Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yabomoa nyumba na kumjeruhi

Mvua Kuendelea Kunyesha Kwa Wiki Mbili | Mvua yabomoa nyumba na kumjeruhi

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mvua za masika zinazoendelea kunyesha maeneo tofauti nchini, zimesababisha athari katika mikoa mbalimbali ikiwamo kujeruhi, nyumba kadhaa kubomoka na baadhi ya barabara kukata mawasiliano.

Katika tukio lililotokea jana, Msimbazi Magharibi, Tabata jijini Dar es Salaam, mkazi wa eneo hilo, Kondo Musa (28), amenusurika kifo baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba aliyokuwa anaishi na wapangaji wenzake wanne.

Akizungumza nasi, majeruhi huyo alisema alirudi nyumbani kwake juzi asubuhi kwa ajili ya kubadilisha nguo ndipo muda mfupi baadaye mvua ikanyesha akiwa amelala.

“Nikiwa nimelala, nilishtuka baada ya kusikia kishindo na ukuta umenijeruhi maeneo ya tumboni na miguuni,” alisema.

Mjumbe wa Shina Namba 11, Nungano Kivuruge, alisema nyumba iliyoanguka ilikuwa na ufa wa muda mrefu.

“Tukio hilo limetokea kwenye eneo langu. Nyumba ina vyumba vinne, mwenye nyumba anafahamika kwa jina moja Mhagama,” alisema.

Mjumbe wa Mtaa Msimbazi Magharibi, Beth Joel, alisema: “Nikiwa ofisini alikuja mjumbe kutoa taarifa ya kuanguka kwa nyumba hii kutokana na mvua iliyonyesha leo (jana).”

Alisema ndani ya nyumba hiyo, kulikuwa na wapangaji wengine watano ambao wao walifanikiwa kukimbia baada ya kusikia kishindo cha kuanguka kwa ukuta huo. Alisema viongozi wa mtaa wamekubaliana kukutana na kukagua nyumba zote ambazo zina nyufa ili kuwashauri wakazi wake wasilale humo.

Fatuma Said, mmoja wa wapangaji wa nyumba hiyo, alisema wakati akiendelea kupika chumbani kwake, alisikia kishindo cha ukuta ukianguka.

"Nilipotoka nje nikakuta ukuta wa chumba cha nje umeanguka na huyu kaka alikuwa amelala ndipo wapangaji wakakimbilia nje,” alisema.

Wakati hayo yakitokea Dar es Salaam, huko Tarafa ya Mukulat iliyoko Arumeru mkoani Arusha, mvua zilizonyesha juzi zimebomoa makazi na nyumba zingine kujaa maji na wananchi wake kukosa mahali pa kukaa.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda, alisema jana kuwa kutokana na tishio la mvua hizo, Jeshi la Polisi limemwarifu kwamba mpaka sasa hakuna mtu aliyepoteza maisha.

“Kumekuwa na uvumi uliosababisha taharuki kwa baadhi ya wananchi kwamba mvua hizi zimesababisha vifo vya watu watatu waliokuwa wamepanda pikipiki moja baada ya chombo hicho kukutwa kikiwa kimefunikwa kwenye kifusi cha tope katika eneo la Kibaoni, Ngaramtoni,” alisema.

Alisema uchunguzi uliofanywa na polisi, umeonyesha hakuna mtu aliyepoteza maisha na mmiliki wa pikipiki hiyo amethibitisha kwamba watu hao walijiokoa.

“Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kumtafuta mmiliki halali wa pikipiki hii na alithibitisha kuwa watu hawa ambao ni wanaume wawili walifanikiwa kujiokoa wenyewe na watatu ambaye ni mwanamke aliokolewa na wasamaria wema, usiku wa Machi 23, mwaka huu,” alisema.

Alisema kulingana na tathmini iliyofanywa na wataalamu waliotembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko, uwapo wa uchafuzi wa mazingira, hasa utupaji wa taka ngumu ambazo zimesababisha mitaro kuziba na kushindwa kupitisha maji.

Mvua hizo zimesababisha uharibifu wa mali za wananchi katika Kata za Oltrumet, Oloirien, Sambasha, Olmotonyi na Kimnyaki, ingawa serikali haijaweka hadharani taarifa ya idadi ya makazi yaliyoharibiwa.

Mkoani Iringa, mvua zilizonyesha juzi kwa zaidi ya saa nne katika mji wa Iringa, zimesababisha athari ya miundombinu eneo la Mkimbizi Bima na baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Iringa baada ya barabara inayounganisha kata hiyo na Mtwivila kuwa hatarini kukatika.

Wakazi wa eneo hilo, Silla Kimwanga na Sara Sanga walisema mvua hizo zimesababisha sehemu kubwa ya barabara kukatika.

Kimwamga alisema eneo ambalo barabara hiyo inakaribia kukatika awali Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Manispaa ya Iringa, walijenga mtaro kwa kuweka karavati.

Alisema eneo hilo kuna karavati ambalo limeziba halipitishi maji hivyo kusababisha kupita juu ya barabara na kuleta madhara makubwa maeneo hayo.

“Kero hii ni kubwa kwetu na barabara hii inaunganisha Kata ya Mtwivila na endapo haitafanyiwa kazi mvua zikiendelea upo uwekezano wa watumiaji wake kukosa mawasiliano,” alisema.

Diwani wa Mkimbizi, Eliud Mvella, alisema eneo hilo linahitaji ufumbuzi kwa kuwa ni moja ya barabara muhimu.

Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Juli Sawani, alisema sehemu kubwa ya manispaa imekumbwa na madhara na tathmini inafanywa na madiwani wa kata husika.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Iringa, Barnaba Jabiry, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, alikiri kuwapo kwa madhara ambayo TARURA imeyapata kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huku akisema baadhi ya barabara zimefungwa kutokana na kukatika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: