Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti ashtakiwa kwa kuzuia ujenzi wa shule

RC Serukamba2da1cd5c47f8 780x470 Mkuu wa Mkoa Singida, Peter Serukamba.

Tue, 6 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, amemshtaki Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimihi, Ramadhani Ally, kwa Mkuu wa Mkoa Singida, Peter Serukamba, kwamba amekuwa kikwazo kwa kuzuia wananchi kushiriki ujenzi wa Shule ya Msingi Murya.

Muragili aliwasilisha malalamiko hayo juzi baada ya Serukamba kufanya ukaguzi katika shule hiyo. Alisema  kusuasua kwa ujenzi huo kumesababishwa na mwenyekiti ambaye anahamasisha wananchi wa vitongoji viwili wasishiriki nguvu kazi.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa nilikuja hapa Mei 20, 2023 kukagua nikabaini kikwazo katika mradi huu ni Mwenyekiti wa Kijiji ambaye alikuwa anazuia shule kujengwa  hapa, lakini wewe niachie hili suala huyu ni saizi yangu nitapambana naye," alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ramadhani Ally, alipopewa nafasi ya kuongea alijibu kuwa hajapinga ujenzi wa shule isipokuwa eneo inapojengwa kulikuwa na mgogoro hali iliyosababisha mvutano wa wananchi wa vitongoji vinne vinavyounda kijiji cha Msimihi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Serukamba, alisema ni jambo la kushangaza kwa wananchi kutoshiriki nguvu kazi katika ujenzi wa shule hiyo wakati serikali imewarahisishia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi huo.

Serukamba alisema ili miradi iweze kukamilika kwa wakati wakurugenzi wa halmashauri wawapangie wakuu wa idara kila mmoja kusimamia mradi mmoja inayotekelezwa hivi sasa na wawe wanatoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi kila siku, kwamba ikamilike kabla ya Juni 30 mwaka huu.

Alisema ujenzi wa miradi unasuasua katika baadhi ya halmashauri kwa sababu kazi ya kuisimamia wameachiwa walimu na kamati za shule.

Mkuu wa mkoa alisema hapendi kuona fedha zilizoletwa katika mkoa huu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo zinarudishwa baada ya mwaka wa fedha kumalizika kwa kushindwa kukamilisha miradi.

Kutokana na hali hiyo,  aliagiza kila mkuu wa idara kukabidhiwa mradi wa kuusimamia ili ikamilike kabla ya Juni 30, mwaka huu.

‘Walimu kazi wanayojua ni kufundisha tu hivyo kusimamia miradi mikubwa wanaweze wasimudu vyema jukumu hilo, hivyo iwapo wakuu wa idara watapewa kazi kuisimamia watasaidia kuweka mipango mizuri ya ujenzi na kuwa daraja kati ya halmashauri, mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa," alisema.

Serukamba aliambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatma Mganga, ambaye alisema serikali imepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hivyo isimamiwe, wananchi waendelee kuhamasishwa kujitolea nguvu kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: