Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama na rekodi zake CAF

Chama Hat Trick Chama na rekodi zake CAF

Mon, 20 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mabao matatu (hat-trick) aliyofunga kiungo wa Simba, Clatous Chama katika mechi dhidi ya Horoya AC ya Guinea juzi, yakimwezesha kufikisha manne na kukaa kileleni katika orodha ya vinara wa ufungaji kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Robertinho Oliveira, amesema haikuwa kazi rahisi kushinda 7-0.

Katika mchezo huo uliopigwa juzi Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi huo mnono shukrani kwa Chama aliyetupia hat-trick, Jean Baleke na Saido Kanoute, ambao kila moja alicheka na nyavu mara mbili.

Kwa mujibu wa takwimu za Ligi ya Mabingwa Afrika, Chama anaongoza akiwa pamoja na straika wa Al Hilal ya Sudan, Makabi Lilepo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambaye naye pia ana mabao manne.

Mzambia huyo wa Simba bao lingine alilifunga mechi iliyopita Machi 7, mwaka huu katika uwanja huo huo, Simba ikiichapa Vipers ya Uganda 1-0.

Wachezaji wanaofuatia ambao wamefunga mabao matatu ni Hamza Khabba wa Raja Casablanca ya Morocco, Mahmoud Kahraba wa Al Ahly ya Misri, Cassius Mailula na Peter Shalulile wote wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao kila mmoja ametupia mara tatu.

Wakati huo huo, mchezaji huyo juzi alizawadiwa mbuzi mmoja na shabiki wa timu hiyo aliyeweka ahadi baada ya kufunga bao kwenye mechi dhidi ya Vipers.

Akizungumza na gazeti hili jana, Robertinho alisema waliwaandaa wachezaji wao kucheza vizuri wakiwa hawana mpira kwa kuwa inapunguza kufanya makosa na kuwasoma wapinzani hivyo kuwa na uwezekano wa kutumia vizuri nafasi walizotengeneza.

Alisema malengo yao yalikuwa kucheza vizuri, kupunguza makosa na kupata ushindi kitu ambacho wamefanikiwa kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.

"Kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika si jambo jepesi na wala haitokei mara kwa mara, tuliwasisitiza wachezaji wetu kuhakikisha tunacheza vizuri tukiwa hatuna mpira.

"Nawapongeza wachezaji wangu kwa kuweza kufuata maelekezo tuliyowapa, nawashukuru pia mashabiki wetu kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu yao.

"Malengo yetu yalikuwa kuingia robo fainali na tunamshukuru Mungu tumefanikiwa hilo ndio jambo zuri la kujivunia,” alisema Robertinho.

Aliongeza kuwa kila mchezaji ndani ya kikosi amefanya majukumu yao mazuri, Kanoute, Chama, Baleke, Mohamed Hussein na Shomari Kapombe walifanya kile alichowaagiza katika uwanja wa mazoezi kwa kukitekeleza uwanjani.

Kocha Msaidizi wa Horoya AC, Sekou Soumah Diego, alisema wamepokea matokeo hayo ingawa hayakuwa mazuri kwao kutokana na kuzidiwa na Simba kila eneo.

Alisema katika soka kuna kushinda, kushindwa na kupoteza, na kwamba mipango yao ilikuwa kushinda mchezo huo na hilo halikutimia, hivyo wanarejea uwanjani kujiandaa na mchezo ujao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah 'Try Again', amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa motisha anaoutoa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kwa timu za Tanzania.

Try Again alisema kiasi cha Sh. milioni tano anazotoa Rais Samia kwa kila bao linalofungwa kimeongeza morali na kuwafanya wachezaji kujiona wana deni kubwa kwa nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: