Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi waandamana wakitaka wapewe mtuhumiwa aliyechinja mtoto

Babati Maandamano WA0033 Wananchi waandamana wakitaka wapewe mtuhumiwa aliyechinja mtoto

Thu, 22 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamia ya wakazi wa Kata ya Magugu, wilayani Babati Mkoa wa Manyara wameandamana na kufunga Barabara kuu ya Babati-Singida kwa saa nne wakishinikiza kupatiwa mtuhumiwa anayedaiwa kumchinja mtoto wa miaka saba.

Watu hao walikuwa wanataka wapewe mtuhumiwa wa mauaji ya mtoto huyo Maria Chacha (7) mwanafunzi wa Shule ya awali na Msingi Mapea ambaye anadaiwa kuuawa kwa kuchinjwa shingo na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.

Hata hivyo, askari Polisi wa kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) kutoka Babati na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi walifanikiwa kuwatawanya watu hao baada ya kupiga mabomu ya machozi.

Vurugu hizo zimetokea leo Jumatano Februari 21, 2024 mji mdogo wa Magugu na mtoto huyo aliuawa jana Jumanne, Februari 20, 2024 kwa kilichodaiwa kuwa alidanganywa anakwenda kupewa matunda ya zambarau shambani.

Kamanda Katabazi amewataka wakazi hao kutawanyika na kuwachia askari wake wafanye kazi yao kwani mtuhumiwa ameshakamatwa.

"Msitake kuchukua sheria mkononi, tuachieni tufanye kazi yetu kwani mtuhumiwa tumeshamkamata na tutamfikisha mahakamani ili akajibu shitaka la mauaji ya huyo mtoto," amesema.

Mmoja kati ya waliofunga barabara hiyo, Hassan Mussa amesema wanamtaka mtuhumiwa huyo aliyepo Polisi anayedaiwa kumuua mtoto huyo kikatili ili nao wamuue, kwani amefanya mauaji kwa kiumbe asiye na hatia.

"Huyu jamaa aliwachukua watoto watatu akawadanganya anakwenda kuwapa zambarau ila wengine walitembea na kuona ni mbali wakarudi,  akambeba Maria na kisha kumuua," amedai.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mapea, Philemon Mbogo amesema mtoto huyo alichinjwa shingoni na kiwiliwili chake kutupwa katika shamba la miwa karibu na mto.

"Matukio ya watu kuuawa kwenye eneo hilo yanatokea mara kwa mara kwani miili miwili ilishapatikana na pia kuna mtoto alipotea hadi sasa hajaonekana," amesema Mbogo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: