilikuwa gumu licha ya kukiri Yanga ilikuwa wazuri, lakini matokeo ya penalti yameendelea kuwapa raha mashabiki wanaoiunga mkono timu hiyo.

Kipa Ally Salim alimshukuru Mungu kwa kudaka penalti akisema ni maelekezo ya makocha naye aliyatimiza kwani tangu awali alishaelewa kuwa na utulivu.

“Kwenye penalti huwa sina wasiwasi, kwani anayepiga ana asilimia 75 na zilizobaki ni za kipa nami nimetimiza wajibu wangu,” alisema Salim.

MECHI ILIVYOKUWA

Katika pambano la jana lililochezeshwa vyema na mwamuzi Jonesia Rukya, timu zote zilianza mchezo kwa kazi kusaka mabao ya mapema, lakini umakini mdogo ulizikosesha timu zote mabao, huku Simba ikionekana kucheza faulo nyingi kulinganisha na Yanga iliyotawala dakika 45 za kwanza.

Mbali na timu kusaka mabao, lakini pia kulikuwa na vita ya aina yake baina ya nyota wa timu hizo zilizowafanya mashabiki waliohudhuria pambano hilo kupata burudani nyingine uwanjani hapo.

Kocha Roberto Oliveira wa Simba aliwaanzisha John Bocco, Kennedy Juma na Luis Miquissone badala ya kina Henock Inonga, Willy Onana na Kibu Denis, huku Yanga ikimuanzisha Clement Mzize sambamba na Kennedy Musonda eneo la mbele huku Maxi Nzengeli na Jesus Moloko wakiliamsha eneo la mbele la Yanga ambalo watajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi ndani ya dakika 90.

YAO v SAIDO, CHAMA

Kama kuna mchezaji aliituliza Simba kwenye mashambulizi basi ni beki wa kulia wa Yanga, Kouassi Yao, wepesi wake wa kurudi haraka kukaba na kutibua mashambulizi ya wekundu hao yaliibeba sana timu yake.

Yao aliwatuliza viungo wa Simba Clatous Chama, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ na Luis Miquissone ambao muda mwingi wa kipindi cha kwanza walikuwa wakipambana naye upande wake kwa kupishana.

MALONE NI BALAA

Mabeki wa kati wa Simba Che Malone Fondoh na Kennedy Juma ambaye alianza kuziba nafasi ya Henock Inonga aliye majeruhi walikuwa na kazi rahisi kumdhibiti mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzinze.

Mzinze nafasi kubwa ambayo ataijutia kwenye dakika 45 za kwanza ilikuwa dakika ya 40 alipopewa pasi na kiungo Maxi Nzengeli lakini akachelewa kidogo na pia alipobaki na kipa Salim ambaye aliutoa mpira na kuwa kona.

BAO LA MOLOKO

Mashabiki wa Yanga walionekana kulia na mwamuzi msaidizi wa kwanza Mohamed Mkono kutoka Tanga aliyelikataa bao la winga Jesus Moloko dakika ya 45 wakiona kama mchezaji wao alipofunga alikuwa hajaotea lakini mwamuzi huyo alimnasa vizuri Mkongomani huyo kabla ya kufunga kwa kichwa.

MKWAKWANI BADO

Mechi nne zote za mashindano ya kuwania Ngao ya Jamii zimeshindwa kuujaza Uwanja wa Mkwakwani kuanzia mchezo wa kwanza wa Azam na Singida Fountain Gate hadi ule wa Fainali uliopigwa usiku.

Kwenye fainali ya jana licha ya kuonekana ndio mchezo ambao ungeweza kuujaza uwanja huo lakini ilishindikana kwa majukwaa ya chini kwa eneo lote kuonekana bila watu, huku ikielezwa ni viwango vya viingilio, huku sehemu kubwa ya mashabiki wakiwa ni wale waliotoka nje ya mkoa huo hasa Dar.

Vikosi vilivyoanza;

YANGA: Diarra, Yao, Lomalisa/Kibabage, Bacca, Mwamnyeto, Aucho, Moloko/Aziz KI, Mudathir/Mkude Mzize/Hafiz, Maxi na Musonda/Pacome.

SIMBA: Salim, Kapombe/Phiri, Tshabalala, Kennedy, Malone, Kanoute/Ngoma, Chama/ Onana, Mzamiru, Bocco/Baleke, Saido na Luis/Kibu

AZAM  YAAMBULIA

Katika mechi ya mapema iliyopigwa saa 9 alasiri, Azam ilipoza machungu kwa kuifumua Singida Fountain Gate kwa mabao 2-0 katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu mabao yote yakifungwa kipindi cha kwanza.

Bao la kwanza lilifungwa na Prince Dube dakika ya kwanza ya mchezo huo kutokana na makosa ya ngome ya Singida wakati Joash Onyango aliyerudisha mpira kwa Beno Kakolanya na kipa huyo kushindwa kuumiliki na kulazimika kuukimbiza wakati ukisererekea langoni akauwahi na kutoa pasi fupi kwa beki wake ambayo ikaibwa katikati na Sospeter Bajana aliyempa asisti ya bao jepesi mfungaji huyo aliyeukwamisha wavuni.

Sopu aliifungia Azam bao la pili dakika ya 42 baada ya ngome ya Singida kujichanganya tena na nyota huyo wa kimataifa kukwamisha kwa shuti.

Katika pambano hilo Kakolanya aliyesajiliwa na Singida kutoka Simba na kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekuwa akikipiga Yanga walijikuta kwenye wakati mgumu kwa kuzomewa na mashabiki wa klabu hizo za Kariakoo waliokuwa wakisubiri fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa usiku.

Fei Toto alitolewa dakika ya 72 na nafasi yake kuchukuliwa na Yahya Zayd na hadi mwisho Azam ilitwaa nafasi ya tatu na kuiacha Singida ikicheza mechi mbili mfululizo za Ngao bila ya kufunga bao lolote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: