Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arafat: Tutawaweka wachezaji hoteli kali zaidi

Gsm 0 Arafat: Tutawaweka wachezaji hoteli kali zaidi

Sat, 27 May 2023 Chanzo: Mwanaapoti

Kitendo cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa ndege kwa ajili ya kuipeleka Yanga huko Algeria kwenye mchezo wa fainali ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, kumeipa jeuri zaidi timu hiyo hivyo lile fungu ambalo lingetumika kwenye usafiri limeingizwa kwenye matumizi mengine.

Yanga itakuwa na fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumapili ya Mei 28, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa huku wiki moja baadaye Juni 3, wakitakiwa Algeria kwa ajili ya kumalizana na USM Alger.

Makamu wa rais wa klabu hiyo, Arafat Haji alisema fedha ambazo awali ziliandaliwa kwa ajili ya safari ya kuifuata USM Alger ambazo ni zaidi ya Dola 100,000 (Sh230 milioni), watazitumia kuongeza hamasa na kuiweka timu kwenye hoteli nzuri ili wafanikishe jambo lao.

Arafat alieleza hilo juzi Jumatano kwenye mjadala maalumu ambao uliendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter na kuhusisha wadau mbalimbali ikiwemo Ofisa habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPBL), Karim Boimanda.

Katika mjadala huo ambao ulihusu hatua iliyofikia Yanga katika mashindano ya CAF, Arafat alisema, "Mpira kwa sasa ni sayansi na sio maneno tu na mambo mengine hivyo unahitaji wataalamu na watu wenye taaaluma katika uongozi na masuala mengine ya kitimu,"

“Wawekezaji na wadhamini wanahitajika kuendeleza kuwekeza nguvu kwenye soka la Tanzania ili tuweze kuendelea kuwa na timu bora na za ushindani;

“Pia klabu zinazoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuzitengea fungu kwa ajili ya kupunguza maumivu makubwa ya gharama za kufanikisha mashindano hayo;

"Mashindano ya kimataifa yanatumia gharama kubwa tunaishukuru Serikali kwa kutupa ndege ambayo itatupeleka kumaliza mchezo wa fainali dhidi ya USM Alger fedha iliyoandaliwa tutaitumia kuongeza hamasa na kuiweka timu kwenye hoteli nzuri ili wapate utulivu,” alisema Arafat.

Kiongozi huyo hakuishia hapo, alisema "Dola laki moja kwa safari moja ni gharama kubwa sana na sio chini ya michezo mitatu kwenda kucheza bado pia changamoto ya safari ndani ya Afrika tuna ndege chache za kwenda moja kwa moja kwenda baadhi ya nchi;

"Tunatumia saa 18 kusafiri mahitaji makubwa yanahitajika kuhifadhi timu kupumzika sehemu nzuri, chakula kizuri hivyo gharama ni kubwa ni timu chache Tanzania zinaweza kumu hivyo tunaomba bajeti kwa upande wa serikali ili timu ziweze kushiriki vizuri;

“Yanga tayari imekuwa chapa kubwa ya kuitangaza Tanzania hivyo mpira ukipewa kipaumbele ni biashara kubwa mfano usajili wa wachezaji wa kigeni lazima walipiwe vibali vya kuishi na kufanya kazi pesa inaingia Serikalini.”

Kwa upande wake, Boimanda alisema,"Mafanikio ya Yanga yanaongeza hadhi, thamani, heshima, mvuto na ushindani katika Ligi yetu. Ushiriki wao unawafanya watu kutoka mataifa mbalimbali kuifuatilia Ligi ya Tanzania ambapo ni nyumbani kwa Yanga jambo ambalo linafaida nyingi kwa Ligi yetu na Taifa kwa ujumla.”

Naye Mwandishi na mchambuzi wa michezo kutoka Mwananchi Communications Limited (MCL), Charles Abel alichangia mada hiyo kwa kusema,"Wachezaji wa kigeni wanawaamsha wazawa na kuwafanya kupambana zaidi ili wapate nafasi kikosini jambo ambalo ni faida kwa wao binafsi, klabu pamoja na timu yetu ya taifa kwani wanakuwa bora na ushindani unaongezeka,"

"Uwepo wa kina Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Yanick Bangala na Mamadou Doumbia unawafanya kina Shomari Kibwana, Ibrahim Bacca, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto kupambana zaidi ili wapate nafasi kwenye klabu na kupelekea kuwa na timu ya taifa yenye wachezaji wengi wazoefu,"

Akifafanua juu ya hatua ambayo waliwahi kuifikia Simba, Abel alisema,"Hatua ambayo Simba ilifika fainali ilikuwa mwaka 1993, likiitwa Kombe la CAF. Mwaka 2003 yalifanyika mabadiliko hivyo Yanga ndio timu ya kwanza kutoka Tanzania kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.”

Ramadhan Elias, ambaye naye ni Mwandishi wa Michezo, Mwananchi Communications Limited, alisema, "Yanga msimu huu imefanikiwa zaidi kwenye kujenga umoja kuanzia viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki. Hiyo ni moja ya sababu za kufikia mafanikio hayo.

Pia uongozi wa sasa wa Yanga umeitoa timu ofisini na kuiweka karibu na mashabiki jambo ambalo kila inapoenda ikutane na watu wengi wa kuisapoti na wao kujisikia sehemu ya timu yao kwa asilimia 100.”

Chanzo: Mwanaapoti
Related Articles: