Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Beki mpya Simba anaetembelea nyota ya Yondani

Kazi Beki mpya Simba anaetembelea nyota ya Yondani

Fri, 28 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye moja ya mahojiano aliyowahi kufanya na Gazeti la Mwanaspoti, beki mpya wa Simba, Hussein Bakari'Kazi' aliyekuwa anakipiga Geita Gold alisema bado ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha anatimiza malengo yake aliyojiwekea kwenye soka.

Kazi alisema mpira wa miguu bado haujamlipa na anatamani siku moja aje kuwa mwanasoka mkubwa na kutimiza ahadi yake ya kuwa mfanyabiashara. Beki huyo matamanio yake makubwa ni kujiona anacheza timu kubwa kama Simba au Yanga ambapo ndoto hiyo imekuwa kweli na rasmi ni mali ya Simba.

"Niseme tu ukweli bado soka halijanilipa na wala sijapata mafanikio ila ndoto yangu kubwa ni kuwa mwanasoka mkubwa ambaye ninatamani kusajiliwa na timu kubwa," aliwahi kusema Kazi.

Kazi alitambulishwa siku moja na mchezaji mwingine wa Simba Hamis Abdallah, alisema kurejea Simba ina maana kubwa sana kwake kwa sababu ni timu ambayo alianza nayo kutafuta mafanikio yake kwenye soka. "Nilianza kucheza Simba timu ya vijana kabla ya kwenda nje kupambana, nipo tayari kwa changamoto mpya," alisema beki huyo wa kati.

MTIHANI ALIONAO

Kama lilivyo jina lake la utani 'Kazi' atakuwa na mtihani mgumu wa kupigania namba mbele ya mabeki wazoefu kina Hennock Inonga, Kennedy Juma na Che Fondoh Malone.

Kennedy hakuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na nafasi hiyo kuchukuliwa na aliyekuwa mkongwe, Joash Onyango ambaye ametangazwa kujiunga na Singida FG.

Inonga ambaye kwa misimu miwili amefanya kazi kubwa katika eneo la ulinzi ambalo limeruhusu mabao 17 pekee ikiwa ni timu iliyofungwa mabao machache.

Kwasasa Kazi atakuwa na kibarua kikubwa kwakuwa bado hajacheza akiwa na Simba tofauti na Kennedy ambaye tayari alishacheza.

YONDANI NDIO KIOO CHAKE

Kazi anasema Ligi Kuu kwa sasa ina wachezaji wazuri lakini kutokana na ubora alionao beki mkongwe, Kelvin Yondani kwake ndiye bora zaidi na anapocheza naye anajifunza vitu vingi kutoka kwake.

Beki huyo ambaye aliwahi kuichezea Mbeya City anasema kitu anachojifunza kutoka kwa Yondani ni namna ya kujituma akiwa mazoezini na kuliheshimu soka.

Anasema anajifunza mengi kutoka kwa beki huyo ambaye amewahi kuzichezea klabu za Simba na Yanga na kufanikiwa pia kuichezea Timu ya Taifa ya Tanzania'Taifa Stars'kwa kuwa na ubora kama ule wa zamani.

Yondani huu unakuwa msimu wake wa 17 tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara na aliwahi kuwa Simba kwa misimu saba mfululizo, kuanzia mwaka 2006-2012.

"Namkubali sana Yondani na najifunza vitu vingi kutoka kwake kwa kuwa amekuwa muda mrefu kwenye soka ana uzoefu na ligi yetu nimekuwa na wakati mzuri sana wa kucheza naye," anasema Kazi.

Kazi anasema licha ya kucheza na Yondani na kutegemewa kutengeneza ukuta mzuri ndani ya Geita Gold mambo yalikuwa tofauti kwao kwani hadi iliposalia michezo miwili ligi kumalizika timu yao ilikuwa inaashika nafasi ya tatu kwa kufungwa mabao mengi (38).

HANA KADI NYEKUNDU

Anasema tangu aanze kucheza ligi ana jumla ya kadi nne za njano na hana hata kadi moja nyekundu.

Beki huyo anasema anajitahidi kila anapopata nafasi ya kucheza kuhakikisha anakuwa makini na makosa madogo ambayo yanaweza kuigharimu timu hiyo.

"Tangu nianze kucheza soka nakuwa makini sana ili mwamuzi asinipatie kadi ambazo hazina maana katika kazi yangu ambazo zinaweza kuigharimu timu."

KITU AMBACHO HATAKISAHAU

Anasema ukiachana na maisha ya soka hata wao wachezaji kuna wakati anapitia changamoto ambazo anajutia kucheza Soka.

Beki huyo anasema aliwahi kwenda DR Congo kwa ajili ya shughuli za michezo lakini alipata matatizo makubwa ambayo yalikaribia kumkatisha tamaa ya kuendelea na maisha ya soka.

Kazi anadai alipata misukosuko ambayo hakutarajia na ilimkatisha tamaa kwa kujiona hana bahati na anachokipigania.

"Kwenye safari zetu hizi za michezo nilikuwa na mimi na dereva tu ila sio vizuri kuyataja madhira yaliyonipata kwasababu naweza kukatisha tamaa watu wengine ila ukweli ni kwamba changamoto zipo tena nyingi."

MAHUSIANO

Wakati alipoulizwa suala la kuwa na uhusiano, Kazi alihema kidogo na kufunguka kwamba kutokana na vijana wa sasa kukosa uaminifu na wenza inasababisha watu kusalitiana.

Anadai alishawahi kuumizwa kwenye uhusiano na hilo halikumpa wasiwasi kwani alidili na kazi yake.

"Ukishakuwa kijana lazima tu utapitia changamoto kama hizo za uhusiano kuna muda lazima ufunike kombe ili vitu vingine vipite," anasema beki huyo aliyezaliwa jijini Dar es Salaam na kuongeza;

"Nilianza kucheza mpira nikiwa mdogo sana huwezi kuamini mimi mwenyewe sikumbuki lini ila baada ya watu kunisifia mtaani najua kucheza nikaenda Uwanja wa Karume na hapo ndipo nikaanza kung'ara sehemu mbalimbali akicheza soka la kulipwa Shelisheli katika Timu ya Forester FC kabla ya kujiunga na Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania na baadaye Geita Gold."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: