Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EXCLUSIVE: Nabi afichua siri nzito Yanga

Nabi Mds Kocha Nabi

Tue, 20 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Yanga bado hawaamini kama kocha Nasreddine Nabi ndo keshasepa ndani ya timu hiyo. Huenda hii inatokana na jinsi alivyowaheshimisha kwa miaka miwili na nusu ya utumishi wake Jangwani.

Kocha Nabi ameachana na Yanga akiwa ameweka alama na kuwaachia Wanayanga wakitambia rekodi tamu alizoweka ambazo hata watani zao wanazimezea mate. Chini ya Nabi, Yanga imeweka rekodi ya kucheza mechi 49 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza, kutwaa taji la Ligi Kuu bila kupoteza na kwa misimu miwili mfululizo amebeba mataji yote ya Bara, ikiwamo Ngao, Ligi na ASFC.

Kali zaidi ni kuifikisha Yanga katika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni rekodi kwani hakuna timu yoyote ya Tanzania na hata Afrika Mashariki iliyowahi kufika hatua hiyo tangu CAF ilipobadilisha na kutambulisha michuano hiyo mwaka 2004.

Kocha huyo hakuwahi kufanya mahojiano maalumu yoyote tangu atue nchini, lakini kutokana na uamuzi huo wa kujiondoa Yanga ambao uliwasononesha mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa na imani kubwa kwake, Mwanaspoti likamsaka na kufanya naye mahojiano maalum kujua mambo mbalimbali ya maisha ya miaka yake miwili ndani ya Yanga.

Katika mahojiano hayo tunayoanza nayo leo, Nabi amefichua siri ya namna Simba ilivyombeba na kutamba kwenye michuano ya ndani, pia ameanika ishu ya kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' pamoja na kumtaja Florent Ibenge namna alivyomsaidia kuifikisha Yanga fainali ya CAF, mara baada ya kocha huyo kumng'oa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Al Hilal ya Sudan. Endelea naye kupata utamu...!

ALIANZAJE YANGA

Kocha Nabi anaanza kwa kueleza safari yake ya miaka miwili na nusu ndani ya Yanga akisema ilikuwa safari yenye kuvutia hasa kuanzia mwaka wa kwanza kwa vipindi tofauti vya furaha na presha kubwa katika kazi yake.

"Kiukweli kwa ujumla ilikuwa miaka miwili ya nusu inayovutia pengine kuliko wakati wote wa muda wangu wa kuwa kocha wa soka, ukweli kuna muda nilikutana na nyakati ngumu kitu cha maajabu baada ya hizo nyakati ngumu kuliibuka mazuri ya kuvutia, ila kwa ujumla naweza kusema miaka miwili hii niliyokuwa hapa ilikuwa ya mafanikio."

KIPI KILIMBEBA KUHIMILI MAGUMU

"Kilichokuwa kinanisaidia kupita salama katika hizo nyakati ngumu ni kwamba mimi ni mtu wa kuheshimu misingi ya kazi yangu, siku zote nimekuwa mtu wa kukubaliana na changamoto na suluhisho sio kuzikimbia au kukata tamaa ni kukabiliana nazo kwa njia sahihi ya taaluma yangu, hizi nyakati ngumu hazikuwa zinasababishwa na mimi, zilikujka kutokana na mazingira ya kazi yangu yanapikuwa hayajakaa sawasawa.

"Nakumbuka mfano mzuri wa nyakati ngumu za kwanza kuzipitia ni pale tuliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu nifike Yanga, kila mtu anajua kwamba tulipata shida katika safari yetu ya maandalizi ya msimu kule Morocco tukapoteza muda badala ya kutumia muda vizuri kama ambavyo klabu na mimi tulipanga pia likaja suala la baadhi ya wachezaji kushindwa kuanza kuitumikia timu kwa wakati kama Djuma (Shaban), Meyele (Fiston) na Aucho (Khalid).

"Iliniumiza sana moyo wangu kwa kuwa zilikuwa ni shida zetu tukatolewa na Rivers (United), haikuwa rahisi hali ile kukubalika niliona kama kila mmoja ananiangalia mimi lakini nilituliza akili na kupanga mikakati ndani ya timu nikiwashirikisha viongozi na baadaye tulivuka salama eneo hilo.

SIMBA ILIVYOMUINUA

Baada ya Yanga kutolewa katika mchezo wa awali wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United wakipoteza kwa bao 1-0 kwa kila mchezo wa nyumbani na ugenini, presha ilikuwa kubwa kwa Nabi akiwa ndio anaanza mwaka wake wa kwanza ndani ya timu hiyo.

Hapa anaeleza baadaye matokeo ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ndio uliombeba na kumsaidia kuiongoza Yanga kibabe na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila kupoteza sambamba na kutwaa Kombe la Shirikisho (ASFC) ikimvua Mnyama walipokutana nao nusu fainali, Jijini Mwanza.

"Tuliporudi kutoka Nigeria kwanza nilijiandaa mwenyewe kwamba nakwenda kucheza mechi ya Ngao ya Jamii, lakini ni kama fainali kwangu, tulikaa na wasaidizi wangu na wachezaji kuweka mkakati wa kuicheza ile mechi, tulitengeneza programu ya mazoezi ambayo ndani ya siku chache yaliwaimarisha wachezaji ilikuwa kama wiki moja tu na siku kadhaa," anasema Nabi na kuongeza;

"Kitu kikubwa zaidi nilifarijika kuona wachezaji wakisema watakwenda kucheza mechi ile kwa lengo kubwa la kunipigania na kuwapigania mashabiki wao ambao waliwaangusha ili tusifungwe tena, walisema timu haikutolewa ligi ya mabingwa kwa ajili ya mapungufu yangu kama kocha ilitokana na sababu zingine zetu za ndani za maandalizi na ukumbuke ile mechi hata wale tuliokuwa tumewakosa kwenye zile mechi mbili waliweza kucheza.

"Wachezaji walicheza kwa nguvu sana ile mechi (dhidi ya Simba) walipambana sana niliona uhalisia wa kile ambacho waliniahidi wakati tukiwa kweye mazoezi, walijua kwamba kama tungepoteza ile mechi ningekuwa nimepoteza kazi kutokana na presha ambayo ilikuja baada ya mechi mbili dhidi ya Rivers lakini pia ingewavunja moyo mashabiki wao ambao waliamini timu yao ingeleta mafanikio makubwa kimataifa.

"Nawakumbuka wachezaji wawili Djuma na Diarra (Djigui) hawa hata baada ya kuongea wao wote kama timu kwamba wanakwenda kupambana lakini wao walinifuata tena na kunisisitiza juu ya hilo ilinifariji sana na kunipa nguvu.

UNBEATEN ILIVYOKUJA

Baada ya kushinda dhidi ya Simba kwa bao la Mayele Yanga haikupoteza tena mechi ya kimashindano mpaka wakachukua ubingwa na hata kombe la Azam shirikisho hapa anaeleza

"Ushindi dhidi ya Simba ulibadilisha hali ndani ya timu yetu, hali ya kujiamini kwa wachezaji na mashabiki ilirudi wka haraka na kutengeneza morali kubwa baina ya pande hizo mbili, tukasema kupitia ile hali tunatakiwa kuendeleza kasi ya kushinda zaidi mechi zetu huku mashabiki wetu nao wakitupa mzuka kwa kila mechi ambayo tulicheza, ilikuwa inavutia kuona wingi wa mashabiki huku wakiwa na imani kubwa na timu yao, tulichofanya tuliweka msisitiozo wa kushinda kila mechi lakini sio kwa kuwa wakali kiasi cha kutishia wachezaji.

"Hatukupanga kuwa tumalize ligi bila kufungwa hapana lakini tulijiwekea malengo kwamba kila mchezo tutacheza kama fainali bila kujali tunacheza na timu za juu ya msimamo wa ligi, katikati au zile za chini, tuliweka malengo makubwa ya ushindi kwa kila dakika 90 tulizocheza.

"Kikubwa kila mchezo tuliomaliza ulionyesha kuna maendeleo makubwa ya wachezaji kuwa fiti lakini pia kimbinu za uwanjani pia tuliimarika, hapa nimpongeze sana Helmy (Gueldich) kocha wa mazoezi ya viungo alifanya kazi kubwa sana, nakumbuka kulikuwa na kelele kwamba Yanga haina pumzi majibu yangu yalikuwa mafupi tu watu wasubiri na hizo kelele baadaye zilikwisha.

SOKA TAMU LILIANZIA HAPA

"Tulikuwa ni mikakati mizuri ya wachezaji gani wa kuja kwenye timu, tulitanguliza utulivu mkubwa nikishirikiana na uongozi ili kupata wachezaji ambao wataingia kwenye falsafa zangu, unapokuwa kocha unayejiamini hili ni rahisi kulisimamia, matunda yake kwwnye hili kila mtu wa Yanga alifurahia ubora wa timu ilipokuwa inacheza, niliahidi awali wakati nafika hapa kwamba nahitaji muda lakini lazima tupambane kuhakikisha timu inashinda na ndani ya ushindi mashabiki wafurahie soka la timu yao.

IBENGE ALIVYOIBADILI YANGA

Msimu uliomalizika Yanga ilirudi tena kwwnye Ligi ya Mabingwa wakiwatoa Zalan FC ya Sudan kibabe lakini wakakutana tena na mfupa mgumu Al Hilal ya Sudan inayonolewa na Florent Ibenge na kujikuta wakitolewa.

Nabi anasema baada ya matokeo hayo dhidi ya Al Hilal, ilimsaidia kurudi nyuma na kujipanga upya na kuiongoza Yanga kucheza mechi 16 za michuano ya Shirikisho, ikipoteza mara mbili pekee hadi ilipofika fainali na anafafanua mabadiliko waliyoyafanya.

"Kama mnakumbuka tulipocheza na Al Hilal ya Ibenge, tulitawala sana mchezo lakini haikutusaidia kupata ushindi kwenye mechi zote mbili, tulipotolewa tukasema tubadili mfumo wetu wa uchezaji, tukasema kwa mashindano haya ya Afrika tunatakiwa kuacha mambo ya kucheza pasi nyingi kama mwanzo tucheze soka la malengo zaidi kupata matokeo," anafichua Nabi na kuongeza;

"Tuligundua kwamba tunapocheza soka la pasi nyingi kuna nafasi kubwa ya wazi tunaitengeneza eneo letu la ulinzi ambalo kama mkicheza na wapinzani wanaojua kucheza kushambulia kwa kushtukiza wanaweza kuwafunga na hili ndilo walilokuwa wakilifanya Al Hilal. Niseme kwa ufupi tukajifunza na kubadilika na mabadiliko yale yalitusaidia hadi tunafika fainali ya Shirikisho, hatukuwa tukawa tumepoteza mechi hizo mbili pekee," amesema Nabi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: