Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili uliofukuliwa na kunyofolewa sehemu za siri, wazikwa tena

Kaburi Msd Mwili uliofukuliwa na kunyofolewa sehemu za siri, wazikwa tena

Tue, 21 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika hali isiyo ya kawaida kaburi la marehemu Ruben Kasala (73) mkazi wa kijiji cha Kasokola wilayani Mpanda aliyezikwa Machi 18, 2023 saa 12:00 jioni baada ya kufariki kwa ugonjwa wa kisukari, limefukuliwa na watu wasiofahamika usiku wa kuamkia Machi 19, 2023 kisha mwili wake kunyofolewa sehemu zake za siri.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi 20, 2023 kijijini hapo mtoto wa marehemu Ruben Kasala amesema tukio hilo limezua sintofahamu kwa wanafamilia baada ya marehemu kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama kinachohusishwa na imani za kishirikina.

“Baba alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu, amepata matibabu baadaye umauti ukampata, tumemzika vizuri, jana asubuhi kama ilivyo desturi yetu tukaenda kuangalia kaburi,” amesema.

“Baada ya kufika tukakuta kaburi wazi limefukuliwa, jeneza linaonekana na mguu wake mmoja upo nje tukashangaa, nilitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa akaja akaita polisi,” amefafanua.

Aidha amesema polisi walipofika eneo hilo waliamuru jeneza litolewe kisha wanafamilia waliitwa kuangalia mwili, walichobaini alikuwa amekatwa sehemu zake za siri.

Amesema baada ya polisi kujiridhisha waliamuru mwili kuzikwa kwa mara ya pili kitendo ambacho kimeleta hofu na huzuni kwa wanafamilia.

“Hatuna ugomvi wowote tofauti na migogoro midogo tu na alikuwa ameoa wanawake wawili lakini waliachana, mtu aliyefanya kitendo hiki atakuwa anataka utajiri kwa njia za kishirikina alaniwe kabisa tumeumia sana,” amesema.

Mmoja wa majirani wa familia hiyo Janeth Kapaya amesema marehemu wameishi naye vizuri alikuwa mwenye busara na hekima na mcha Mungu.

“Kimetusikitisha kitendo hiki tunaomba watu wenye tabia ya kupenda utajiri kwa imani za kishirikina waache kwasababu wanatenda dhambi na sheria hairuhusu,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasokola, Calos Joackim amekiri kutokea tukio hilo na kwamba alipokea taarifa kutoka kwa wanafamilia kisha kufika eneo hilo.

“Niliwaita polisi wakaja tukafukua tukakuta katolewa sehemu za siri, wakaruhusu kuzika tena, hiki kitendo hakijawahi kutokea katika eneo langu lakini aliyefanya hivyo siyo mkazi wa hapa atakuwa mgeni nalaani vikali kitendo hiki,” amesema Joackim.

Jeshi la Polisi mkoani Katavi limethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba linaendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na ukatili huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: