Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam, Yanga safari ya gwaride

MUDATHIRI FEI TOTO Azam, Yanga safari ya gwaride

Sun, 20 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pale Chamazi kuna jambo. Yanga inarejea leo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikianzia hatua ya mtoano dhidi ya Asas ya Djibouti. Ndio safari ya zile tambo za gwaride la kukatiza Msimbazi inaanza rasmi leo.

Lakini, sio Chamazi tu, lakini kule Ethiopia katika Uwanja wa Abebe Bikila, matajiri wa Jiji la Dar, Azam FC watakuwa wakisaka alama tatu dhidi ya Bahir Dar Kenema kwenye mchezo unaopigwa kuanzia 9.30 alasiri.

Azam ilifanya mazoezi ya mwisho jana kwenye uwanja huo, huku ikitamba kuwa mastaa wake wote wako vizuri kiafya.

Kwa upande wa Yanga, mechi zote mbili zitapigwa Chamazi ambapo Yanga leo watakuwa ugenini. Ikiwa chini ya kocha mpya, Miguel Gamondi, Yanga itaingia na kikosi chenye sura mpya saba ikitaka kuthibitisha ubora wa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita mara baada ya kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa.

Macho ya wengi yatakuwa kwa mastaa sita ambao ni mabeki Kouassi Yao, Gift Fred, viungo Jonas Mkude, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na mshambuliaji Hafiz Konkoni ambao ndio wanaoweza kutumika kwenye mchezo wa leo.

Yanga itamkosa winga Msauzi Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ambaye licha ya uongozi kudai amepona, lakini juzi alfajiri alitimka kurudi kwao ikielezwa amekwenda kushughulikia pasi yake mpya ya kusafiria.

Ikiwa kwenye maandalizi AVIC Town - Kigamboni, Gamondi ametumia muda mwingi kuboresha muunganiko wa viungo washambuliaji na washambuliaji.

Akizungumzia mchezo huo ambao utaanza saa 11 jioni, Gamondi alisema wamepania kumaliza mechi hiyo leo.

Wapinzani wa Yanga, Asas walikuja nchini kwa mafungu wakiwa na msafara wa watu 23 pekee yaani mpaka viongozi.

Mara ya mwisho Asas kucheza Ligi ya Mabingwa ilikuwa 2018 ikitolewa hatua ya awali kwa jumla ya mabao 5-3 na Jimma Aba Jifar wakitangulia kupoteza kwao (1-3) kisha kulazimisha sare ya 2-2 ugenini.

Hesabu za makaratasi zinaibeba Yanga kushinda mchezo huo, lakini hata hivyo Gamondi ameonyesha kuwaonya wachezaji kutowadharau wapinzani akitaka waimalize mechi hiyo mapema.

Wageni watamtumia beki mkongwe Gilbert Kaze (38), raia wa Burundi aliyewahi kuitumikia Simba miaka ya nyuma.

Kaze ana kumbukumbu nzuri na Yanga akiwahi kuifunga kwenye sare ya mabao 3-3 akiwa Simba na leo atarudi kuwaongoza Asas kupambana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Kocha wa wageni hao, Mohamed Kader Ahmed alisema jana: “Tumekuwa tunafuatilia mechi zao (Yanga). Tunajua ni timu kubwa ambayo imetoka kufanya vizuri kwenye mashindano ya Shirikisho msimu uliopita. Tumejiandaa kupambana na timu ya ukubwa huo.”

“Tunajua ubora wa Yanga kwenye kikosi chao wanacheza vizuri kwenye ulinzi na kiungo chao lakini tunajua kwamba kwasasa hawako vizuri kwenye ushambuliaji.”

Gamondi alisema: “Hatuna taarifa za kutosha juu ya ubora wa wapinzani wetu, lakini tuko sawasawa kupambana. Maandalizi yanatupa imani kwamba tuko tayari kwa mchezo.”

“Jambo muhimu kwa wachezaji tumewasisitiza juu ya kutowadharau wapinzani wetu.”

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: