Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fadlu: Simba hii bado kidogo tu

Fadlu Davids Simba Bado.jpeg Kocha Fadlu Davids

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu na alama sita baada ya juzi kuishushia kichapo cha mabao 4-0 Fountain Gate huku mastaa wapya kikosini hapo akiwemo Charles Ahoua wakionyesha kiwango bora lakini kocha mkuu wa Wanamaimbazi hao, Msauzi Fadlu Davies amesema bado hajapata kile anachokitaka kwa asilimia mia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu amesema licha ya timu yake kuonyesha kiwango bora lakini bado kuna vitu anaendelea kuvifanyia kazi mazoezini na vikiwa sawa basi Simba itakuwa tishio zaidi.

"Tumecheza vizuri na kushinda mechi. Nimefurahishwa na kiwango walichoonyesha wachezaji. Umekuwa ni muendelezo wa kile tunachokitaka. Tunataka Simba iwe imara zaidi hivyo bado kuna mambo tunapaswa kuyafanyia kazi zaidi kwenye uwanja wa mazoezi. Ni machache ya kiufundi ambayo kama yatakamilika basi timu itakuwa imara zaidi ya hapa," amesema Fadlu.

Kocha huyo amewapa mapumziko ya siku mbili wachezaji wake kabla ya kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya itakayopigwa Septemba 13, mwaka huu, ugenini.

"Tutapata mapumziko mafupi kisha tutarejea kambini kujipanga na mechi dhidi ya Tripoli. Akili zetu zote kwa sasa tumezielekeza huko.

"Tunajua tutaanzia ugenini na itakuwa mechi ngumu lakini tunaenda kutafuta mpango sahihi utakaotufanya kuwa na matokeo chanya ugenini kabla ya marudiano nyumbani," amesema

MASTAA GARI LIMEWAKA

Mastaa wapya wa Simba, Kiungo mshambuliaji Charles Ahoua na mastaika Steve Mukwala na Valentino amshaka gari lao limewaka na juzi walionyesha ubora wao Simba ikiichapa 4-0 Fountain.

Ahoua aliyekuwa MVP wa Ligi ya Ivory Coast msimu uliopita kwenye mechi ya juzi alihusika moja kwa moja katika mabao yote manne ya Simba akifunga moja na kutoa pasi za mwisho 'asisti' mbili na kumfanya kuongoza kwa Asisti hadi sasa kwenye ligi akiwa nazo tatu.

Kwa upande wa Mukwala baada ya kukosa mabao kwenye mechi zilizopita, juzi alifungua rasmi kitabu chake cha upachikaji mabao kwenye ligi kwa kuifungia Simba bao moja.

Staa mwingine mpya kikosini hapo ambaye gari limewaka ni straika Valentino Mashaka anayeongoza kwa mabao kwa sasa kwenye ligi akifunga bao moja moja kwenye mechi zote mbili Simba ilizocheza.

Katika mechi mbili za Simba ilizocheza kwenye ligi hadi sasa, imefunga jumla ya mabao saba, ikiwa haijaruhusu bao lolote huku wafungaji wakiwa Mashaka mwenye mabao mawili, Awesu Awesu, Ahoua, Mukwala, Edwin Balua na Che Malone Fondoh.

MSIKIE PAWASA

Beki wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa ni kocha, Boniphace Pawasa almesema mashabiki na wadau wa soka nchini wanapaswa kuwa wavumilivu na kuisapoti Simba kwani inajijenga upya.

"Ni mwanzo mzuri lakini hauwezi kusema moja kwa moja kuwa timu imekamilika. Simba imefanya usajili wa wachezaji wapya zaidi ya 10, inajijenga upya hivyo mashabiki wake waipunguzie presha bali waisapoti timu naamini kadri muda unavyoenda wataimalika na kuwa bora zaidi," amesema Pawasa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: