Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hapa Mkude, mbona kazi anayo

Mkude Yanga Ers Jonas Mkude.

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Bara na wanafainali wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu uliopita, Yanga imenasa saini ya aliyekuwa kiungo wa muda mrefu wa watani wake wa jadi Simba, Jonas Mkude lakini swali kubwa kwa wadau wa soka nchini ni 'atatoboa?'

Tayari Mkude amejiunga na kambi ya Yanga iliyopo Avic Kigamboni baada ya kukaa Msimbazi kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo na sasa kinachofanyika ni mazoezi kwa msimu mpya ambayo yatakuja na majibu kuwa atatoboa ama atafeli ndani ya jezi ya Yanga.

Kupitia makala haya, Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa viunzi vitano ambavyo vitatoa majibu kuhusu kutoboa au kutotoboa kwa Mkude kutokana na rekodi na historia yake.

USHINDANI WA NAMBA

Hapa ndipo sehemu ya kwanza ambapo mashabiki na wadau wa soka nchini wanasubiri kuona kama Mkude atatoboa ama atakwama.

Hakuna shaka Mkude ni miongoni mwa viongo wazawa walioonyesha ubora wao kwa muda mrefu tangu mwaka 2012 alipoanza kucheza Simba.

Licha ya kuwepo kwa kupanda na kushuka kwa ubora, kupata ushindani mpya lakini Mkude aliweza kucheza mara kwa mara na kufanya vizuri.

Msimu uliopita akiwa Simba hakuwa na muda wa kutosha kucheza kwenye kikosi cha kwanza na nafasi yake walicheza Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin na wakati mwingine Erasto Nyoni na hiyo ni moja ya sababu ya kuachwa baada ya mkataba wake kumalizika.

Pale Yanga anaenda kukutana na mafundi wengine wengi katika eneo lake ambao anahitaji kushimndana nao ili kupata muda wa kutosha kucheza.

Atakutana na ushindani wa Yanick Bangala, Kharid Aucho, Mudathir Yahya, Zawadi Mauya na Salumu Abubakar 'Sure Boy' je atatoboa?

Hiki ndio kiunzi ambacho Mkude anatakiwa akiruke kwa ufasaha ili kuongeza thamani, heshima na imani yake ndani ya Yanga.

NIDHAMU

Pili ni Nidhamu. Kwa mara kadhaa Mkude akiwa Simba na hata timu ya taifa ya Tanzania amekuwa akishutumiwa na kushitakiwa kwa makosa ya kinidhamu.

Hilo limefanya picha ya Mkude kwa baadhi ya watu kuonekana kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini mwenye shida linapokuja suala la nidhamu.

Sasa yupo Yanga na wadau na mashabiki wengi wanawaza juu ya nidhamu yake wakijiuliza maswali mbali mbali. Ni kweli hana nidhamu au walikuwa wakimsingizia? Basi Mkude ndiye ana jukumu la kujibu maswali hayo kutokana na atakavyokuwa akiishi Yanga, ndani na nje ya uwanja.

Hiki ni kiunzi kingine ambacho kinamkabili Mkude kuvuka ili kuendelea kula maisha na kuheshimiwa ndani ya Yanga.

HADHI

Mkude ni miongoni mwa wachezaji wazawa kwenye Ligi Kuu walio kwenye hadhi ya juu kabisa. Kuanzia ubora, heshima, maisha na hata utajiri. Mkude yuko vizuri.

Swali linakuja Mkude ataweza kulinda hadhi yake ndani ya Yanga?, Ataweza kuwa mvumilivu msikivu na mnyenyekevu kwa wadogo zake aliowakuta pale Yanga wakiwamo viongozi mfano nahodha Bakari Mwamnyeto?.

Ili kutoboa hapo, anatakiwa kubadilisha aina ya maisha yake aliyokuwa akiishi Simba (Uandamizi), na kuendana na matakwa ya Yanga kwani akiwa Simba aliheshimika kama mchezaji aliyedumu kikosini pale kwa muda mrefu, aliwahi kuwa nahodha, pia alikuwa kiongozi kwa wenzake maisha ambayo hatakutana nayo Yanga.

USHABIKI

Kiunzi kingine ambacho Mkude anatakiwa kuongeza umakini ili kukivuka ni hiki cha Ushabiki. Kwa uzoefu alionao Mkude kwenye Ligi Kuu, lazima anatambua tabia za mashabiki wa Simba na Yanga.

Baadhi yao wanapenda mazuri tu, kiufupi wanapenda kufurahi na sio vinginevyo. Wapo mashabiki wa Yanga wanaoamini Mkude ni shabiki wa watani zao Simba lakini pia wapo wanaoamini Mkude ni Mwananchi.

Anachotakiwa kufanya ili kuvuka hapa ni kuishi namna mashabiki wa Yanga wanataka, awafurahishe uwanjani na awafurahie na kuwapa ushirikiano nje ya uwanja na kama atafanya tofauti na hivyo basi huenda akawa na muda mchache wa kufurahia maisha ndani ya jezi za kijani, njano na nyeusi.

MKUDE

Kiunzi kingine na cha mwisho katika Makala haya ni Mkude mwenyewe, Wazungu wanasema 'Me vs Me' kwa maana ya mimi dhidi ya mimi.

Mkude anahitaji kujishindanisha na hali yake mwenyewe na kuhakikisha anashinda. Unaweza kusema kila kitu kuhusu Mkude lakini cha msingi ni yeye kushinda dhidi yake.

Katika maisha yake mapya ya Yanga mkude anatakiwa kubadili baadhi ya mambo ambayo ni tabia zake, mazoea yake na mtindo wa maisha yake.

Anatakiwa kupambana Mkude wa Yanga dhidi ya yule Mkude wa Simba ili kujipata zaidi, na kama atafanikiwa katika hilo basi ana nafasi kubwa ya kutoboa akiwa kwa Wakali hao wa Jangwani.

Jina: Jonas Mkude

Kuzaliwa: Des 3, 1992

Mahali: Dar es Salaam

Uraia: Tanzania

Nafasi: Kiungo Mkabaji

Klabu: Yanga

Jezi: Namba 20

Alikopita: Mwanza United, Simba U-20, Simba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: