Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ateba kuiongoza Simba Jumamosi

Lionel Ateba Kimeeleweka Simba SC,  Kuwavaa Singida Big Stars.png Straika mpya Mkameroon, Leonel Ateba

Thu, 29 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Straika mpya Mkameroon, Leonel Ateba, anatarajia kuongoza safu ya ushambuliaji ya Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan itakayochezwa kesho kutwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam imefahamika.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema anatarajiwa kumtumia straika huyo aliyesajiliwa kutoka USM Alger ya Algeria ambaye hakumpanga katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Fountain Gate kutokana na taratibu za vibali kutokamilika.

Fadlu alisema kwa sasa taratibu zote za kumtumia mchezaji huyo zimekamilika hivyo ataongoza mashambulizi katika mchezo huo ambao ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya raundi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya.

"Sikumtumia sio kwa sababu za kiufundi, ila alikuwa na matatizo ya vibali, kwa sasa kila kitu kipo tayari, nitamtumia katika mchezo huo ili kumweka sawa, azoeane na wenzake kuelekea katika mechi yetu ya Kombe la Shirikisho," alisema kocha huyo.

Ateba ni mchezaji wa mwisho kusajiliwa na Wekundu wa Msimbazi, akiwa ni mbadala wa Freddy Michael, ambaye inasemekana kocha huyo hakuridhika naye, hivyo kuwataka mabosi wa klabu hiyo kumtafutia straika mwingine kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili.

Hata hivyo, Fadlu alisema pamoja na kutarajia kumchezesha straika huyo, pia atamchezesha Valentino Mashaka, nyota  ambaye ameanza kumpa mwanga mzuri katika kikosi chake.

"Steven Mukwala yeye amekwenda katika kikosi chake cha timu ya taifa ya Uganda, kwa mastraika nimebakia na Mashaka, atasaidiana na Ateba, ni straika mzuri sana na mmeona kila akitokea benchi anafunga katika michezo yote miwili ambayo amecheza," alisema kocha huyo.

Mashaka ambaye kabla ya mechi za Ligi Kuu jana alikuwa anaongoza kwa kupachika mabao, akiwa na mabao mawili, akiyafunga katika mechi mbili tofauti, dhidi ya Tabora United, Simba ikishinda mabao 3-0 na dhidi ya Fountain Gate, ikishinda mabao 4-0 na zote akitokea kwenye benchi.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amethibitisha Ateba kwamba ana kila kitu ambacho kinamruhusu kucheza, hivyo kuwataka mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kumuona kwa mara ya kwanza straika huyo akiwa na uzi mwekundu.

Ahmed alisema wameamua kuandaa mchezo huo wa kirafiki ili kuwajenga zaidi wachezaji wao kwa sababu wanahitaji kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa wanayoshiriki.

Wakati Simba ikijiandaa kucheza dhidi ya Al Ahly Tripoli huku Al Hilal nayo inajiandaa kucheza mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya San Pedro ya Ivory Coast, baada ya kuing'oa, Al Ahly Benghazi ya Libya, kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda bao 1-0 ugenini na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Juba, nchini Sudan Kusini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: