Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wezi waua mtoto wakitaka pesa za TASAF

Kisu.jpeg Wezi waua mtoto wakitaka pesa za TASAF

Tue, 11 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanafunzi wa kidato cha tatu, Shule ya Sekondari Ally Mchumo, Tarafa ya Kipatimu, mkoani Lindi, Jamila Adamu (17), ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na watu waliovamia nyumba yao wakitaka wapewe fedha walizopokea kutoka Mfuko Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na viongozi wa Serikali ya Kijiji, Kata na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, tukio hilo lilitokea Juni 30, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumo, Abdallah Ngomba, amesema, tukio hilo lilitokea baada ya vijana wawili kuvamia nyumbani kwa mama wa marehemu Jamila, Manate Kikaka na kulazimisha wapewe fedha alizolipwa na TASAF.

Amesema siku ya tukio, Jamila na mama yake wakiwa ndani ya nyumba yao wamelala, vijana wawili aliowataja kwa majina, Nassoro Mailo na Abbasi Kapandaila, waliingia ndani mwao na kuanza kupekua wakitafuta fedha ndipo Jamila aliposhtuka kutoka usingizini na kupiga kelele za wezi.

Ngomba amesema kitendo cha kupiga kelele za kuomba msaada huo, vijana hao waliokuwa na silaha zenye ncha kali walimchoma mwanafunzi huyo kwenye mbavu na kutokomea zao kusikojulikana.

“Wakati wakipekua mule ndani, Jamila aliamka na kuuliza nyie kina nani? Wakamwambia awape fedha alizolipwa na TASAF,” amesema Ngomba.

Ofisa Mtendaji Kata ya Chumo, Marachius Mutalemwa, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba watuhumiwa wote wawili wamekamatwa na kufikishwa kituo cha polisi, mji mdogo Masoko, Wilaya ya Kilwa wakiendelea kuhojiwa.

Mutalemwa amesema hilo ni tukio la pili kufanywa na watuhumiwa hao, kwa kuwa wiki mbili zilizopita wanadaiwa kuiba Sh. 80,000 kwa wazee wengine waliokuwa wamelipwa fedha zinazotokana na TASAF.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Pilli Mande, amekiri kutokea kwa mauaji hayo na kueleza tayari vijana wawili wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya mwanafunzi huyo wanawashikilia kwa mahojiano.

Mande amesema watuhumiwa wote kwa pamoja wanatarajia kufikishwa mahakamani baada ya kukamilisha kazi ya upelelezi wa tukio hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: