Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndege ya Jeshi yaanguka Ziwa Victoria Bukoba

Ndege Jwtz Ndege ya Jeshi yaanguka Ziwa Victoria Bukoba

Thu, 20 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ndege ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) iliyokuwa na marubani wawili imeanguka ndani ya maji ya Ziwa Victoria, hatua chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba.

Tukio hilo limetokea Saa 3:30 asubuhi ya leo Julai 20, 2023 na kuibua hofu na taharuki miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba ambao wamerejewa na kumbukumbu ya tukio la ndege ya abiria ya kampuni ya Precision Air kuumbukia ndani ya Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26.

Katika tukio hilo la Novemba 6, 2022 ndege hiyo ya Precision Air namba ATR 42-5H PWF ilitumbukia ziwani baada ya marubani kushindwa kuona njia ya kutua kutokana na hali mbaya ya hewa.

Akizungumzia tukio la leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasia Chatanda amesema ndege hiy ya Jeshi yenye namba JW 9127 ameanguka wakati marubani wake wawili walipokuwa kwenye mazoezi ya kawaida.

Kamanda Chatanda ametaja marubani hao ambao wamekimbizwa kwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kuwa ni Leonard Nkundwa (45) na Alex Venance (30).

Theophilda Kamaleki, mkazi wa mtaa wa Nyamkazi Manispaa ya Bukoba ambaye ni miongoni mwa walioshuhudia ajali hiyo amesema mwanzoni alishuhudia ndege mbili ndogo zikizunguka na kuondoka katika anga la mji wa Bukoba kabla ya ndege moja kuonekana kuangukia ziwani.

‘’Tangu jana (Julai 19, 2023) niliona ndege ndogo zikipita juu ya anga la mji wa Bukobaya; leo asubuhi pia nimezishuhudia ndege hizo mbili zikipita angani kabla ya kusalia ndege moja. Baada ya muda tukapata taarifa kuwa kuna ndege imeanguka ziwani; lakini wengine wakadai ni mazoezi ya utayari wa uokoaji wakati wa ajali,’’ amesema Theophilda

Mmoja wa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Athman amesema yeye alikuwa kati ya watu wa kwanza kukimbilia eneo la uwanja wa ndege baada ya kuona ndege hiyo ikianguka ziwani lakini wakazuiwa kusogea karibu na maofisa wa jeshi waliokuwa wakifanya jitihada za kuwaokoa wenzao.

‘’Walituzuia kusogelea eneo ndege ililopoangukia; mwanzoni tulijua wanafanya mazoezi lakini baadaye ikathibitika ni ajali ya kweli. Naona tayari wamefanikiwa kuivuta kutoka ndani ya maji ya Ziwa Victoria,’’ amesema Athman

Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege (TCAA), Hamza Johari kupata taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo zinaendelea baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: