Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balaa la Yanga na jezi nyeuzi

Mayele Job Mn Balaa la Yanga na jezi nyeuzi

Sun, 19 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga inashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo Jumapili kuikaribisha TP Mazembe kutoka DR Congo katika mchezo wa pili hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga inahitaji ushindi ili kufufua matumaini baada ya mechi ya kwanza ya kundi 'D' kupoteza mabao 2-0 dhidi ya US Monastir ya Tunisia huku wapinzani wao TP Mazembe ikiwa na kumbukumbu ya kushinda 3-1 na Real Bamako ya Mali.

Wakati mchezo huo ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki na wadau wengi wa soka nchini, macho yameelekezwa kwenye jezi nyeusi ikayotumika na miamba hiyo ambayo imekuwa ikipata matokeo mazuri tangu imeanza kuivaa.

Imani katika jezi ipo katika timu nyingi Duniani. Aprili 13, 1996 Manchester United ya Ligi Kuu England ikiwa chini ya kocha wake, Alex Ferguson ikicheza dhidi ya Southampton mpaka kufikia mapumziko katika Uwanja wa The Dell (sasa Saint Maryís), ilishafungwa mabao 3-0 ila kipindi cha pili United ilibadilisha jezi za kijivu iliyokuwa imezivaa.

Ferguson akiwa mwenye hasira alidai wachezaji wake walikuwa hawawezi kuonana vizuri kwenye mwanga mkali wa jua kutokana na rangi ya jezi hizo.

United ilibadilisha jezi hizo na kuvaa za rangi ya bluu na nyeupe na hadi mwisho mchezo uliisha kwa miamba hiyo kupoteza mabao 3-1.

Hilo pia limetokea kwa upande wa Yanga ambao nao wameonekana kuwa na jambo lake katika jezi za rangi nyeusi inayopenda kuitumia na kuivaa sana kwa sasa katika mechi zake nyingi hivyo kusababisha kuibua mijadala mingi.

Jezi hiyo ina mzuka wa aina yake na haijawahi kuiangusha pindi inapocheza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara au CAF.

Ni kama ina bahati flani hivi kwa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu tangu ilipoivaa mwaka jana na kumtoa Mwarabu wa Tunisia, Club Africain ugenini kwa jumla ya bao 1-0 na kufuzu makundi Kombe la Shirikisho Afrika mara ya tatu ikifanya hivyo mwaka 2016, 2018.

Rasmi Yanga ilianza kuivaa jezi rangi nyeusi Oktoba 26, dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo wake nyota, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Ikiwa katika hali ngumu baada ya kutoka sare tasa nyumbani dhidi ya Club Africain katika mchezo wa pili wa mtoano kufuzu makundi, Novemba 9, Yanga ilitinga uzi huo nchini Tunisia na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na nyota wake, Stephan Aziz Ki katika Uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic ambao zamani ulikuwa ukiitwa 7 Novembre.

Yanga ambayo imejitambulisha zaidi kwa kuvaa jezi zenye rangi ya asili za kijani na njano baada ya kuitoa Club Africain imeonekana kunogewa zaidi na uzi huo mweusi kwani Novemba 13, iliuvaa tena na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kirumba, Mwanza ikiwa ni siku chache tu tangu iwasili nchini ikitokea Tunisia.

Kama haitoshi Novemba 17, mwaka jana, Yanga ilishusha kipigo kitakatifu dhidi ya Singida Big Stars (SBS) ikiwa ndani ya uzi mweusi.

Straika Fiston Mayele aliondoka na mpira katika mchezo huo baada ya kufunga mabao matatu 'Hat-Trick huku bao lingine likifungwa na beki wake, Kibwana Shomary likiwa ndio la kwanza kwake tangu ameanza kucheza mpira.

Mara baada ya mchezo huo wa Ligi Kuu kumalizika Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe aliposti picha ya kikosi cha timu hiyo kikiwa kimevaa uzi mweusi kwenye mitandao ya kijamii na kuandika maneno yaliyosomeka ‘Rais naomba hizi jezi nyeusi tusizivae tena tutakuja kuua watu." huku Rais wa Yanga, Hersi Said akikomenti kwa kuonyesha imoji za kucheka.

YAPELEKWA CAF Mwezi huu pia imezindua jezi zake itakazozitumia katika mashindano ya kimataifa lakini uzinduzi huo umekuja na mabadiliko ambayo imeyafanya ikiamini yanaweza kuwa chachu ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Mabadiliko hayo ni ya kutumia jezi zenye rangi nyeusi kwa mechi za nyumbani za mashindano hayo huku mechi za ugenini wakipanga kutumia jezi za kijani na jezi yenye rangi ya njano ikitumika kama ya tatu (third kit), iwapo watakutana na mazingira ambayo yatawafanya washindwe kutumia jezi za nyumbani au ugenini.

Mwanaspoti imethibitishiwa kuwa Yanga tayari imeshatuma taarifa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika(CAF), ikiwajulisha kuhusu jezi itakazozitumia katika hatua hii ya makundi na hata itakapofika kwenye fainali.

"Ni jezi ambazo tumekuwa na bahati nazo pindi tunapozitumia hivyo tumeamua katika mashindano ya kimataifa msimu huu, mechi za nyumbani tutatumia jezi nyeusi na ugenini tutavaa jezi za rangi ya kijani. Lakini kama mazingira yataruhusu hata huko ugenini, tutavaa nyeusi na tumeshawapa taarifa CAF kwa mujibu wa kanuni," kilifichua chanzo chetu .

REKODI YA KIBABE Baada ya mchezo huo wa ugenini dhidi ya Club Africain, Yanga imecheza mechi 17 za mashindano tofauti ambapo katika hiyo, michezo 10 ilicheza ikiwa imevaa jezi nyeusi na kupata ushindi yote ikifunga mabao 20 na kuruhusu bao moja tu, jezi za rangi ya kijani imecheza mechi sita ambazo imeshinda zote ikifunga mabao 21 na kufungwa matatu huku jezi ya njano ikichezea mechi moja na ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu Novemba 29, mwaka jana.

MSIKIE HERSI Rais Hersi, alipoulizwa kuhusu jezi nyeusi za Yanga na matokeo wanayoyapata anasema jezi ya rangi hiyo ndiyo pendwa kuanzia kwa mashabiki hadi wachezaji wao huku akidai ndio jezi inayoongoza kwa kufanya vizuri katika mauzo, ingawa hakutaka kusema kama ni ya bahati au la kwa upande wao.

"Siku chache baada ya kuzinduliwa na kuingizwa sokoni iliongoza kwa mauzo sokoni. Hadi sasa bado inafanya vizuri sana," anasema na kuongeza:

"Kuhusu kuvaliwa na timu na kupata matokeo mazuri sina jibu la moja kwa moja japokuwa naamini ni imani tu kwa sababu jezi haichezi.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: