Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wawili wa darasa la kwanza wauawa kwa kushambuliwa na fisi

Fisiiii Watoto wawili wa darasa la kwanza wauawa kwa kushambuliwa na fisi

Fri, 28 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanafunzi wawili wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Ilumya wilaya ya Magu mkoani Mwanza wamefariki katika matukio mawili tofauti baada ya kushambuliwa na fisi wakati wakiwa njiani kwenda shuleni.

Matukio hayo yametokea Aprili 27 na 28, 2023 kati ya Saa 12 na Saa 1 asubuhi katika kijiji cha Ilumya wilayani humo, ambapo waliofariki ni Saraha Ncheye (7) mkazi wa kitongozi cha Sanganyika kijiji cha Nsola na Elizabeth Emmanuel wa kijiji cha Ilumya –Busega.

Sarah Ncheye ameuawa leo Aprili 28, 2023 katika kitongoji cha Kilulu baada ya kushambuliwa na fisi Saa 1 asubuhi wakati akienda shuleni ambapo alikuwa akisoma shule iliyo jirani na kijiji cha Ilumya wilayani Busega.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema Sarah alikutana na fisi huyo na kabla ya kushambuliwa alisikika akipiga kelele za kuomba msaada ndipo wakawahi eneo hilo na kumkuta fisi ameshamshambulia na kukimbia naye akiwa amemng’ata kichwani ananing’inia.

Kaka wa marehemu, Jackson Ncheye amesema alikuwa njiani anakwenda shambani kulinda mpunga dhidi ya ndege waharibifu ndipo akasikia mayowe kisha kumuona fisi anakimbia.

“Nilianza kumfukuza nikidhani amechukua mifugo, lakini baadaye nikaitwa na kukuta mdogo wangu ameshauawa baada ya kujeruhiwa vibaya kichwani na mikono,”amesema

Shuhuda mwingine, Mariam Leonard amesema “Nilikuwa nakwenda shambani kuchimba viazi nikakutana na fisi akiwa na mtoto anakimbia analia nikamkimbiza lakini akaanza kunifuata mimi nikakimbia kwenda kwa watu kuomba msaada wa kumuokoa, tulivyorudi tukakuta mtoto ameshafariki,”

Mwalimu wa shule ya msingi Ilumya, Stephano Mangilima amesema matukio hayo ya mara kwa mara yanasikitisha nakuwaomba wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule ili wasidhurike huku akiitaka Serikali ya kijiji kuwawinda wanyama hao.

“Ni tukio la kuhuzunisha na kushangaza, mtoto alikuwa na maendeleo mazuri darasani, wito wangu kwa wazazi kwakuwa matukio haya yanajirudia tuombe wanaoishi maeneo ya mbali watu wazima wawe wanawasindikiza watoto shuleni na viongozi wa vijiji watafute njia mbadala za kumaliza tatizo hili kwani tutaendelea kupoteza watoto,” amesema Mangilima

Mwenyekiti wa kijiji cha Nsola, Damian Kabudu amesema baada ya kupata taarifa za kushambuliwa kwa mtoto huyo aliyekuwa amejeruhiwa vibaya kichwani huku kiganja chake cha mkono wa kushoto kimekatwa, aliwajulisha idara ya wanyamapori ambao walifika na kutoa msaada wakishirikiana na wananchi.

Diwani wa kata ya Lubugu, Lucas Ntingi amesema matukio ya fisi kuwashambulia watoto yameongezeka katika vijiji vya Nsola na Ilumya ambapo Aprili 24 mtoto, Paul Elias (5) alishambuliwa na fisi katika Kijiji cha Nsola na  anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Magu, huku akizitaka mamlaka kuwawinda fisi hao ambao wamegeuka tishio kwa watu.

Jeshi la Polisi Wilaya ya Busega lilifika katika tukio hilo na kushughulikia taratibu mbalimbali kisha mwili wa marehemu kukakabidhiwa kwa familia kwa ajili mazishi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: