Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taharuki: Watatu wakifa kwa kula nyama msibani

IMG 20221012 WA0047 001 768x576 Nyama Watatu wakifa kwa kula nyama msibani

Tue, 23 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu watatu wakiwemo mume na mke wamefariki dunia baada ya kula nyama msibani inayodhaniwa kuwa na vimelea vya ugonjwa wa kimeta katika Kijiji cha Msaranga, Kata ya Kisale Msaranga, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Kufuatia tukio hilo lilitokea Mei 4, watu 188 waliokuwepo msibani hapo tayari wamepewa dawa kinga, huku wengine 15 wakiumwa matumbo, kuhara na kutapika huku baadhi wakihusiaha na maradhi ya mifugo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, tayari timu ya matabibu kutoka mkoani wapo katika kata hiyo kufuatilia tukio hilo.

Taarifa za tukio hilo zimeibuliwa na Diwani wa kata hiyo, Mathias Assenga aliyesema tukio hilo limezua taharuki katika eneo la hilo kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuhara na kwamba wengine walioshiriki katika mazishi hayo wanaendelea kuchunguzwa kwa ukaribu.

"Kulikuwa na mazishi mahali hapa kwenye kata yangu, ambayo yalifanyika kwa mzee mmoja aliyekuwa amefiwa na kijana wake, sasa wakati wa mazishi kuna mama alikuwepo anahudumia kule jikoni, ambaye pia alichukua na chakula na kupeleka nyumbani baada ya shughuli ya mazishi kumalizika.

"Chakula hicho baada ya kupeleka nyumbani alikula yeye na mume wake, mwali wake pamoja na mjukuu wake aliyekuwepo nyumbani hapo siku ya Mei 4.

“Siku iliyofuatia ambayo nilikuwa Ijumaa huyu mama alijisikia vibaya na siku ya Jumapili alipoenda hospitali alizidiwa na Jumatatu ya Mei 8 alifariki dunia.

"Lakini wakati huo tayari mume wake naye alikuwa ameshaanza kuharisha na alikuwa hospitalini na hakuweza kumzika mke wake.Alhamisi ya Mei 11 mume wake naye akafariki na mwali (mkwe) wake naye pia akawa amelazwa hospitalini.”

Alisema kufariki kwa watu hao kumeleta taharuki kubwa kwenye kata hiyo baada ya kijana mwingine aliyekuwa akihudumia chakula katika msiba huo kufariki dunia.

"Sasa hii imeleta taharuki kidogo kwa sababu kuna kijana mwingine wa familia nyingine ambaye naye alikuwa anahudumia pale msibani naye akawa amekufa na alizikwa Mei 17 na wale wote ambao walikuwa wanaharisha walielekezwa kwenda hospitali," alisema.

Alisema katika kata hiyo watu 15 ambao walikuwa wanahara walikwenda hospitali na kupewa tiba na kurudi na kwamba kinachofanyika kwa sasa ni kuendelea kufuatilia hali zao.

Wagonjwa wasimulia

Mkazi wa Kijiji cha Msaranga, Monika Tesha ambaye amelazwa katika Hospitali ya Ngoyoni alisema baada ya kula nyama msibani alishikwa na tumbo la kuhara na kutapika na kuwa hali yake ilikuwa mbaya sana mpaka alipowahishwa hospitali.

"Nilikula nyama msibani baada ya kutoka hapo nikaanza kuumwa tumbo na kuharisha choo chenye damu, usiku wa Ijumaa kichwa kikaanza kuuma, nikabanwa na kifua na mgongo huku tumbo linauma, ndipo ikabidi niletwe hapa Ngoyoni (kituo cha afya) maana hali yangu ilikuwa si nzuri," alisema.

“Tulikula nyama ya ng’ombe aliyechomwa sindano nyumbani akapelekwa buchani, wakachinja wakaleta msibani , tunaiomba Serikali hawa watu wanaofanya hivyo kutuangamiza, mhusika atafutwe ahojiwe ili iwe fundisho kwa wengine maana sisi ndio tunaoumia,” alisema

Getruda Kalisti, mkazi wa Msaranga ambaye alikuwa amelazwa katika kuituo hicho, alisema hakushiriki msiba lakini chakula ambacho mama mkwe wake alileta kutoka msibani familia nzima walikuwa usiku na wote waliumwa na kwamba amepoteza wakwe zake baada ya kula nyama hiyo.

"Mama ndiye aliyekuwa msibani na alikuwa kwenye kamati ya chakula kwenye huo msiba na alituletea chakula nyumbani baada ya kula, mama siku ileile alianza kuumwa. “Alikuwa anaharisha sana na ilipofika Jumapili hali yake ikazidi kuwa mbaya zaidi akapelekwa Hospitali ya Huruma lakini hali ilizidi kuwa mbaya baada ya hapo Jumatatu akawa amefariki.

"Baba naye alianza kuharisha kama mama akawa amepelekwa Huruma hali yake ilikuwa si nzuri sana na baadaye naye alifariki dunia. Wakati huo na mimi nilikuwa nimeshaanza kuharisha, hali yangu ilikuwa si nzuri sana, lakini namshukuru Mungu baada ya kupata matibabu ninaendelea vizuri, japo nimepoteza mama na baba mkwe wangu,” alisema.

Alisema mtoto wake ambaye pia alikula nyama hiyo alipatwa na tatizo kama hilo lakini aliwahishwa hospitali anaendelea vizuri japo alikuwa anaumwa tumbo.

Wataalamu watumwa

Akizungumzia tukio hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RMO), Dk Jairy Khanga alisema timu ya mkoa ipo katika maeneo hayo na kwamba watu 188 katika eneo hilo la msiba tayari wameshapewa dawa kinga kwa lengo la kuwakinga kama watakuwa walipata tatizo.

"Tulipoenda kuchunguza mpaka sasa huwezi kuthibitisha hiki ndiyo sababu, lakini tulipofuatilia habari zao hospitali ni kwamba walikuwa wanaumwa tumbo na kutapika na wote walikuwa kwenye msiba. Kwa hiyo mmoja baada ya kula kile chakula tumbo lilianza kumuuma na kutapika na akafariki na mwingine hivyo hivyo.

"Waliopewa dawa kinga mpaka sasa ni 188 katika Hospitali ya Huruma na vituo vya afya Karume na Ngoyoni na mpaka sasa tunafuatilia na tayari timu iko huko inafuatilia pamoja na kutoa elimu kwenye jamii,” alisema.

Pamoja na mambo mengine Dk Khanga alisema mpaka sasa hakuna sampuli ambayo imechukuliwa kupelekwa maabara ili itoe majibu kwamba ni kitu gani kwani tukio limetokea Mei 4 mwaka huu.

Wizara ya Mifugo

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Benezeth Malinda, alisema watatuma timu ya watalaamu wa maabara ya mifugo kwenda Rombo ili kujua chanzo cha mnyama ni wapi.

Alisema baada ya kupata majibu hayo watayalinganisha na yatakayotoka hospitalini. “Pia tutataka kujua huyu mnyama alichinjwa kwa utaratibu gani, maana kama alihusika mtaalamu wetu wa mifugo, alitakiwa kujua mapema ikiwemo viasharia vya kuona mnyama hakuwa salama. Au alichinjwa kienyeji kwa kutumia wazee au vijana? Alisema Dk Benezeth Malinda,.

Alisema uchunguzi huo utatusaidia pia kutoa elimu kwa wananchi kwamba wanapokuwa na sherehe au misiba, wanapaswa kufuata utaratibu ikiwemo kuhusisha ofisa mifugo kwa chakula kinachohitaji watu wengi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipotafutwa kwa simu, hakupatikana kwa kuwa simu yake iliita bila kupokelewa.

Hata hivyo, Englibert Kayombo, kaimu mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya alisema wanafuatilia wakipata tarifa wataueleza umma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: