Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchunguzi washika kasi tuhuma mafunzo 'ushetani'

Nurdin Babu Wef.jpeg Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku chache baada ya uongozi wa Wilaya ya Same kusitisha mafunzo kwa walimu yaliyodaiwa kukiuka maadili ya kitanzania, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema wameongeza nguvu kuchunguza suala hilo.

Amesema Katibu Tawala wa Mkoa huo, Tixon Nzunda ni sehemu ya timu ya uchunguzi huo na jana alikuwa safarini kwenda wilayani Same kwa lengo la kushughulikia suala hilo.

Juzi, iliripotiwa namna Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Same iliyolazimika kuingilia kati na kusitisha mafunzo hayo yaliyokuwa yanatolewa kwa walimu 244 na taasisi isiyo ya kiserikali (jina tunalo) baada ya kubaini dosari, ikiwamo vitabu vinavyotumika kufundishia kuwa na viashiria vya maadili yasiyofaa.

Mafunzo hayo yalikuwa yalikuwa yanatolewa kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo, yakipewa jina la 'Mafunzo ya Afya ya Jamii, Afya ya Uzazi na Uhusiano'.

Mkuu Mkoa (Babu), katika mazungumzo na Nipashe jana, alisema: "Kamati ya Usalama ya Mkoa tunalijua hilo suala, na Katibu ameondoka leo (jana) Aprili 20 kuelekea wilayani Same kwa ajili ya kufanyia kazi suala hilo.

"Nilisahau kumuuliza kama kuna tume yoyote imefika kwa ajili ya suala hilo ila kama ipo ni kawaida kwa utendaji wa kazi wa serikali.

"Mimi nilikuwa safari, nilirejea jana (juzi), hivyo tunalifanyia kazi jambo hili kwa mikakati ya siri na ya wazi na litakapokamilika, tutatoa taarifa," alifafanua Babu.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema ni wajibu wa serikali kuhakikisha hakuna vitendo vya uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa maadili, akitoa angalizo kwa watu wanaonung'unika kuwa walimu hao wameonewa, akisisitiza "waache mara moja".

Katika hilo, Babu alisema "Nimesikia kuna manung'uniko na malalamiko kwa baadhi ya walimu, wakiona walimu wale wameonewa, lakini niwaombe walimu wawe watulivu wakati Katibu Tawala wa Mkoa anashughulikia jambo hili na hakuna hata upande mmoja utakaoonewa.

"Lengo sio kumwonea mtu ila tunataka walimu wetu fursa nzuri zinapokuja, waweze kunufaika nazo, na wasinufaike na mambo mabaya yatakayokuja kuharibu watoto," alisema.

Kiongozi huyo wa mkoa pia aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoko mkoani Kilimanjaro, kutii sheria zote, hasa wale wanaojihusisha na utoaji wa elimu kwa jamii na kuahidi kutolivumilia shirika lolote litakalovunja sheria.

"Ninaruadia, kuna vitabu ambavyo vimekatazwa na kupigwa marufuku na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na zipo baadhi ya NGO bado zinavitumia, Niwaombe kuacha mara moja na kufuata utaratibu. Wasipofuata utaratibu, hatutowavumilia," alionya.

CWT WAFUNGUKA

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Kilimanjaro, Daudi Mafwili, alisema watatumia mifumo yao kuendelea kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa walimu ili kunusuru jamii ya kitanzania.

"Wanachama wetu wamekuwa wahanga (waathirika) wakubwa wa kila kitu kipya kinachokuja kwenye jamii hasa chenye maslahi, walikuja watu wa QNET na DECI na sasa wamekuja hawa jamaa wenye mambo yao, bado wanaonekana walimu ndio kundi kubwa la waathirika. Tutatumia vikao na makundi yetu kuendelea kutoa elimu kwa wanachama wetu.

"Ila hatutowavumilia wale wote serikali itakaobaini walishiriki jambo hili kwa nia ya kuharibu kizazi cha watanzania," Mafwili alihadharisha.

Mwezi Januari mwaka huu, Nipashe iliripoti kuhusu baadhi ya watendaji wa shule binafsi mkoani Kilimanjaro kuwafundisha kulawitiana wanafunzi, hasa wanaolala bwenini. Serikali iliunda timu ya kuchunguza suala hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: