Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hadi mshahara huu kaukataa, sasa itakuwaje?

Mayele 4 Chrome Fiston Mayele

Sun, 2 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabeki Yannick Bangala na Djuma Shaban wamemalizana na Yanga na kupunguza presha za mashabiki wa klabu hiyo walikuwa na hofu kwa nyota hao kutimka. Kilichowashangaza wakubwa wa klabu hiyo ni straika Fiston Mayele kugomea mshahara mpya licha ya kwamba ni mkubwa maradufu.

Bangala na Djuma walitaka kulipwa fedha zao za usajili la sivyo wangesepa zao na mabosi wa Yanga wakaona isiwe tabu na kuwalipa na sasa wachezaji hao watakuwepo kikosi hadi mwishoni mwa msimu ujao.

Wote wawili walisaini mkataba wa miaka miwili Jangwani huku kila mmoja akipatiwa fedha nusu za usajili huo yaani mwaka mmoja huku wa pili wakikubaliana kulipwa baada ya mwaka mmoja kumalizika (sasa).

ISHU YA MAYELE Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Mayele ameugomea mshahara wa zaidi ya Sh34 Milioni alizoahidiwa kulipwa ilimradi abakie klabu hapo.

Nyota huyo aliyemaliza msimu uliopita kama kinara wa mabao wa Kombe la Shirikisho Afrika akifunga saba na kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akifunga 17 sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba, imeelezwa anataka kuondoka baada ya kupata ofa zenye donge nono nje ya Tanzania.

Mayele mwenye mkataba wa mwaka mmoja na Yanga amegoma kusaini mkataba mpya ambao ungemfanya awe analipwa pesa ndefu kuliko mchezaji yeyote ndani ya timu hiyo huku akidaiwa amepagawa na ofa nono kutoka Esperance ya Tunisia, Zamalek na Pyramids za Misri.

Imethibitika kuwa Mayele na Yanga wamekaa vikao visivyopungua vitatu tangu kumalizika kwa ligi ili kuboresha mkataba wake, lakini hakuna mabadiliko yaliyokamilika hadi sasa kwa vile straika huyo kukomaa kutaka aachiwe aende kwenye klabu nyingine.

Yanga ilimpa Mayele ofa ya kumuongezea mshahara kutoka kiwango anacholipwa sasa cha Dola 9,000 (zaidi ya Sh 20 milioni) hadi kufikia dola 15,000 (zaidi ya Sh 34 Milioni) lakini staa huyo amechomoa, japo inaelezwa mazungumzo baina yao yanaendelea ili kupata muafaka.

Hata hivyo, taarifa zaidi zinalidokeza Mwanaspoti kwamba siku tatu zilizopita Mayele alienda kambi ya Yanga, iliyopo Avic Town, Kigamboni na kuchukua kila kitu chake jambo lililoongeza hofu kwa Yanga juu ya kumbakiza.

Hata hivyo katika moja ya mahojiano ya Rais wa Yanga, Hersi Said akizungumzia kuhusu Mayele alisema;

"Mayele ni mchezaji bora na ninafurahia kuona anahusishwa na timu nyingine, hii inaonyesha kuwa Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wakubwa. Kama atakuwa anataka kuondoka, tutaangalia vitu vitatu, moja tutataka kumbakiza, mbili tutaangalia bei nzuri, tatu ni nani atachukua nafasi yake."

Mayele jana alikuwa Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri akicheza mechi ya hisani iliyoandaliwa na wachezaji wenzake wa Yanga, Dickson Job na Shomari Kibwana kupitia mradi wao wa 'Wape Tabasamu' na baada ya hapo atarejea Dar es Salaam kuendelea na mazungumzo na Yanga.

Straika huyo alijiunga Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2021/2022 kwa Mkataba wa miaka miwili, na baadae kusaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja utakaotamatika 2024, hivyo timu yeyote itakayomtaka italazimika kununua mkataba huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: